Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Magufuli aja na mwarobaini wa ardhi
Magufuli aja na mwarobaini wa ardhi
By Habari Tanzania | Published  04/12/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Rahel Chizoza


MISWADA ya sheria ya ardhi iliyowasilishwa bungeni jana, itasaidia kutatua migogoro ya ardhi iliyopo katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwa ni pamoja na kuwawezesha wanawake kumiliki ardhi.

Miswada hiyo iliyosomwa kwa mara ya pili na kuwasilishwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, John Magufuli, ni muswada wa sheria ya kuweka mwongozo wa kuandaa na kutekeleza masuala mbalimbali yanayohusu mipango miji wa mwaka 2006.

Muswada mwingine ni wa sheria ya kuanzisha Bodi ya Usajili ya Mipango Miji wa mwaka 2006 na muswada wa sheria ya kuweka mwongozo wa kuandaa, kuendesha na kutekeleza sheria ya mipango ya ardhi.

Akiwasilisha miswada hiyo bungeni, Magufuli alisema migogoro ya ardhi iliyopo hivi sasa, inachangiwa na kuwepo kwa sheria ambazo hazionyeshi njia ya kutatua migogoro hiyo.

Alisema kupitishwa kwa miswada hii mipya, kutapunguza migogoro na kurudisha thamani ya ardhi kama inavyoeleweka kuwa ardhi ni mali kwa mujibu wa sheria.

Alisema mapendekezo yaliyopo katika miswada hiyo mitatu, yatasaidia kutengeneza mipango miji na kutekeleza mchakato wa maendeleo ya ardhi na makazi kwa ujumla wake.

Magufuli alisema, kuanza kutumika kwa sheria hiyo mpya, kutatoa fursa kwa wanawake kuwa na haki ya kumilikishwa ardhi kama ilivyo kwa wanaume tofauti na fursa zilizokuwa zikitolewa na sheria za zamani.

Kamati ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ilitoa mapendekezo yake kuhusu kuboreshwa kwa miswada hiyo ya sheria ambayo yalisomwa na Castor Ligalama (Kilombero-CCM).

Kamati hiyo ilipendekeza mamlaka za wilaya zipatiwe uwezo wa kifedha na vifaa kwa ajili ya kusimamia majukumu ya ardhi yaliyopo chini ya wilaya husika.

Pia kamati hiyo imependekeza kuundwa kwa sera za upimaji wa ramani ili kuwasaidia wananchi, kwani kukosekana kwa sera hizo kumekuwa kukisababisha kazi ya upimaji wa ramani kuendeshwa bila mpangilio maalumu.

Walisema ni vema miswada ya sheria inapoandaliwa, ikaambatana na sera zinazohusu sheria husika kwa kurahisisha utendaji.

Akitoa maoni ya kambi ya upinzani, Salim Hemed (Chambani-CUF), alipendekeza mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji ipangwe na wanavijiji wenyewe, kwani wao ndiyo wanaofahamu vipaumbele vyao.

Aidha, amesema kuwa, fidia zinazotolewa kwa wananchi baada ya ardhi yao kuchukuliwa, hazilingani na thamani ya ardhi husika kwani wananchi wanaomiliki ardhi hiyo hawapatiwi nafasi ya kushiriki katika mchanganuo wa ugawaji na tathmini ya ardhi wanayoimiliki.

Taarifa hiyo imebainisha kuwa, asilimia kubwa ya wananchi wanaohamishwa katika makazi yao na kulipwa fidia, wamekuwa wakipatwa na umasikini uliokithiri kutokana na kulipwa fidia ndogo isiyolingana na thamani ya ardhi yao, ambapo mwananchi analipwa fidia ya sh 6,000 kwa mnazi mmoja ambao anautegemea katika maisha yake.

Katika muswada huo, kipo kipengele kinachohusu sifa za Mkurugenzi Mkuu wa Tume, lakini kambi ya upinzani ilipendekeza kuwa pamoja na sifa zilizoainishwa katika muswada, ni muhimu kikaongezwa kipengele kingine kinachosema kuwa, mtendaji mkuu awe na ufahamu wa masuala yanayohusu serikali za mitaa.

Kambi hiyo ya upinzani ilisema kuwa, haina tatizo na miswada hiyo ambayo itaboresha sekta ya ardhi, bali wangependa mapendekezo waliyotoa yazingatiwe ili kuboresha zaidi sheria hizo mpya kwa manufaa ya wananchi walio wengi.

Akichangia katika kujadili miswada hiyo, Peter Selukamba (Kigoma Mjini-CCM), alisema serikali iangalie uwezekano wa kutoa fidia kulingana na thamani ya ardhi ili kuwaondolea wananchi unyonywaji wanaoupata kutokana na utoaji wa fidia.

Pia alisema kutokana na waziri kupatiwa mamlaka makubwa ya kusimamia ardhi, upo uwezekano wa kupuuzwa kwa maamuzi yanayotolewa na halmashauri kuhusu matumizi ya ardhi.

Alisema ni vema hivi sasa serikali ikaanza kupanga makazi ya wananchi kwa viwanja vipya inavyopima na si kusubiri wananchi wakishajenga ndiyo waanze kuambiwa habari za kupanga makazi yao.

“Tanzania inaweza kupanga makazi yake na kuifanya miji ivutie kama viongozi wa ngazi zote watasimamia majukumu yao. Ni aibu kuwa na miji ambayo haijapangiliwa vizuri wakati wataalamu wa mipango miji wakiwepo na wanaendelea kufanya kazi,” alisema.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.