MUSWADA wa sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa wa mwaka 2007, hauna maana kama Ofisi ya Taasisi ya Kupambana na Rushwa (TAKURU) haitakuwa huru na mkurugenzi wake kuendelea kuteuliwa na rais; Bunge limeelezwa.
Hoja kuhusu kutoingiliwa kwa utendaji wa TAKURU, ndiyo iliyotawala mjadala wa muswada huo, huku serikali ikitakiwa kulipa Bunge mamlaka ya kupendekeza majina matatu ya wateule wa kushika nafasi hiyo kabla rais hajamteua mmoja miongoni mwao.
Akichangia mjadala huo, baada ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Philip Marmo kuusoma, Mbunge wa Karatu, Dk. Wilbroad Slaa (CHADEMA), alisema binafsi haungi mkono muswada huo endapo TAKURU itaendelea kubaki chini ya Ofisi ya Rais na uteuzi wa mkurugenzi wake kuendelea kufanywa na rais mwenyewe.
“Muswada huu, ukiuangalia kwa haraka haraka, utaona kama una jipya, lakini ukiuchambua, hakuna jipya hapa. Kama kweli tuna dhamira ya kupambana na rushwa, ofisi hiyo isiwe chini ya idara au ofisi yoyote ya serikali, na uteuzi wa mkurugenzi wake usifanywe na rais.
“Bunge ndio lifanye kazi hiyo na hata kufukuzwa kwake kufuate taratibu na misingi itakayowekwa tofauti na sasa rais akiona Mkurugenzi wa TAKURU amesimamia suala la rushwa la mtu anayemhusu, anaweza kumtimua kazi mara moja,” alisema Dk. Slaa.
Mbali ya kuitaka TAKURU iwe huru, Dk. Slaa pia aliitaka ofisi ya DPP isiwe na uwezo wa kuingilia masuala ya TAKURU kama ilivyo sasa, kwani ofisi hiyo imekuwa moja ya vikwazo vya TAKURU kufanya kazi zake kwa ufanisi.
Kuhusu suala la adhabu, Dk. Slaa alisema bado adhabu ya kulipa faini iliyopendekezwa katika muswada huo ni ndogo.
Kiongozi wa upinzani bungeni, Hamad Rashid (CUF), alisema TAKURU iwe ndani ya katiba ili kuiondoa katika Ofisi ya Rais.
Alisema Ofisi ya Rais kama taasisi, nayo inakabiliwa na malalamiko mengi ya rushwa na endapo TAKURU itakuwa chini ya ofisi hiyo, haitaweza kufanya kazi yake kwa uhuru.
“Utaiwekaje TAKURU chini ya taasisi ambayo nayo inatuhumiwa kwa rushwa?” alihoji Hamad Rashid na kuongeza kuwa, bila TAKURU kuwapo ndani ya katiba, haitaweza kufanya kazi zake kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Muleba Kusini, Wilson Masilingi (CCM), pia aliulalamikia muswada huo kwamba unampa madaraka DPP wa kuingilia na hata kufuta kesi za rushwa zinazoshughulikiwa na TAKURU.
Pia alitaka mshahara ya watumishi wa TAKURU uongezwe ili kuwaondoa wafanyakazi wake katika vishawishi vya rushwa.
Naye Mbunge wa Chunya, Victor Mwambalaswa (CCM), alisema chini ya sheria hiyo, suala la manunuzi ya vifaa vya serikali liwekwe bayana ili kuepuka dhana ya kuwapo kwa rushwa.
Akitolea mfano wa ununuzi wa rada, ndege ya rais, mbunge huyo alisema mawaziri waliuosimamia ndio wanaobebeshwa lawama, lakini wanaonewa kwani kazi ya ununuzi wa vifaa hivyo ingefanywa na kusimamiwa na wataalamu.
Pia alitaka wanaochukuliwa kufanya kazi TAKURU, wachaguliwe kwa utaratibu, tofauti na sasa, wa kutangaza nafasi hizo kwenye magazeti ili wachunguzwe tabia zao kabla ya kupelekwa kwenye kozi maalumu ya kupambana na rushwa.
Kwa upande wake, msemaji wa kambi ya upinzani, Khamis Shoka (CUF) alisema muswada huo umeshindwa hata kutoa tafsiri ya neno rushwa na kwamba taasisi hiyo siyo huru kwani bado imeachwa chini ya Ofisi ya Rais.
Baadhi ya mapendekezo yaliyomo katika muswada huo ni kuanzishwa kwa taasisi huru za kuzuia rushwa chini ya Ofisi ya Rais, kuipa taasisi mamlaka ya kufilisi mali zilizopatikana kwa njia ya rushwa na kuzirejesha serikalini, kuwalinda watoa taarifa za vitendo vya rushwa.
Marmo alisema muswada huo ulipokuwa unajadiliwa na kuchambuliwa katika nyakati tofauti, ilipendekezwa kuwa vitendo vya rushwa nyakati za uchaguzi za kisiasa kuongezwa katika makosa yaliyoorodheshwa katika muswada, lakini baadaye imeonekana si vema kufanya
hivyo kwa sasa, jambo ambalo wachangiaji wengi hasa wa upinzani wamepinga.
Spika wa Bunge, Samuel Sitta, alisema mjadala wa muswada huo utaendelea Jumatatu ijayo kutokana na idadi kubwa ya wabunge waliojitokeza kutaka kutoa maoni yao kabla ya kupitishwa na kuwa sheria.