MBUNGE wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela (CCM), juzi alilieleza Bunge kushangazwa kwake na hatua ya serikali kutumia muda mrefu kutafuta njia mbadala ya tatizo la nishati kwa kutumia mitambo ya kukodi inayoendeshwa na kampuni binafsi.
Kilango, mmoja wa wabunge wachache wanawake wanaotoka katika majimbo, huku akitaja kwa majina miradi ya umeme wa kukodisha, aliitaka serikali kuanza sasa kuangalia mbele kwa kugeukia mipango ya muda mrefu kuwekeza katika sekta ya nishati, ili hatimaye tatizo sugu la ukosefu wa umeme liweze kumalizika.
Akitoa mfano, Kilango aliitaka serikali kuwekeza katika mradi wa maji ya Mto Rufiji yanayopotea bure ili kuweza kuyatumia katika kuzalisha umeme badala ya kuendelea kutumia mitambo ya kukodi inayoligharimu taifa hili mamilioni ya fedha.
Kwa bahati mbaya, pamoja na ushauri mzuri na ambao kimsingi ni wa kukumbushana alioutoa mbunge huyo, Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi pasipo kutafakari kwa kina, alimtaka mbunge huyo kutosahau kuwa ni mwaka jana tu taifa hili lilikumbwa na tatizo la uhaba mkubwa wa umeme, ambalo ndilo lilisababisha serikali ilazimike kutumia umeme wa kukodi, tena akisema ilifanya hivyo ikiungwa mkono na wabunge.
Kwa maelezo yoyote yale yawayo, majibu hayo ya Karamagi yalikuwa ya kukurupuka na ambayo hayakupaswa kutolewa na waziri mwenye dhamana ya kuendeleza sekta ya nishati nchini.
Tunasema hivyo kwa sababu, si jambo rahisi hata kidogo kwa mbunge kama alivyo Kilango, ambaye ameweza kukumbuka haja ya lazima ya kuwekeza katika miradi ya umeme ya muda mrefu, akasahau kuhusu tatizo la ukame la mwaka jana.
Sisi tunaamini na hivyo ndivyo ilivyo kwamba, Kilango alitoa ushauri huo akitambua vyema kuwa nchi hii mara kadhaa, ikiwamo mwaka jana, imekuwa ikikumbwa na tatizo la ukosefu wa umeme, ambao jibu lake ni rahisi na linalofahamika sawasawa kuwa, ni uwekezaji wa muda mrefu.
Miezi michache tu imepita tangu Bernard Membe wakati huo akiwa naibu wa Karamagi, alipowaeleza waandishi wa habari kuwa, serikali imekuwa ikibeba mzigo mzito kuzilipa kampuni zinazoiuzia nishati ya umeme.
Membe ambaye wakati huo alikuwa akitokea Kyela kuangalia maendeleo ya uzalishaji wa umeme utakaotokana na makaa ya mawe kule Kiwira, aliwaeleza waandishi wa habari kwamba, serikali ilikuwa ikilazimika kutumia sh bilioni 29 kuzilipa kampuni zinazozalisha umeme unaotokana na mashine hizo za kukodi, kiwango ambacho alisema ni kikubwa mno.
Membe hakuishia hapo, bali alikwenda mbali zaidi na akanukuliwa akisema; “Lengo letu ni kuhakikisha kuwa tunaondokana na umeme wa kukodi ambao unaiondolea serikali mabilioni ya shilingi kila mwezi. Kiwira ikiwaka (ikizalisha umeme), itatuondolea gharama hizi.”
Ukiyasoma kwa makini maelezo ya Membe na ukaiangalia Ilani ya Uchaguzi wa mwaka 2005 ya CCM mara moja utabaini namna Karamagi alivyotoa majibu ya kibabaishaji bungeni, pengine kwa dhamira ya kutaka kukwepa kujibu swali muhimu la mbunge.
Aidha, ukiwaangalia wote wawili, Karamagi na Kilango, ni rahisi kabisa kubaini kuwa, waziri ndiye aliyeonekana kuwa msahaulifu kutokana na kusahau wajibu wake kama kiongozi, kusahau Ilani yake ya uchaguzi na kusahau mwelekeo wa kisera wa wizara anayoiongoza. Hii ni fedheha kwa serikali.