Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Spika - Malima kanifedhehesha
Spika - Malima kanifedhehesha
By Habari Tanzania | Published  04/11/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:
na Martin Malera, Dodoma


SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Samuel Sitta, amesema adhabu inayomfaa Mbunge wa Mkuranga, Adam Malima (CCM) kwa kosa la kulidhalilisha Bunge na Spika (Sitta), ni kumpuuza na kuwataka wabunge washirikiane kumpa ushauri nasaha.

Akionekana mwenye hasira, Sitta alisema kitendo hicho si tu kwamba kimelidhalilisha Bunge, bali pia kimemdhalilisha yeye, na kwamba hajawahi kudhalilishwa kiasi hicho katika maisha yake ya utumishi serikalini.

Sitta alitoa tamko hilo jana wakati akiahirisha kipindi cha maswali na majibu mjini Dodoma.

Alilazimika kutoa kauli hiyo kutokana na barua iliyoandikwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Halima Mdee (CHADEMA), aliyetaka Bunge kujadili tena hatua ya Malima kulidhalilisha Bunge, hasa ya kukataa kikao cha usuluhishi kilichoandaliwa na Spika Sitta katika kesi yake na Reginald Mengi.

“Nimepata barua ya Mheshimiwa Halima Mdee, anayetaka mwongozo wa nini kifanyike kuhusu mbunge mwenzetu, Adam Malima na jinsi alivyoathiri sifa ya Bunge na sifa ya Spika. Naomba nisisome barua yote.

“Suala la Malima linaweza kulifanya Bunge lionekane Bunge la kuchemka. Yeye Malima ameshindwa kuthibitisha aliyoyasema na kuyaona, na mimi namwita mwongo, lakini anaona sio mwongo. Binafsi nimesononeshwa sana katika maisha yangu kwani ni mara yangu ya kwanza kujikuta kwenye wakati mgumu wa hali hiyo…,” alisema Sitta.

Sitta alitoa ufafanuzi wa suala hilo kuwa, alipanga kukutana na Malima Machi 3, mwaka huu katika ofisi yake mjini Dar es Salaam ili kuangalia jinsi ya kumshirikisha mtu wa tatu (Mengi), ambaye si mbunge katika kikao cha usuluhishi.

“Malima mwenyewe alipowasiliana na Katibu wa Bunge, alichagua nikutane naye Machi 7 saa 5:00 asubuhi ofisini kwangu. Ilipofika saa 5.40, Secretary (katibu muhtasi) wangu alimpigia simu, akamjibu kwamba angekuja mchana. Siku hiyo niliondoka ofisini saa 12:00, Malima hakutokea wala kutoa taarifa za kutofika kwake…

“Sikukata tamaa, kwa siku mbili mfululizo niliendelea kumtafuta, lakini simu tuliyokuwa tunampata na tunayoijua, hakawa hapatikani tena, kumbe tayari alishaandika barua kwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Machi 3. Hii ina maana wakati tunajaribu kuwasiliana naye Machi 7, Malima alishafanya uamuzi wa kutoonana na Spika,” alisema.

Huku idadi kubwa ya wabunge ikionekana kutulia, Sitta aliwataka kutambua kuwa, ingawa Malima anasema Sitta ni mbunge kama alivyo yeye (Malima), ukweli unabaki kuwa anapokuwa hapo (bungeni), yeye ni kiongozi wao na wana wajibu wa kumheshimu.

“Suala la Malima na Mengi limetumia zaidi ya sh milioni 100 kuendesha vikao vya Kamati ya Maadili na Haki za Bunge, na wajumbe wote walikuwa wakilipwa posho mpaka mashahidi.

“Malima mwenyewe ndiye aliyeleta mashahidi wengi mpaka wengine wasiohusika kabisa na Bunge, sasa wabunge hatuwezi kuendelea kujadili suala hili na kuendelea kupoteza fedha za wananchi ambazo zingeweza kutumika katika shughuli zingine za kimaendeleo,” alisema Sitta huku akishangiliwa na idadi kubwa ya wabunge.

Alisema katika suala hili, jamii inaelewa Malima yukoje, hali kadhalika inaelewa Spika Sitta yukoje, hivyo haina sababu ya kuendelea kujadili suala hili, kwani hata wananchi wataanza kulishangaa Bunge hilo.

Sitta alieleza pia kwamba, kwa kuwa suala hilo limekuzwa na kuanza kuchukua mwelekeo tofauti, ameufunga rasmi mjadala kuhusu suala hilo.

Akifafanua, alivirushia lawama vyombo vya habari kuwa, vimekuwa vikikuza suala hilo na kwamba ndio wanaonufaika zaidi katika kesi ya Malima, Mengi na Sitta.

“Vyombo vya habari ndio vimekuza suala hili. Wanakupigia simu, ukisema umechoka kuzungumzia hoja hiyo, asubuhi utaiona kwenye ukurasa wa kwanza. Sasa nasema nimefunga mjadala wa Malima na kuanzia leo, sitazungumza na mwandishi yeyote juu ya suala la Malima, Mengi na Sitta.

“Bado tunampenda mbunge wetu, bado kijana, wabunge tusaidieni kumpa ushauri nasaha. Sitatoa adhabu kwake kwani wakati mwingine kumpuuzia mtu ni adhabu kubwa kuliko kutoa adhabu yenyewe,” alisema Sitta na kufunga hoja hiyo.

Wabunge wengi waliozungumza na Tanzania Daima nje ya Bunge, walimuunga mkono Sitta kwa hatua hiyo, ingawa baadhi yao walitaka Malima apewe adhabu, kwani amelivunjia heshima Bunge.

“Mimi mwenyewe sijaona amefunga vipi mjadala. Kwa sababu yeye kasema hataki kuzungumza na waandishi, ndio kufunga mjadala. Sasa Malima akizungumza na Waandishi itakuwaje? Hakuna ubishi kwamba Malima alistahili adhabu. Mimi ni CCM mwenzake, lakini nasema katika hili hapana, busara ya Spika imevuka mipaka,” alisema mbunge mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Kwa upande wake, Malima hakutaka kuzungumza na waandishi, hata walipomfuata kutaka kujua maoni yake juu ya kauli ya Spika Sitta.

Wakati akichangia hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Utamaduni na Michezo mwaka jana, Malima alitoa kauli bungeni kuwa, vyombo vya habari vya IPP vinavyomilikiwa na Reginald Mengi, vimekuwa vikitoa nafasi kubwa ya habari zinazomhusu mmiliki wake (Mengi) na kwamba vinatoa muda mfupi kwa matukio ya kitaifa hata yale yanayofanywa na viongozi wakuu.

Kutokana na kauli hiyo, Mengi alipeleka malalamiko yake bungeni na Sitta alilipeleka lalamiko hilo kwa Kamati ya Haki na Maadili ya Bunge.

Hata hivyo, kamati ilibaini kuwa, kauli ya Malima haikuwa sahihi na Spika katika uamuzi wake, alisema Malima ni muongo, ameliongopea Bunge na Mengi aliambiwa hakumtendea haki Malima kwa kutangaza kwenye vyombo vya habari kwamba Malima ni mwongo.

Hivyo alimtaka Malima na Mengi kufika ofisini kwake si kwa ajili ya kuombana radhi, bali kwa usuluhishi, jambo ambalo Malima alilipinga.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by AFRODIME)
    Rating
    Mtu anatoka mkuranga kila siku kwa mjumbe wanashitakiana mpka inakuwa jadi yao. BRAVO Speaker mpuuze huyo Kijana mwenye Kiburi ya White House.
    "Sisi ndo tunaongoza nchi" ndio jeuri yao hao Pwani line.
    Thanks
     
Submit Comment


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.