HIVI karibuni Ghana iliadhimisha miaka 50 tangu ijipatie uhuru wake kutoka kwa wakoloni wa Kiingereza.
Hata hivyo, maelezo yoyote yale kuhusu harakati za kupigania uhuru wa nchi hiyo, hayawezi kuwa ya ukamilifu kama jina la Rais wa Kwanza na Baba wa Taifa hilo, Osagyefo Kwame Nkrumah, halitatajwa au kukumbukwa kutokana na mchango wake.
Aidha, mchango wake haukuishia Ghana peke yake bali aliuendeleza kwa nchi nyingine za Afrika kwa jumla na hivyo kuifanya nchi hiyo kuwa ni kifungua mimba cha kupatikana kwa uhuru wa nchi za Afrika, kusini mwa Jangwa la Sahara kutoka kwenye mikono ya wakoloni.
Akiwa ni mwanaharakati wa ukombozi wa Afrika, Nkrumah alitaka nchi za Afrika kuungana mara moja kwa kuunda taifa moja lenye umoja na kuzungumza kwa sauti moja.
Hata hivyo, hatua hiyo haikuweza kufanikiwa katika hatua zake za awali, lakini mwangwi wake bado unaakisiwa kwa nchi huru za Afrika hadi leo, lakini njia ya haraka kama alivyokuwa anataka Nkrumah hivi sasa imekuwa ni ya kuzunguka kwa kuunda jumuiya na mashirikisho.
Licha ya hali hiyo, moja ya mambo yanayomfanya Nkrumah aendelee kukumbukwa ni nadharia yake iliyolenga kundi la watu wa tabaka la chini.
Nkrumah alisema kuwa lipo kundi la jamii aliloliita déclassé na alisema kuwa likitumiwa vizuri linaweza kuleta mapinduzi au mageuzi makubwa ndani ya nchi.
Aidha, kundi hilo alisema kuwa linajumuisha watu wanaoonekana ndani ya jamii kuwa ni watu waliokosa mwelekeo, waliobanwa kimaisha na hata kitabia au kimaadili.
Watu hao ni pamoja na wanaoonekana kuwa ni wazururaji na wasio na ajira, kundi la vijana wanaofanya biashara ya ukahaba maarufu kama ‘changudoa’, vibaka na kwa jumla kundi la wanajamii ambalo kutokana na kutokuwa wanafanya kazi zenye heshima au zinazohesabika kuwa zinazoendana na maadili na hivyo kuonekana kuwa ni kundi lililokosa haiba.
Hali kadhalika, kundi hilo linajumuisha watu wasio na ajira wakiwamo vijana leo hii wanaounda kundi la wafanyabiashara ndogo ndogo kama wamachinga.
Kwa jumla, kundi hilo linaweza kuelezwa kuwa ni kundi la walalahoi waliokuwa wamekosa fursa katika dhana nzima ya kufaidi matunda ya nchi, ama enzi za utawala wa kikoloni au baada ya baadhi ya nchi kujipatia uhuru, na hivyo kuendelea kuwekwa pembezoni mwa keki ya taifa.
Katika dhana hiyo, Nkrumah alisema kuwa walalahoi hawa wakitumiwa vizuri wanaweza kuleta mapinduzi makubwa katika maendeleo ya nchi, kwa kuwa ndiyo nguzo na mhimili wa jamii na kwamba kundi hili linaundwa na wanajamii walio wengi kuliko kundi linaloundwa na wanajamii walio na maisha ahueni.
Mtazamo huo wa Nkrumah ulilenga kuangalia jamii kuanzia chini badala ya kuiangalia kuanzia juu, au kwa maana nyingine ni kwamba walio juu waangalie kwanza makundi ya jamii yaliyo chini ambako kiutawala ni mtazamo wa chini-juu badala ya mtazamo wa juu-chini.
Mtazamo wa mwanaharakati huyu ulikuwa ni wa kuona mbali kwa sababu jamii haiwezi kufanikiwa ikiwa kundi la jamii linaloonekana kukosa haiba, litaachwa pembezoni na kutojumuishwa ndani ya uchumi wa nchi na hata maamuzi katika ngazi yoyote ile, hali itakayolileta katika marekebisho na dhana nzima ya kukubalika katika jamii kuwa nao wana mchango muhimu.
Katika kuonyesha kukubalika kwa mtazamo huo baada ya kupata uhuru, nchini nyingi zilizamisha falsafa zake katika mtazamo kama huu wa Nkrumah kwa kuzijali jamii za walalahoi ikiwa ni jitihada za kuboresha maisha yao.
Hali hiyo ilitokana na sababu kuwa kundi hili la wanajamii ndilo lililotumiwa na viongozi wenyewe katika kujipatia umaarufu hususan katika kueneza siasa zake na mapambano dhidi ya ukoloni, na hivyo kuwaacha bila kuwapatia kile kilichokuwa kinahubiriwa kwao na viongozi wa vyama vya kupigania uhuru ilikuwa ni kufuru.
Hata hivyo, kwa baadhi ya nchi mtazamo huu wa Nkrumah haukupata nafasi hususan baada ya kupatikana kwa uhuru, kwa kuwa viongozi wengi waliuchukulia uhuru huo kama ni shughuli iliyofanywa na wao wenyewe na haikupata mchango kutoka kwa ‘wachovu’ wanaounda kundi hili la walalahoi.
Viongozi wengi walikumbatia dhana ya utawala ya juu-chini na hivyo kusababisha kundi la wachovu na wasaidizi wakuu katika harakati za kupigania uhuru, kuendelea kusota pembezoni na kusabababisha kuwapo makundi ya walalahai na walalahoi.
Katika enzi za mageuzi ya kisiasa, miongoni mwa nchi nyingi za Afrika kundi linaloundwa na wanajamii hawa wengi walipokea mageuzi hayo kama moja ya nguzo ya kuondokana na kusota kwao katika ulingo wa kuwekwa pembezoni.
Kutokana na hali hiyo, wanasiasa walio wengi hawakusita kuwatumia wanajamii wanaounda kundi hili katika kuhamasisha shughuli zao au kueneza propaganda zao.
Lakini katika hali inayoweza kuelezwa kuwa ni kuwakomboa, baadhi wamekuwa wanatumia fursa hiyo kuwalisha propaganda ambazo, kwa mtazamo wa kina, ni za kuendelea kuliweka kundi hilo pembezoni.
Kundi hili la wanajamii limekuwa linayumbishwa hususan inapofikia nyakati za kampeni za chaguzi mbalimbali kwa kulishwa mambo ambayo, kwa mtazamo mwepesi, yanaonekana ni kujaaliwa maisha bora, lakini linapokuja suala la mtazamo wa kina, inakuwa ni kuzamishwa na kutopea kwenye karaha na maisha kuwa ni ya kuendelea kuwekwa pembezoni, hali inayokuwa kinyume na mtazamo wa Nkrumah.
Suala la mageuzi ya kisiasa lilikuwa sanjari na kuingia kwa mfumo wa biashara huria ambako umilikishwaji wa mali umekuwa unalenga kuingia kwenye uendeshaji binafsi zaidi kuliko uendeshaji uliokuwa unafanywa na serikali.
Licha ya kwamba baadhi ya shughuli za biashara huria zimekuwa za manufaa kwa uchumi wa nchi kwa jumla, lakini hali ya aina hiyo miongoni mwa makundi ya walalahoi bado imekuwa mbaya na hususan linapotokeza suala la mageuzi hayo kuwa sanjari na mifumo huru ya biashara.
Kwa mfano Nkrumah katika hatua za mwanzo nchi hiyo ilipopata uhuru, alihakikisha kuwa zao la kokoa linapanda chati na kuwa na bei inayowezesha wakulima kukidhi mahitaji yao, lakini jambo la kushangaza hujuma zilifanyika na kusababisha bei yake kuporomoka katika soko la dunia, hali ambayo mara nyingi imekuwa ni moja ya sababu zilizochochea kufanyika kwa mapinduzi ya kijeshi yaliyomwondoa madarakani.
Hali kama hiyo si tofauti na iliyopo leo miongoni mwa nchi za Afrika. Biashara huria imebomoa soko la mazao mbalimbali ya biashara na hivyo kuwafanya walalahoi kuyumba katika uendeshaji wa maisha yao.
Jana waliokuwa wanaitwa ‘mabeberu’ na ambao Nkrumah alipingana nao kwa kila njia, leo wapo katika sura mpya ya ‘wabia’, ‘wahisani’, ‘wawekezaji’ na maneno mengine yanayotajwa kwa lugha laini na yenye misamiati inayopoozesha ukali wa neno ‘beberu’, lakini hali inakuwa ni ile ile aliyokuwa akipambana nayo.
Hali ya aina hiyo ni sawa na maneno ‘ukoloni mamboleo’ uliokuwa unapigwa vita, na shauku ya Nkrumah ilikuwa ni kuondokana na hali hiyo kwa kuunganisha nchi zote za Afrika. Leo hii hakuna anayeuona mwangwi wa ukoloni mamboleo kama upo zaidi ya kupewa majina ya kusifika ya ‘wabia na wawekezaji kutoka nje’.
Leo hii hakuna anayezungumzia mazao ya biashara bali ni suala la viwanda na biashara, hali ambayo jamii zilizo pembezoni zinakuwa hazina mwanya wa kuingia kwenye ushindani wa sekta hizo mbili, na hivyo kubakia kwa kiwango kikubwa njia panda.
Pamoja na hali hiyo inayounda kundi hili la déclassé, kwa namna moja au nyingine limekuwa ni mgongo wa kujinufaisha kwa tabaka lililo ahueni, na mara nyingine tabaka tawala na hapa ni lazima ikumbukwe kuwa wapiga kura walio wengi ndiyo wanaounda kundi hili.
Lakini ukweli unabakia kuwa kama tabaka hili likitumiwa vizuri linaweza kuleta mapinduzi katika nchi. Mapinduzi yanayozungumzwa leo hii ni ya kuondoa umaskini kwa kuwa idadi kubwa ya wanaounda kundi hili ndiyo waliotopea katika lindi la umasikini.
Mtazamo wa Nkrumah na mapinduzi aliyokuwa anayaona kabla na hata baada ya uhuru, kwa kutumia kundi hili kwa kiasi kikubwa tayari yameshamezwa na utandawazi.
mlayndeleio@yahoo.com
0756503761