SIKU chache tu baada ya jarida la The Economist la Uingereza kuukosoa utawala wa Rais Jakaya Kikwete, jarida jingine linaloheshimika sana huko Marekani, Wall Street Journal, limetoa ripoti inayoonyesha kuwa Tanzania inaserereka katika masuala ya uchumi.
Ripoti ya mwaka huu ya ‘Uhuru wa Kiuchumi’ ya jarida hilo, imeorodhesha nchi 161 katika maeneo 10 ya kiuchumi kama vile hakimiliki, kiwango cha kodi na ujasiriamali huku Tanzania ikionyeshwa kushika mkia kwa nchi za Afrika Mashariki.
Ripoti hiyo imetolewa na Taasisi ya Marekani ya Heritage Foundation na jarida la Wall Street.
Uganda iliongoza Afrika Mashariki ikishika nafasi ya tano kati ya nchi 40 za kusini mwa jangwa la Sahara Afrika na 59 duniani.
Hong Kong ilishika nafasi ya kwanza duniani huku Marekani ikishika nafasi ya nne na Uingereza ya sita.
Mauritius iliziongoza nchi za kusini mwa jangwa la Sahara Afrika ikifuatiwa na Botswana, Afrika Kusini na Namibia.
“Uchumi wa Uganda una kiwango cha wastani wa asilimia 63.4 za uhuru,” ripoti hiyo ilibainisha.
Kenya inashika nafasi ya pili Afrika Mashariki baada ya kuorodheshwa katika nafasi ya nane kwa nchi za kusini mwa jangwa la Sahara huku Tanzania ikishika nafasi ya 15 kwa nchi hizo.
Uganda ilipata kura nyingi katika uhuru wa kikazi kwa kupata asilimia 94, wakati uhuru wa kifedha ilipatiwa asilimia 87.1. Hiyo ni kulinganisha na Kenya iliyopata asilimia 65 kwa uhuru wa kikazi na Tanzania iliyojikongoja kwa kupata asilimia 49.4.
Utendaji wa Uganda katika uhuru wa kibiashara ulipewa asilimia 58.8.
“Serikali ya Uganda imeonyesha mafanikio katika uendeshaji wa biashara huria, lakini kuna matatizo ya ufanisi na uwazi katika utekelezaji wa taratibu za kodi na mapato, mipaka ya uingizaji bidhaa, udhaifu katika utekelezaji wa hatimiliki na kukithiri kwa rushwa ambako kunaigharimu biashara,” ripoti hiyo ilisema.
Katika suala la kupambana na rushwa, Uganda iko chini kwa kupata asilimia 25 na hatimiliki asilimia 30. Uhuru wa biashara ilipata asilimia 54.1.