UCHUNGUZI uliofanywa na Jeshi la Polisi kuhusu sakata la vijana watatu waliokamatwa jijini Mbeya hivi karibuni wakihusishwa na tukio la ujambazi wa kutumia silaha, umethibitisha kuwa walihusika na tukio hilo na si wafanyabiashara kama inavyodaiwa na baadhi ya ndugu zao.
Ripoti iliyoandaliwa na timu ya makachero waliotumwa jijini Mbeya kutoka makao makuu ya jeshi hilo, inaonyesha kuwa vijana hao walihusika kwenye jaribio la uporaji na kutupiana risasi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, jijini Dar es Salaam, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Peter Kivuyo, alisema upelelezi wa awali umekamilika na polisi wamejiridhisha kuwa vijana hao walishiriki katika tukio hilo.
Kivuyo, aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Geodfrey George aliyejeruhiwa sehemu ya nyonga upande wa kushoto, Ipyana Patson na Sambayeti Chacha waliokuwa wakimhudumia majeruhi huyo.
Utata kuhusu vijana hao uliibuka mara baada ya kukamatwa kwao kufuatia tukio la uporaji wa kutumia siala uliofanywa katika duka moja jijini Mbeya.
Watu waliohusika na tukio hilo, walifanikiwa kutoroka, lakini siku moja baadaye, polisi mkoani humo ilitangaza kuwakamata vijana hao watatu kwa tuhuma za kuhusika na tukio hilo, ambalo lilisababisha kifo cha askari polisi ambaye alikuwa mwanafunzi wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu Mzumbe, kampasi ya Mbeya.
Hata hivyo, watuhumiwa hao walidai kuwa alfajiri ya Machi 24, mwaka huu, walivamiwa na majambazi wakiwa kwenye nyumba ya kulala wageni ya Mapemba, Mbalizi, nje kidogo ya mji wa Mbeya na kupigwa risasi na kusababisha mwenzao huyo kujeruhiwa.
Siku iliyofuata, kundi kubwa la watu, waliodai kuwa wanawafahamu vijana hao, waliizingira ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, wakidai kuwa vijana hao wameonewa kwa sababu hawakuwa majambazi bali wafanyabiashara wa nyama.
“Upelelezi wa awali wa polisi umebaini kuwa watuhumiwa hao si wafanyabiashara wa ng’ombe kama baadhi ya ndugu zao walioandamana walivyosema.
“Upelelezi huo umebaini kuwa, mtuhumiwa aliyekutwa na jeraha katika paja la kushoto jirani na nyonga, alihusika kwenye tukio hilo kwa kuwa tume imewahoji watu 24 wakathibitisha kuwa hapakuwa na ujambazi kwenye eneo hilo (la nyumba ya kulala wageni),” alisema Kivuyo.
Alisema kati ya watu waliohojiwa, ni daktari wa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, ambaye alikiri kumpokea majeruhi huyo na kueleza kuwa wakati alipofikishwa hospitalini hapo, damu ya majeruhi huyo ilikuwa imeshaganda, ikiwa ni dalili kuwa jeraha hilo halikuwa la siku hiyo.
“Aidha, wataalamu wa silaha wamebainisha kuwa, kigololi kilichotolewa kwenye jeraha la Godfrey, kimetoka kwenye silaha aina ya shotgun, inayodaiwa kutumiwa na mmiliki wa duka lililokuwa limevamiwa, Simon Kahemela, kwenye mapambano hayo alipokuwa akijihami.
“Mbali na daktari huyo, wengine waliohojiwa ni mjumbe wa nyumba kumi, wahudumu na majirani wanaoishi karibu na nyumba ya kulala wageni ya Mapemba pamoja na wafanyabiashara wa maduka ya nyama.
“Kadhalika, wamiliki wa duka hilo, na mkewe aitwaye Irene, walimtambua majeruhi huyo na kueleza kuwa alikuwepo siku ya tukio,” alisema Kamanda huyo.
Alisema polisi inasubiri taarifa zaidi za wataalamu wa silaha na upelelezi ukikamilika, watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani kwa makosa ya wizi na kutumia silaha.
Tukio hilo lilitokea Machi 23, mwaka huu, saa 12 jioni ambapo watu wanne wanaodhaniwa majambazi, walivamia duka la Ndiyo Super Marketi lililopo kwenye barabara kuu ya Mbeya-Zambia eneo la Forrest jijini Mbeya.
Katika tukio hilo, watuhumiwa hao walifanikiwa kupora sh milioni moja, simu na vitu mbalimbali ambavyo hata hivyo viliokolewa wakati wa shambulio la kutupiana risasi kati ya Simon na mmoja wa watuhumiwa hao.
Wakati wa tukio hilo, Simon alitumia silaha yake aina ya shotgun kupambana na majambazi hayo. Alifanikiwa kumpiga risasi ya kichwa jambazi aliyekuwa na mfuko uliokuwa na mali hizo ambaye alifariki dunia hapo hapo.
Simon pia alimpiga risasi ya mguu wa kushoto, jambazi mwingine wakati wa mapambano hayo. Majambazi hayo pia yalimuua kwa risasi mwanafunzi wa mwaka wa pili, kitivo cha sheria, Chuo Kikuu cha Mzumbe Kampasi ya Mbeya.
Watuhumiwa hao walikamatwa saa 24 baada tukio hilo kutokana na taarifa za raia wema waliowaona wakiingia kwenye nyumba hiyo ya wageni.