Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Lipumba amvaa Lowassa
Lipumba amvaa Lowassa
By Habari Tanzania | Published  06/22/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
Adai katengewa fedha nyingi kuliko JK
Na Kulwa Karedia
 

MWENYEKITI wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amelalamika kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu imetengewa kiasi kikubwa cha fedha katika bajeti ya mwaka huu.
 
Akizungumza na waandishi ofisini kwake, Buguruni, Dar es Salaam jana, Lipumba alisema Ofisi ya Waziri Mkuu, imetengewa fedha nyingi kuliko hata Ikulu ya Rais Jakaya Kikwete.
 
Alihoji vigezo vilivyotumika kutenga fedha hizo, sh bilioni 4 kwa mwaka 2006/7, wakati bajeti iliyopita ilikuwa sh bilioni 1.7.
 
Lipumba alisema: “Matumizi ya Waziri Mkuu (Vote 25) ndiyo yenye kasi kali ya kuongezeka kwa matumizi ya fedha kwani bejeti yake sasa imefikia bilioni 4/- ambapo awali ilikuwa bilioni 1.7/-. Ongezeko hili ambalo ni sawa na asilimia 130, limezidi hata Ikulu yenyewe. Matumizi haya yote yanatoka wapi?” alihoji Lipumba.
 
Lipumba alieleza pia kutoridhishwa na washauri wa Rais Kikwete: “Rais Kikwete anastahili kupata washauri wazuri… mimi ninaye mtu ambaye akimhitaji, hata sasa hivi nampelekea kwani ni mtaalamu mzuri, amefanya kazi kwa kipindi kirefu, wamesoma wote na Rais pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam . Sasa wale alionao akina Kingunge Ngombale-Mwiru hawawezi kumshauri vizuri, labda kumshauri kuwang'atua kina Malecela,” alisema Lipumba.
 
Lipumba aliishutumu awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete, akisema imeongeza kasi ya kutisha katika gharama za uendeshaji wa serikali. Alisema matumizi ya kawaida ya wizara yameongezeka kutoka sh trilioni 1.7 hadi sh trilioni 2.0, ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 17, hali ambayo alisema inatisha kwa nchi maskini kama Tanzania .
 
“Kasi hii ya ongezeko la bajeti kwa kila wizara imetoka wapi? Gharama za uendeshaji sasa zinatisha …au hii ndiyo ari, kasi na nguvu mpya aliyotangaza Rais Jakaya Kikwete kabla ya kuingia madarakani? Sisi CUF tunamtaka achukue hatua madhubuti za kupambana na matumizi haya, ni makubwa kwa nchi masikini kama Tanzania ,” alisema Lipumba.
 
Alisema kwa kuwa bajeti ya Tanzania bado inategemea misaada ya wafadhili wa nje kwa asilimia 46, Ofisi ya Waziri Mkuu haikutakiwa kuonyesha kasi ya matumizi makubwa kama hayo, kwa vile kufanya hivyo ni sawa na kuwaongezea mzigo wananchi.
 
Hata hivyo, Lipumba aliipongeza serikali kwa kuongeza matumizi ya bajeti ya maendeleo, akisema hatua hiyo itasaidia wananchi wa hali ya chini.
 
Lakini alisema bajeti hiyo imekuwa na kasoro nyingi, ikiwamo ya Waziri wa Fedha, Zakhia Meghji, kushindwa kutoa taarifa ya mapato ya Tanzania kutokana na mauzo ya dhahabu nje ya nchi, kwani imekuwa inaambulia kipato kidogo zaidi kikilinganishwa na wingi wa dhahabu inayouzwa.
 
Akizungumzia kilimo, alisema: “Zaidi ya robo tatu ya Watanzania wote wanategemea sekta ya kilimo na mifugo. Waziri wa Fedha anasema eti mwaka huu wametoa kipaumbele sana kwenye kilimo ambapo wametenga asilimia 3 tu, hali hii imesababisha wamepunguza kiasi cha fedha zilizokuwa zikitengwa katika bajeti zilizopita.”
 
Vile vile, Lipumba alimtaka Rais Kikwete ambane Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ili atangaze mali alizoondoka nazo madarakani, kwani kufanya hivyo kutasaidia viongozi wengi kufuata utaratibu huo.
 
“Mkapa bado anayo nafasi nzuri kabisa ya kueleza Watanzania nini alichokivuna tangu alipoingia madarakani kwani tunakumbuka siku ya kuingia madarakani alitangaza, sasa itakuwaje anaondoka kimya kiasi hiki? Nasema hii ni changamoto kwa Rais Kikwete na serikali yake kutangaza mali walizonazo,” alisema Lipumba.
 
Rais Kikwete amekaririwa mara kadhaa akisema kuwa angeongeza matumizi ya serikali hasa katika mishahara na kuboresha maisha ya wananchi kitu ambacho ni wazi kinaongeza ukubwa wa bajeti.
Kutoka: Tanzania Daima

How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
This article has been added to your 'Articles to Read' list.
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.