Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Samaki wazua hofu Dar
Samaki wazua hofu Dar
By Habari Tanzania | Published  04/15/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:
na Happiness Katabazi


WAKATI watu wengi nchini wanategemea samaki na kuku kama kitoweo kikuu baada ya kuibuka kwa homa ya bonde la ufa (RVF), Tanzania Daima imebaini kuwa, samaki ni kitoweo hatari kwa maisha ya binadamu.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kwa ujumla kuwa, maisha ya Watanzania wengi, hasa wakazi wa Dar es Salaam, yapo hatarini kutokana na kulishwa vyakula vyenye kemikali na vimelea vinavyoweza kuwasababishia magonjwa ya hatari kama vile kansa.

Hali hii inajitokeza wakati RVF, ambayo huambukiza binadamu kupitia mazao ya wanyama kama ng’ombe, mbuzi na kondoo, bado ikiwa ni tishio nchini.

Aidha, watu wengi waliamua kuacha kula nyama kwa muda na kukimbilia kwenye kuku na samaki, lakini uchaguzi wao hivi sasa unaonekana kuwa unaweza kuwaletea matatizo makubwa.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa samaki hatari zaidi kutumiwa na binadamu kama kitoweo, ni wale wanaovuliwa katika Ziwa Victoria na kusafirishwa hadi jijini Dar es Salaam na maeneo mengine nchini.

Tanzania Daima limedokezwa na wataalamu wa afya kuwa, wafanyabiashara wa samaki wanatumia dawa zinazotumika kuhifadhia maiti za binadamu ili kuwahifadhi samaki hao wasiharibike haraka wanaposafirishwa kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa kwenda kwenye mikoa mingine.

Baadhi ya madaktari na wauguzi wa jijini Dar es Salaam waliozungumza na gazeti hili (majina tunayahifadhi), walilithibitishia Tanzania Daima kuwa, vifo tayari vimeshatokea kutokana na watu kula samaki waliohifadhiwa kwa kutumia dawa hizo.

Waliitaja dawa hiyo kuwa ni Fomalin, ambayo inatumiwa zaidi kwa kuhifadhia maiti ili zisiharibike haraka.

Wataalamu wa afya wa Hospitali ya Taifa Muhimbili waliozungumza na Tanzania Daima, walieleza kuwa, dawa aina ya Fomalin inaweza kupatikana kiurahisi kutoka kwa wafanyakazi walioko katika vyumba vya kuhifadhi maiti na kwamba ndio wanaojua jinsi ya kuitumia kwa ufasaha.

Mmoja wa wataalamu hao, alisema kuwa dawa hiyo imetengenezwa katika mfumo wa ungaunga wa aina ya poda na majimaji.

“Ni jambo la hatari kula samaki aliyenyunyiziwa dawa ya kukausha maiti, dawa hiyo ina kemikali ambayo ina madhara mwilini, madhara hayo yanaweza yasionekane mara moja mtu anapokula samaki walionyunyiziwa dawa hiyo, lakini baada ya muda, mtumiaji lazima aandamwe na magonjwa hasa ya kansa,” alisema mmoja wa madaktari bingwa wa Hospitali ya Muhimbili.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwenye maduka ya samaki jijini Dar es Salaam, umeonyesha kuwa, matumizi ya dawa hiyo ni jambo la kawaida kwa samaki wanaosafirishwa kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Uchunguzi umebaini kuwa, wafanyabishara wa samaki kutoka eneo hilo, wanatumia zaidi dawa hiyo kuhifadhi samaki kwa sababu inapatikana kwa gharama nafuu.

Inadaiwa kuwa wafanyabiashara hao wameamua kuitumia dawa hiyo kuhifadhia samaki kutokana na mwendo mrefu ambao inabidi wawasafirishe kuelekea kwenye masoko.

Ubovu wa barabara nao umetajwa kuwa ni moja ya sababu zilizowafanya wasafirishaji hao kubuni mbinu hizo, kwani hawawezi kuutumia usafiri wa ndege ambao ni wa haraka kwa kukwepa gharama.

Mfanyabiashara mmoja wa samaki aina ya sato, aliyejitambulisha kwa jina la Abdallah Gomama, kutoka mkoani Mwanza, alisema kuwa utumiaji wa dawa ya kuhifadhi maiti kuhifadhia samaki, unawasaidia wafanyabiashara kufikisha mizigo yao Dar es Salaam na maeneo mengine bila ya samaki hao kuharibika.

“Mimi hata ukinitaja jina siogopi, andika, ninaitwa Abdallah Gomama, tunatumia ndio na walaji wanajua, lakini samaki hawa tukishawafikisha huwa tunawaosha vizuri, dawa yote inatoka.

“Kama unataka kujua samaki ambaye bado ana dawa hiyo, anakuwa na harufu kali sana, lakini aliyeoshwa vizuri, ndio ana harufu fulani, lakini analika, kama watazuia kutumia dawa hiyo, Dar watakuwa hawali samaki, unafikiri kwa barabara hizi utafikisha samaki bila kuoza njiani?” alisema kwa kujiamini na kuhoji.

Alisema zaidi ya kusaidia kumhifadhi, samaki aliyepakwa dawa hiyo huvimba na kuongezeka uzito. Baada ya hapo hupakiwa kwenye maboksi na kisha kutumbukizwa ndani ya magunia ili kupunguza harufu kali.

Gomama alieleza kuwa wakishafika sehemu wanakopelekwa, samaki hao hupakuliwa na kuoshwa ili kuondoa dawa hiyo na harufu na hapo hurudia hali yake ya kawaida.

Kuhusu bei ya dawa hiyo, alisema wanainunua sh 15,000 hadi sh 30,000, lakini alikataa kutaja wauzaji na sehemu inakopatikana kwa wingi.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by paul)
    Rating
    hii ni habari ya kutisha na ya kusikitisha sana kusikia.ina maana tumeshindwa kutumia barafu kuhifadhi samaki mapaka tunafikia hatua ya kuhifadhi kwa kutumia dawa ya kuhifadhia maiti?halafu bado tunataka tupate soko la samaki ulaya unadhani wakisikia hili kuna mtu atataka kula samaki wetu?hebu tuamke wabongo.na je serikali inasema nini kuhusu suala hili maana sijaona hata mmoja serikalini kutoka kuliongelea.
     
  • Comment #2 (Posted by paul)
    Rating
    hii ni habari ya kutisha na ya kusikitisha sana kusikia.ina maana tumeshindwa kutumia barafu kuhifadhi samaki mapaka tunafikia hatua ya kuhifadhi kwa kutumia dawa ya kuhifadhia maiti?halafu bado tunataka tupate soko la samaki ulaya unadhani wakisikia hili kuna mtu atataka kula samaki wetu?hebu tuamke wabongo.na je serikali inasema nini kuhusu suala hili maana sijaona hata mmoja serikalini kutoka kuliongelea.
     
Submit Comment


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.