Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Uchumi  »  Ubinafsishaji wakuza uzalishaji wa mazao ya biashara
Ubinafsishaji wakuza uzalishaji wa mazao ya biashara
By Habari Tanzania | Published  04/13/2007 | Uchumi | Rating:

TANGU kuanza ubinafsishaji wa viwanda na mashirika mbali mbali hapa nchini, mafanikio makubwa yamepatikana kwa wakulima, wafanyakazi, wananchi na wenye viwanda mbalimbali pamoja na serikali inayopata faida kwa upande wa kodi mbalimbali zinazolipwa na wawekezaji.

Mtu anaweza kujiuliza wakulima nao wanafaidikaje? Jibu ni rahisi. Wakulima wanafaidika kwa kuuza mazao yao kwa wawekezaji mbalimbali wenye viwanda vya kusindika mazao, viwanda hapo awali vilivyokuwa vikimilikiwa na serikali kwa asilimia mia moja.

Serikali, kupitia Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC), iliamua kuvibinafsisha viwanda hivyo kwa lengo la kuongeza tija, uzalishaji na maslahi kwa wafanyakazi.

Lakini pia serikali inakusanya kodi mbalimbali kutoka kwa wawekezaji hao. Wawekezaji wengi wa maeneo ya vijijini wamekuwa wakichangia kuboresha huduma za jamii katika maeneo yanayowazunguka kwa kujenga vyumba vya madarasa, zahanati na barabara.

Katika eneo hili, wawekezaji hao ni makampuni binafsi ama vyama vya ushirika vilivyoamua kununua viwanda hivyo.

PSRC ndiyo inayoratibu zoezi la ubinafsishaji hapa nchini na mwamuzi wa mwisho anayeamua shirika fulani liuzwe kwa nani na kwa kiasi gani huwa ni serikali.

Baadhi ya wakulima wanaofaidika na ubinafsishaji ni wakulima wa chai katika Wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya, Kwa mujibu wa taarifa ya Chama Cha Wakulima Wadogo wa Chai Rungwe (RSTGA), kilo milioni 11 za chai mbichi ziliuzwa na wakulima hao mwaka 2002, na 2001 ziliuzwa kilo milioni 5.

Takwimu hizo zinaonyesha ni jinsi gani wakulima wanavyoongeza uzalishaji ili kuweza kufaidi matunda ya ubinafsishaji.

Taarifa hizo zinaongeza kwamba uzalishaji uliongezeka kutoka kilo 450 kwa hekta moja kwa karibu miaka kumi iliyopita hadi kufikia zaidi ya kilo 1,000 kwa hekta hivi sasa.

Kama tunavyofahamu, chai ni moja ya mazao ya biashara ambayo matumizi yake ni makubwa kwa jamii yetu inayopendelea kutumia chai kama kinywaji muhimu na pia kiburudisho. Baada ya nchi yetu kuamua kufuata sera za uchumi huria, makampuni mengi ya ndani na nje ya nchi yameamua kuwekeza na kusindika bidhaa hiyo kabla ya kuiuza kwa walaji.

Juma Ali, mkazi wa Dar es Salaam, anaipongeza serikali kwa kuruhusu makampuni binafsi kujihusisha na biashara ya chai, kwani hivi sasa walaji wanapata bidhaa hizo zikiwa katika ubora unaotakiwa. Majani ya chai yanauzwa kwa walaji yakiwa yamefungwa kwenye paketi za ujazo wa aina mbalimbali.

“Hivi sasa tunashuhudia bidhaa hizo zikifungwa katika paketi ndogo kabisa. Mlaji anaweza kupata paketi ndogo kabisa kwa sh 10 na kuendelea na tunaona jinsi makampuni ya chai yanavyoshindana kujitangaza…mara utasikia chai bora, wengine chai jaba, lakini mwisho wake ni manufaa kwa mlaji,” anasema.

Juma anasema kwamba pamoja na viwanda hivyo kuilipa serikali kodi mbalimbali, pia hutoa ajira kwa vijana wengi wa Kitanzania.

“Si unaona pale Tatepa (Jina la zamani la kiwanda) Nyerere Road, vijana wengi wanaomaliza vyuo mbalimbali hapa nchini wanavyopata ajira. Hicho ni kitu kizuri sana, kwani mbali na ajira, pia nchi yetu inapata fedha za kigeni kutokana na uuzaji wa chai nje ya nchi,” anasema.

Kwa mujibu wa RSTGA, kuongezeka kwa uzalishaji wa zao hilo kunaenda sambamba na kupanda kwa kipato cha mkulima mmoja mmoja, hali ambayo ni muafaka kwa sasa kwani serikali yetu inatekeleza mikakati mbalimbali ya kupambana na umaskini miongoni mwa wananchi na mikakati hiyo inalenga katika ‘kuwajaza’ mapesa wananchi.

Kilo mmoja ya chai mbichi imepanda hadi kufikia sh 94 mwaka 2005 kutoka sh 60 (2000) na kwamba chama hicho kilipata faida ya sh milioni 555 mwaka 2004 ikilinganishwa na sh milioni 150 mwaka 2003, na kwamba kutokana na faida hiyo ya sh milioni 555, RSTGA ilitenga sh milioni 118 kama gawiwo la wanachama wake kwa mwaka 2005.

Simon Mwakalinga ni mchumi Jijini Dar es Salaam. Anasema kwamba iwapo nchi yetu itafanikiwa kunyanyua kipato cha wakulima, basi pato la taifa litaongezeka hasa ikizingatiwa kwamba hadi sasa Watanzania wengi wanategemea kilimo kinacholiingizia taifa fedha nyingi za kigeni kwa kiwango kikubwa.

“Kwa sasa kuna sekta nyingine zinazochangia katika kuliingizia taifa fedha za kigeni wa mfano, hivi sasa kuna madini na pia samaki na mazao yake (Ziwa Victoria), lakini pamoja na sekta hizo kuibuka miaka ya hivi karibuni kilimo kwa kweli bado ni muhimili,” anasema mchumi huyo.

RSTGA pia inajivunia tafiti mbalimbali zilizosababisha kukua kwa uzalishaji wa chai wilayani Rungwe na kwamba kituo cha utafiti wa chai wilayani humo kimekuwa kichocheo cha kukua kwa uzalishaji wa zao hilo.

“Kwa kweli bila utafiti huwezi kujua njia za kuongeza kwanza ubora wa zao lenyewe na pia njia nyingine za kuongeza uzalishaji, hivyo nafikiri tafiti wanazofanya wakulima wa Rungwe nazo pia zimechangia kuongeza uzalishaji. Lakini pia hiyo ni sababu ya msingi ambayo imewasukuma wawekezaji kununua zaidi chai hiyo kwani nao wanataka mazao bora ambayo mwishoni yanatoa chai bora kwa walaji,”

Mbali na chai, kahawa nayo inachangia sana pato la taifa. Kahawa ina soko zuri la ndani na la kimataifa – Marekani. Kahawa ya Afrika inapendwa sana na ina soko kubwa, kuna mitaa mingine katika majiji ya Marekani ni maarufu sana kwa uuzaji wa kahawa na kinywaji chake kutoka Afrika hususan Tanzania.

“Hata nyimbo katika mitaa hiyo ni zile za Kiafrika, hivyo utaona ni jinsi gani kahawa inavyopendwa Marekani. Ni kitu cha kufurahisha sana kuona kahawa ya Afrika inaongoza kwa kupendwa nchini kwetu,” anasema Susan Campbell raia wa Marekani,”

Nchini Tanzania, kahawa inalimwa katika mikoa ya Kilimanjaro, Kagera na Ruvuma ambako kuna kiwanda vya kukoboa na kusindika vinavyomilikiwa na kampuni ya Mbinga. Hisa zake kwa kiasi kikubwa zinamilikiwa na vyama vya ushirika.

Uongozi wa kampuni hiyo unasema kwamba hivi sasa katika soko huria umechukua hatua mbalimbali za kuongeza uzalishaji wa kahawa mkoani Ruvuma, kwa lengo la kuwanufaisha wakulima. Baadhi ya hatua hizo ni kuwakopesha wakulima pembejeo.

Pia kampuni inazalisha kahawa ya unga inayojulikana kama Mbiga Café na pia imenunua mitambo ya kukoboa kahawa mbichi, imenunua hisa kutoka soko la hisa la Dar es Salaam pamoja vipande vya Umoja Fund kupitia Dhamana ya Uwekezaji Tanzania.

Uongozi unasema kuwa juhudi hizo zimezaa matunda, kwani kampuni imeweza kujiendesha kwa faida kwa miaka minane kati ya kumi hadi kufikia mwaka 2004.

Mwakalinga anasema kwamba hayo yote ni mafanikio ya ubinafsihaji, kwani hapo awali viwanda karibu vyote vya kusindika mazao vilikuwa chini ya serikali kupitia mamlaka na bodi za mazao mbalimbali.

Anasema serikali ilipoamua kuwaachia wananchi kupitia vyama vyao au wawekezaji binafsi, ushindani umeongezeka na hivyo kuongeza uzalishaji na ubora wa mazao mbalimbali ya biashara hapa nchini.

Anafafanua kuwa ubinafsishaji pia umeongeza uwazi na uadilifu miongoni mwa watendaji, tofauti na hapo awali wakati watu wachache waliopewa dhamana ya kuongoza vyombo hivyo vya wakulima walikuwa wakiviendesha viwanda na mashirika ya umma kama mali yao binafsi, na hivyo kuwakatisha tamaa wakulima walio wavuja jasho.

Hivyo mbali na viwanda mbalimbali kama vile vya bia na sigara kuongeza uzalishaji, lakini uzalishaji katika viwanda vingine mbalimbali vya kusindika mazao, umeongezeka na hivyo kusababisha uzalishaji na ubora wa mazao mbalimbali pia kupanda. Hayo yote ni matunda ya ubinafsishaji.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by bahati)
    Rating
    Samahani, hujaweza kuonyesha Faida kwa wakulima katika hii makala yako!!! Swali bado linakuwa ni kwa BEI ipi wakulima hawa wanauza mazao yao??? ikiwa ni pamoja na cost ya kuotesha hadi kuvuna haya mazao! je wakulima wadogo wananufaika vipi pia, elezea vizuri ukiwa na takwimu za mafanikio hayo bila hivyo utakuwa ukitupigia stori tu hapo! Ubinafsishaji ni moja nguzo za Umaskini. pole
     
Submit Comment


Article Options
This article has been added to your 'Articles to Read' list.
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.