Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Matumizi mabaya sasa yaitikisa dola
Matumizi mabaya sasa yaitikisa dola
By Habari Tanzania | Published  04/14/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Mwandishi Wetu


UPEPO wa matumizi mabaya ya fedha za umma katika serikali kuu na za mitaa, umeanza kutikisa mihimili mikuu miwili ya dola; Serikali na Bunge; Tanzania Daima imebaini.

Aidha, ahadi aliyoitoa Rais Jakaya Kikwete mwanzoni mwa mwaka jana, wakati alipotembelea Wizara ya Fedha chini ya utaratibu wake wa kuzitembelea wizara na idara nyeti za serikali, kuhusu namna ya kudhibiti matumizi holela ya fedha za umma, bado haijatoa mwanga wa kuanza kutekelezwa.

Hata hivyo, uamuzi wa Rais Kikwete kuitisha kikao cha Baraza la Mawaziri kuijadili Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) inayochambua matumizi yanayoishia Juni mwaka 2006 na ile ya Spika Samuel Sitta kutangaza rasmi kujadiliwa kwa ripoti hiyo hiyo, ni ushahidi kwamba, tatizo sugu la matumizi mabaya huenda likapatiwa ufumbuzi wa kudumu siku zijazo.

Hali hiyo inakuja baada ya mwaka jana, wahisani na asasi huru ya kijamii ya HakiElimu, kwa nyakati tofauti, kuhoji kuhusu kuendelea kuwekwa kapuni kwa ripoti ya CAG.

Aidha, matukio hayo yanakuja zaidi ya mwaka mmoja sasa, tangu Rais Kikwete mwenyewe alipotamka dhamira yake ya kuona CAG akipewa meno zaidi na akataka kuona wale wote wanaohusishwa na uchafu wa matumizi mabaya ya fedha za umma au yale yanayotiliwa shaka, kuchukuliwa hatua za kisheria kwa kupelekwa polisi na hatimaye mahakamani.

Pamoja na taarifa ya Ikulu ya jana kuonyesha kwamba, ripoti hiyo ya CAG ilijadiliwa katika kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika Dodoma chini ya uenyekiti wa Rais Kikwete mwenyewe, haikueleza hata kidogo maamuzi yaliyofikiwa katika mkutano huo.

Aidha, taarifa hiyo ya Ikulu haikusema iwapo ahadi ya Kikwete kumuongezea nguvu CAG au ile ya kuanza kuchukuliwa kwa hatua za kisheria kwa watuhumiwa wa matumizi mabaya au yale yenye shaka, ilikuwa ni moja ya ajenda zilizojadiliwa.

Hata hivyo tukio la Baraza la Mawaziri, kuijadili ripoti hiyo ya CAG ambayo imeendelea kuonyesha kuendelea kuwapo kwa matatizo makubwa katika matumizi, inakuwa ya kwanza ya aina yake tangu taifa hili lipate uhuru miaka zaidi ya 45 iliyopita.

“Baraza la Mwaziri, jana (juzi) Aprili 12 limepokea na kuijadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2005/2006,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo ya Ikulu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Ikulu, CAG aliwasilisha ripoti yake kwa rais Machi 26, mwaka huu, kama sheria inavyotaka.

Hatua hiyo imekuja sambamba na taarifa aliyoitoa Spika Sitta juzi, aliposema kuwa ripoti hiyo ya CAG itajadiliwa na Bunge kwa mara ya kwanza tangu Sokoine alipokuwa Waziri Mkuu mwanzoni mwa miaka ya 1980.

Ripoti ya CAG ambayo Baraza la Mawaziri limeijadili juzi na jana, inaonyesha kuwa bado fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zimeendelea kubakia kuwa ni kidogo kuliko zile za matumizi ya kawaida.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, matokeo ya ukaguzi wa fedha za serikali kwa mwaka wa fedha wa 2005/2006, yanaonyesha kwamba, nusu ya wizara, idara na wakala wa serikali, zina hati zinazotiliwa shaka na zisizoridhisha kimahesabu.

CAG, Ludovick Utouh, juzi aliwaeleza waandishi wa habari mjini Dodoma kuwa, tangu mwaka wa fedha wa 2003/2004, 2004/2005 na 2005/2006 fedha za miradi ya maendeleo hazijawahi kuzidi asilimia 25, wakati zinazotengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ni zaidi ya asilimia 75.

Kwa mujibu wa Utouh, katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2004/2005, matumizi ya serikali yaliongezeka kutoka sh 2,138,860,343,786 hadi sh 2,732,455,841,323 wakati mwaka huo wa 2005/2006, fedha za matumizi ya maendeleo zilipungua kutoka sh 850,353,139,955 mwaka 2004/2005 hadi sh 844,103,204,420 mwaka 2005/2006.

Moja ya mambo yaliyobainika katika ripoti hiyo ni Kwamba, Wizara ya Usalama wa Raia, hadi Juni mwaka jana ilikuwa inadaiwa sh bilioni 14.1 kwa huduma zilizotolewa na wadai mbalimbali na mpaka sasa madeni hayo hayajalipwa.

Ripoti hiyo inaonyesha pia kwamba, baadhi ya mambo yaliyochangia kuwa na hati chafu, kwa upande wa Serikali Kuu, ni pamoja na madeni yasiyolipwa katika mashirika ya umma yenye thamani ya sh bilioni 63.2.

“Pia kuna matumizi yasiyokuwa na faida kwa serikali (Nugatory expenditure) ya sh milioni 218.8. Hasara hii inarudiwa kila mwaka bila afisa masurufu kuchukua hatua za kinidhamu,” alisema Utouh akirejea ripoti yake aliyoiwasilisha bungeni juzi.

Kwa upande wa Serikali za Mitaa, ripoti inaonyesha kuwa, mambo yaliyochangia kuwa na hati chafu, ni pamoja na kutorejeshwa kwa masurufu yanayofikia sh milioni 800.7 kutoka katika mamlaka za serikali za mitaa 16.

Aidha, ripoti ya sasa inaonyesha kuwa, katika kipindi hicho cha mwaka 2005/06, mamlaka za serikali za mitaa 46 zilikuwa na matumizi yenye nyaraka ya sh bilioni mbili ambazo zililipwa bila ya hati za malipo.

Kuhusu hati zinazoridhisha, ripoti inaonyesha pia kwamba, wizara na idara zinazojitegemea, wakala na sekretarieti 40 kati ya 70 sawa na asilimia 57, zilikaguliwa na kupewa hati zinazoridhisha, wakati wakala na sekretarieti za mikoa 27 kati ya 70 sawa na asilimia 39, zilipewa hati zenye shaka.

Mwaka jana alipotembelea Wizara ya Fedha, Kikwete alimtaka Katibu Mkuu wa Hazina kuomba mamlaka ya rais ili awe na uwezo wa kuhoji matumizi ya fedha za halmashauri, na akaahidi kuwa, alikuwa tayari kutoa idhini hiyo ili kudhibiti matumizi mabovu ya fedha za umma.

“Sina ratiba ya kuonana na wakaguzi, lakini swali langu lilikuwa kwa nini wanapokuta upotevu wa fedha za umma hawafikishi polisi suala hilo na badala yake wanakazania kupeleka ripoti hiyo bungeni kwa ajili ya mijadala?” alihoji Rais Kikwete wakati huo.

Baadaye mwaka jana tena, taasisi ya HakiElimu nayo ilifanya mapitio ya ripoti ya miaka mitatu ya CAG na ikaeleza kusikitishwa kwake na baadhi ya wizara na taasisi za umma zilizokuwa zikitumia vibaya fedha za umma.

Uchambuzi uliofanywa na HakiElimu ukinukuu taarifa hiyo ya CAG, ulikuwa ukionyesha kuwa katika mwaka 2004/05, wizara na idara za serikali kuu na wakala (MDA), walishindwa kutoa maelezo ya sh bilioni 203, sawa na asilimia 10 ya matumizi yote ya kawaida kiasi ambacho ni zaidi ya mara tatu ya kile cha miaka miwili iliyotangulia.

Takwimu zinaonyesha kuwa, katika kipindi cha mwaka 2002/03 kiasi cha sh bilioni 65 kilitumika pasipo kuwa na maelezo ya kuridhisha huku mwaka uliofuata wa 2003/04, fedha kama hizo zikiongozeka hadi kufikia sh bilioni 82.

Katika kipindi hicho, wizara ambazo matumizi yake yalikuwa na dosari ni pamoja na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kiasi cha sh bilioni 36.4, Wizara ya Afya sh bilioni 32.4, Hazina/Deni la Taifa sh bilioni 29.4, Wizara ya Ujenzi sh bilioni 28.0, Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia sh bilioni 25.6, ambapo kulikuwa na jumla ya sh bilioni 151.8 kwa mwaka 2004/05.

Katikati ya mwaka jana, kundi la wafadhili linalojulikana kwa jina la ‘Wabia wa Maendeleo’ (Development Partners Group) liliitaka serikali kufanya marekebisho yanayotokana na kuwapo kwa mapungufu makubwa katika matumizi ya fedha za umma.

Kundi hilo la wahisani ambalo nchi na mashirika ya kimataifa wanayoyafanyia kazi yalichangia asilimia 46 katika bajeti ya serikali, walisema ili kuiondoa nchi kwenye umaskini, taarifa za CAG ni muhimu kutumika.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.