Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Tendwa atishia kufuta chama cha Mtikila
Tendwa atishia kufuta chama cha Mtikila
By Habari Tanzania | Published  04/5/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Irene Mark


MSAJILI wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa, ametoa onyo na kutishia kuvifutia usajili baadhi ya vyama vya siasa visivyofuata masharti ya kuandikishwa kwake, kikiwamo Democratic Party (DP), kinachoongozwa na Mchungaji Christopher Mtikila.

Tendwa alitoa onyo hilo jana, muda mfupi baada ya kutoa hati ya usajili wa muda kwa chama kipya cha siasa kijulikanacho kama National Progressive Democratic Party (NPDP).

Alivitaja vyama vingine ambavyo vipo katika orodha ya vyama anavyofikiria kuvifutia usajili kutokana na kushindwa kutekeleza matakwa kisheria kuwa ni, Forum for the Restoration of Democracy (FORD) na National Reconstruction Alliance (NRA) vyenye maskani yake jijini Dar es Salaam.

Alisema vyama hivyo vyote, kikiwamo DP, vimeshindwa kufanya uchaguzi kulingana na katiba zake kama inavyoelekezwa na sheria namba tisa ya vyama vya siasa.

Akifafanua, Tendwa alisema kwa mfano FORD, ilitakiwa kufanya uchaguzi Oktoba mwaka jana, lakini hadi sasa chama hicho hakijafanya hivyo pamoja na kukumbushwa zaidi ya mara tatu na ofisi yake.

“Tuliwapigia simu mara mbili kuwakumbusha, lakini hawakujibu, tukawapa taarifa za kuwafuta kwa kuwa hawana uongozi.

“Zaidi ya miezi sita, chama FORD kimekaa bila viongozi kwa mujibu wa sheria na kanuni za usajili wa vyama vya siasa… ifikapo Aprili 16, kama hawatakuwa na uongozi tutakifuta,” alisema Tendwa.

Mbali na FORD, chama kingine kitakachofutiwa usajili ni NRA ambacho kinatakiwa kufanya uchaguzi ifikapo mwishoni mwa Aprili.

Alisema NRA iliomba muda wa ziada ambao hata hivyo umekwisha na kwamba Aprili 10, mwaka huu atakutana na viongozi wa chama hicho kuzungumzia suala hilo.

Pamoja na hayo, Tendwa alisema Chama cha Democratic (DP), kimepewa taarifa ya tahadhari ya kufanya uchaguzi, hivyo kinatakiwa kuwa na viongozi ifikapo Juni mwaka huu.

“Kama ilivyokuwa kwa vyama vingine, DP tumewapa ‘notice’ na wao wanatakiwa kufanya uchaguzi Juni mwaka huu… ni utaratibu wa kisheria hivyo unapaswa kufuatwa,” alisema Tendwa.

Hata hivyo, Tendwa alisema ni wajibu wa msajili kuvikumbusha vyama kufanya uchaguzi kwa wakati na ikibidi kuvifuta kabisa vitakavyoshindwa kufanya hivyo.

Wakati huo huo, mbunge wa Biharamulo Magharibi kwa tiketi ya Tanzania Labour Party (TLP), Fares Kabuye, amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho kuziba nafasi ya Alipipi Kasyupa aliyetimuliwa uanachama na kwenye nafasi hiyo.

Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema, aliiambia Tanzania Daima jana kuwa, hatua hiyo imetokana na maamuzi ya kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho, iliyokutana Dar es Salaam, juzi.

Alisema NEC imeridhika kuwa, Kasyupa amekuwa akishirikiana na baadhi ya wanachama kuihujumu TLP.

Kwa mujibu wa Mrema, kikao hicho pia kimemchagua Mbunge wa zamani wa chama hicho, Jimbo la Kyerwa, Benedicto Mutungirehi, kuwa Katibu Mwenezi kuziba nafasi ya Octavin Matikila aliyehamia Chama Cha Mapinduzi (CCM) mapema mwaka huu.

Nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Bara, imechukuliwa na Richard Lyimo.

Mrema alitaja viongozi wengine waliotimuliwa kuwa ni Mhasibu Mkuu, Richard Rubandiza na Msaidizi wake Steven Ng’anzu na kuongeza kuwa TLP imeazimia kuwafikisha mahakamani kwa madai ya kuwapo ubadhirifu wa fedha katika hesabu za chama hicho.

“Hayo ndiyo maamuzi. Chama kimeamua kujisafisha na kuziba nafasi zilizoachwa wazi. Kwa hatua hiyo, nasema TLP bado ipo, kwani wajumbe 57 kati ya 80 wa NEC walihudhuria mkutano huo na wamepitisha azimio kuwa mimi ni mwenyekiti halali wa chama hicho,” alitamba Mrema.

Maazimio mengine ya chama hicho, ni pamoja na kupitisha bajeti ya chama kwa kipindi cha mwaka wa fedha wa 2007/2008 na kupitia ripoti ya ukaguzi wa hesabu za fedha za chama hicho.

Ili kuonyesha kuwa chama kiko hai, Mrema alisema ana mpango wa kusambaza mkanda wa video wa mkutano huo kuwaonyesha wanachama kuwa TLP bado iko hai.

Pia alisema kikao hicho kimeridhia pendekezo la TLP kutaka kuungana na CUF katika shughuli za kisiasa kwani kimebaini kuwa bila kuungana, vyama vya upinzani haviwezi kushinda.

Mrema aliwahi kukaririwa kuwa endapo atang’atuka, mtu anayefikiria kumwachia chama ni Kabuye kwa madai kuwa ni mpole, mwenye busara, hekima na uwezo mkubwa wa kuongoza.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.