JESHI la Polisi nchini, limesema siku za wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya kuwa huru, sasa zinahesabika.
Upelelezi kuhusu vigogo hao wa dawa za kulevya, ambao orodha yao ilifikishwa katika jeshi hilo mapema mwaka jana, unakaribia kukamilika.
Akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalumu ofisini kwake jana, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Manumba, alisema kuwa hivi karibuni, jeshi hilo litaanza kuwakamata wauza unga hao mmoja baada ya mwingine.
DCI Manumba alilihakikishia gazeti hili kuwa, Jeshi la Polisi limeyafanyia kazi majina ya vigogo hao, na sasa upelelezi unaowahusu unakaribia kukamilika.
Manumba ametoa kauli hiyo baada ya Askofu Mokiwa wa Kanisa la Anglikana Dar es Salaam, kuitaka serikali kuwataja wale wote wanaojihusisha na dawa za kulevya, hasa ikizingatiwa kuwa, miongoni mwa wale wanaoshukiwa ni viongozi wa kidini.
“Kumekuwa na mafanikio mazuri katika operesheni hii, na tumefanikiwa kupata majina mengi, ninachokuhakikisha ni kwamba, baada ya kukamilisha uchunguzi na kuwabaini wanaohusika, watashughulikiwa ipasavyo na majina yao yatakuwa wazi,” alisema DCI.
Alisema wapo wengi ambao bado wanaendelea kuchunguzwa na kuwa maamuzi yao yatatolewa muda si mrefu.
Alisema uchunguzi unaoendeshwa na Jeshi la Polisi dhidi ya watu ambao majina yao yapo kwenye orodha hiyo, ni pamoja na kuangalia mali zao na jinsi walivyozipata.
“Hawa watu wanaofanya biashara hii wamekuwa matajiri wakubwa sana, wapo wenye magari kama daladala, wanamiliki majengo, yakiwemo maghorofa na kujenga nyumba za kifahari, sasa haya yote tunayachunguza,” alisema Manumba.
Mkurugenzi huyo aliongeza, juhudi zilizofikiwa zinatia matumaini ya kupungua kwa tatizo hilo, ingawa litachukua muda mrefu.
Alisema kwa sasa jeshi hilo limefanikiwa kudhibiti mianya mingi ya wafanyabiashara wadogo wadogo wa dawa za kulevya.
“Tumefikia sehemu ambayo ni nzuri na sasa tumekazia zaidi kuhakikisha ile mitandao ya wauuzaji wa chini inavunjwa, na kwa hili naona kuna mafanikio makubwa baada ya kuunda “Task Force” nchi nzima na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa,” alisema Manumba.
Alisema jeshi hilo limefanikiwa kupunguza makali ya uingizaji wa dawa hizo katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Mbeya, ambayo siku za nyuma ilikuwa tishio kwa biashara hiyo.
Alisema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mkubwa toka kwa wananchi, ambao wamekuwa wakitoa taarifa nyingi na nzuri kwa jeshi hilo.
“Moyo huu unaoonyeshwa na wananchi katika utoaji wa taarifa za wafanyabiashara hawa, unatia matumaini kwani wamesaidia kunasa watu wengi wanaojihusisha na biashara hii, kwa kweli nawaomba waendelee na moyo huo,” alisema Manumba.
Tangu alipoingia madarakani, Rais Jakaya Kikwete alitangaza rasmi vita dhidi ya dawa za kulevya, na kutaka jeshi hilo na taasisi zingine kuhakikisha zinawasaka na kuwakamata wale wote wanaohusika katika biashara hiyo haramu.