MGOGORO wa ardhi kati ya viongozi wa Kata ya Kibasuka na wananchi wa Kijiji cha Nyakunguru wilayani hapa mkoani Mara, umefikia mahali pabaya baada ya wananchi kudai kuwa, wametishiwa kuuawa kama wataendelea kuhoji uuzwaji wa ardhi ya kijiji chao.
Mbali na kutishiwa kuuawa, wananchi hao wanadai pia kuwa wamekuwa wakipokea vitisho vya kubambikiwa kesi za mauaji iwapo wataendelea kulilalamikia suala hilo kupitia kwa viongozi wa ngazi za juu na vyombo vya habari.
Wananchi hao walitoa kilio chao jana katika mkutano wa hadhara ulioitishwa na Mbunge wa Tarime, Zakayo Wangwe, kijijini hapo.
Wangwe alifika kijijini hapo kufuatilia chanzo cha mgogoro huo uliosababisha wanachi kutokuwa na imani na viongozi wa kijiji na kata.
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kijijini hapo, Sairo Wambura, aliwaongoza wananchi hao na kudai kuwa, viongozi waliojichukulia ardhi bila ridhaa ya serikali ya kijiji hicho, wamekuwa wakiwatisha wananchi kuwa watawaripoti katika Jeshi la Polisi kuwa, walihusika katika mauaji ya watu kadhaa ili wapate kesi za mauaji na hivyo kukosa nafasi ya kufuatilia suala hilo.
Walimwambia mbunge wao kuwa, tayari watu watatu, akiwemo Mwenyekiti wa CCM wa Kijiji cha Nyakunguru, wameunganishwa katika kesi za mauaji kwa madai kuwa ni moja ya mbinu za kuwanyamazisha.
Inadaiwa kuwa, watu hao walikamatwa na kuunganishwa katika kesi hiyo baada ya taarifa zilizotolewa polisi na baadhi ya viongozi wa kijiji na kata, wakiongozwa na ofisa mtendaji wa Kata ya Kibasuka, Rhobi Matugura.
Wakazi hao waliwakataa viongozi hao mbele ya mbunge wao na kuamua kumuondoa madarakani Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji, Abel Maginga na kamati yake.
Aidha, waliiomba Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, itangaze uchaguzi mdogo wa kuziba pengo hilo, sambamba na kuitaka serikali iwahamishe mara moja watendaji wake wanaotuhumiwa kujihusisha na sakata hilo.
Waliwataja wanaodaiwa kubambikiwa kesi za mauaji kuwa ni Mwenyekiti wa CCM wa kijiji hicho, Julius Magebo Magige, Chacha Mwita Gotono na Maro Seba.
Inadaiwa kuwa baadhi ya viongozi wa kijiji na kata ya Kibasuka, wamejichukulia ardhi kinyemela, na eneo lipatalo ekari 10 tayari limeshauzwa kwa mgodi wa dhahabu wa North Mara.
Viongozi wanaodaiwa kuhusika katika njama hizo, ni pamoja na diwani wa kata hiyo, John Mayo, Ofisa Mtendaji Rhobi Matugura, Mratibu Elimu Kata, Adriano Johanes, Mwenyekiti wa Kijiji, Abel Maginga, Mwenyekiti wa Kitongoji, Timas Chacha sambamba na wajumbe wa kamati ya fedha na mipango ya kijiji hicho.
Viongozi hao wanadaiwa kuchukua eneo lenye ukubwa wa ekari 24, na kuuza matofali 30,000 yaliyokuwa kwa ajili ya ujenzi wa shule. Tayari ekari 10 zimeshauzwa kwa Kampuni ya North Mara likiwemo jengo la ofisi ya CCM.
Kampuni hiyo imekiri kununua eneo hilo kwa sh milioni 6.2, fedha ambazo pia hazijulikani zilipo hadi sasa.
Baada ya kusikia malalamiko hayo, Wangwe alisema atayafikisha kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, John Magufuli, kwa hatua zaidi.
Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa Kijiji cha Nyakunguru na kata hiyo ya Kibasuka, walikanusha kuhusika na uporaji wa ardhi na kubambika watu kesi za mauaji, huku wakikiri kuwa suala la uuzaji wa ardhi lilifanyika kwa baraka zote za wananchi.
Diwani wa kata hiyo, Mayo na Mratibu Elimu Kata, Johanes, walisema wanao ushahidi wa nyaraka, ambazo zinaonyesha kuwa wananchi walikubali kuuza ardhi hiyo kwa kutia saini zao katika nyaraka hizo, jambo ambalo linapingwa vikali na wananchi wanaodai kuwa nyaraka hizo ni za kugushi.