Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Lowassa ashtushwa kasi ya RVF
Lowassa ashtushwa kasi ya RVF
By Habari Tanzania | Published  04/10/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Rahel Chizoza, Dodoma


WAZIRI Mkuu, Edward Lowasa, ameshtushwa na hali za wagonjwa wa homa ya bonde la ufa (RVF), waliolazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, baada ya kutembelea hospitali hiyo jana.

Katika ziara hiyo, Lowassa aliwashuhudia wagonjwa waliolazwa katika wodi namba 4 na 5 wakiwa na hali mbaya sanjari na kupatiwa taarifa iliyoeleza ongezeko la idadi ya wagonjwa na vifo, tangu kumalizika kwa ziara ya manaibu waziri watatu aliowaagiza kuja kuangalia hali ya ugonjwa.

Baada ya kuona hali halisi ya wagonjwa wa RVF katika wodi hizo, Lowassa aliridhia kutolewa kwa fedha zilizoombwa na Serikali ya Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya kuwalipa wauguzi wa wagonjwa wa RVF na utoaji wa elimu kwa wananchi.

Lowasa aliagiza serikali mkoani Dodoma kujikita katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu ugonjwa huo, kutokana na kutokuwepo kwa dawa ya kutibu RVF kwa binadamu.

Akitoa taarifa ya ugonjwa huo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, William Lukuvi, alisema serikali mkoani hapa imeomba jumla ya sh 41,255,000 kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa huo, yakiwemo malipo ya wauguzi kwa kazi za ziada wanazozifanya kwa kuhudumia wagonjwa wa RVF.

Alisema tangu kumalizika kwa ziara ya manaibu waziri watatu, kumekuwepo na ongezeko la vifo 10 na wagonjwa 12 mkoani hapa.

Mpaka sasa, alisema jumla ya watu 110 wameugua ugonjwa huo tangu ulipoingia mkoani hapa. Waliougua, wakatibiwa na kupona ni 21 ambapo watu 34 wameshafariki kutokana. Jumla ya watu 55 bado wamelazwa katika hospitali na vituo mbalimbali vya afya mkoani hapa wakiendelea na matibabu.

Alisema jumla ya vijiji 90 vimeathirika na RVF mkoani hapa ambapo ng’ombe 200,410, mbuzi 81,949 na kondoo 37,789 kutoka katika vijiji hivyo vya wilaya zote mkoani hapa wameathirika na ugonjwa huo.

Lukuvi alisema katika kukabiliana na homa hiyo, mkoa umechukua hatua mbalimbali, ikiwemo kutoa vyandarua vyenye dawa 200 katika maeneo walikolazwa wagonjwa, mablanketi 200, vipeperushi 4,000 vyenye ujumbe maalumu na elimu dhidi ya ugonjwa huo katika vijiji 56.

Vilevile, alisema serikali mkoani hapa imepokea jumla ya dozi 100,00 za RVF ambazo zimegawanywa katika wilaya zote na kutumika kwa baadhi ya mifugo. Mkoa bado unatarajia kupokea dozi nyingine 195,000 wiki ijayo.

Kutokana na kuwepo kwa idadi kubwa ya mifugo mkoani hapa, alisema kuwa chanjo hizo zilizotolewa na zinazotarajiwa kuletwa hazitakidhi mahitaji ya mifugo yote, hivyo serikali inatakiwa kuongeza nguvu zaidi katika kuleta chanjo mkoani hapa ili kupunguza kasi ya maambukizi.

Mikakati iliyowekwa na mkoa hivi sasa ni kupeleka dawa ya chanjo itakayowasili wilayani na kununua vifaa vya kuchanjia, kusimamia karantini ya usafirishaji wa mifugo kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine.

Alisema jitihada zinaendelea pia katika kuhamasisha na kusimamia uogeshaji mifugo, kufuatilia mlipuko wa ugonjwa huo kwa binadamu na mifugo katika maeneo ya vijiji na kutoa elimu zaidi kwa wakazi wa Dodoma.

Ongezeko la wagonjwa wa RVF na vifo mkoani hapa, limesababishwa na wananchi kujisahau na kuanza kula nyama ya ng’ombe, mbuzi na kondoo bila kufuata masharti ya Afya.

Mwishoni mwa wiki, gazeti hili lilishuhudia baadhi ya wananchi katika Kijiji cha Vikonje, wakila mzoga ambao Ofisa Mifugo wa Kata ya Mtumba, aliyetambulika kwa jina moja la Kimoro, aliamuru uzikwe.

Ng’ombe huyo alifariki baada ya kugongwa na gari na alipopimwa, hakuonekana na maambukizo ya RVF, lakini afisa huyo alisema kwa tahadhari, nyama yake isiliwe.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.