Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Safari ya Chitalilo mahakamani yaanza
Safari ya Chitalilo mahakamani yaanza
By Habari Tanzania | Published  04/12/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Happiness Katabazi


HATIMAYE wapiga kura wa Jimbo la Buchosa mkoani Mwanza, jana waliwasilisha rasmi ombi lao kutaka Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, iwarushu kumshtaki mbunge wao, Samwel Mchele Chitalilo, kwa utaratibu wa mwendesha mashtaka binafsi (Private Prosecution), kwa tuhuma zinazomkabili za kughushi vyeti na kudanganya kuhusu elimu yake.

Wapiga kura hao, wakiongozwa na mlalamikaji, Henriko Msheleja, walifungua kesi hiyo jana saa tano asubuhi katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, na tayari imeishapewa namba 25 ya mwaka 2007. Wapiga kura hao wanatetewa na Kituo cha Kutetea Haki za Binadamu (LHRC), chini ya wakili wake, Fred Mkatambo.

Mlalamikaji wa pili katika shauri hilo ni Alfred Ngotezi, ambaye ndiye aliyefungua jalada namba SEN/104/2006 la uchunguzi kuhusu elimu ya Chitalilo, mjini Sengerema mkoani Mwanza mapema mwaka jana.

Kwa mujibu wa hati ya madai iliyowasilishwa mahakamani jana, walalamikaji wanaomba waruhusiwe kumshtaki Chitalilo kwa utaratibu wa uendeshaji mashtaka binafsi chini ya kifungu cha 99 cha mwenendo wa makosa ya jinai.

Mwezi Machi mwaka huu, Msheleja alifika katika ofisi za gazeti hili, akiwa na mpigakura mwenzake, Ramadhani Amani, wakiwa na majina na saini za wapigakura wengine 184 wa Jimbo la Buchosa, wakiomba msaada wa kisheria ili kumshtaki Chitalilo kwa kudanganya kuhusu elimu yake.

Hatua hiyo ilifuatia Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, kuthibitisha Februari mwaka huu kuwa, upelelezi wa Polisi umebaini kuwa, mbunge huyo alikuwa amedanganya kuhusu elimu yake katika chaguzi za 2000 na 2005, lakini akasema polisi haiwezi kumfungulia mashitaka kwa sababu hakuwa amevunja sheria ya uchaguzi.

Kwa kawaida, masuala yote ya jinai hushughulikiwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), isipokuwa pale inapobidi kufanya kinyume ambapo ruhusa maalumu inaweza kutolewa na Mahakama Kuu kwa kutumia kifungu cha 99 cha mwenendo wa makosa ya jinai.

Hati ya kiapo iliyowasilishwa na kupokelewa mahakamani hapo jana, ambayo gazeti hili limepata nakala yake, imeorodhesha hoja 13 na viambatanisho sita, katika maombi hayo ya kutaka Chitalilo ashtakiwe kwa utaratibu huo.

Hati hiyo inadai kuwa, Chitalilo alighushi vyeti na kujipatia sifa zisizokuwa zake na kuwa alifanya makosa hayo katika chaguzi za 2000 na 2005.

Inaongeza kuwa alidanganya wapigakura kwa kutoa vipeperushi, akionyesha kuwa alimaliza kidato cha nne kwenye Shule ya Sekondari Bupandagila mkoani Shinyanga kati ya 1985 hadi 1990, na kuwa alisoma Sekondari ya Katikamu nchini Uganda kati ya 1990 na 1991.

Walalamikaji wanadai pia katika hati hiyo kuwa, Baraza la Mitihani la Uganda na Shule ya Katikamu, wametoa nyaraka kukanusha kuwa Chitalilo aliwahi kusoma huko. Wanadai pia kuwa wamewasilisha malalamiko yao katika ngazi mbalimbali za utawala, bila mafanikio yoyote.

Hati hiyo pia inadai kuwa, walalamikaji walimwandikia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Spika wa Bunge kuhusu tatizo hilo, lakini wanadai hakuna kilichofanyika.

Wanasema kuwa wanatafuta haki katika suala hilo, ili liwe fundisho kwa watu wengine wenye mwenendo kama huo.

Hati hiyo inaeleza pia kuwa, DCI alithibitisha bayana kuwa baada ya uchunguzi wao, polisi walibaini kuwa mbunge huyo alikuwa ametenda kosa la jinai kwa kughushi vyeti. Wameongeza kuwa, pindi polisi walipoanza kuchunguza elimu yake, alibadilisha wasifa aliokuwa ameweka kwenye tovuti ya Bunge, mabadiliko ambayo hata hivyo wanadai yanaonyesha kuwa alimaliza kidato cha pili kwenye Sekondari ya Bupandagila mwaka 1991, ilhali akiingia kidato cha tano mwaka huo huo wa 1991.



How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.