Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Lipumba ampa Kikwete mtihani wa uchumi
Lipumba ampa Kikwete mtihani wa uchumi
By Habari Tanzania | Published  04/5/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:
na Kulwa Karedia


MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, jana alifanya tathmini na kutoa mwelekeo wa maamuzi kadhaa ya kiuchumi ya Serikali ya Awamu ya Nne.

Lipumba mmoja wa viongozi wa kisiasa aliyejenga utamaduni wa kuichambua serikali, alifanya hivyo jana wakati akiichambua hotuba ya mwishoni mwa mwezi uliopita ya Rais Jakaya Kikwete.

Mwanasiasa huyo ambaye kitaaluma na bingwa wa uchumi na mtu aliyepata kuwa profesa wa somo hilo katika Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, na kwa vipindi tofauti akawa mshauri wa uchumi wa Rais Ali Hassan Mwinyi na Yoweri Museveni wa Uganda, alitoa mtazamo wake katika masuala kadhaa ambayo Kikwete aliyagusia katika hotuba yake.

Katika tathmini yake hiyo, Lipumba aliyekuwa ameambatana na Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad, makao makuu ya CUF, Buguruni, Dar es Salaam, alibainisha kuwapo kwa kasoro kadhaa za kiuchumi katika mikopo ya uwezeshaji wajasiriamali, ambayo katika siku za karibuni, imekuwa ikijulikana kwa jina la ‘Mabilioni ya Kikwete’ na namna mabenki na serikali zilivyosimamia na kuendesha mchakato wa upatikanaji wake.

Aidha, Lipumba alizungumzia ugonjwa wa homa ya bonde la ufa (RVF), na akaeleza kwa mtazamo wake namna serikali ilivyozembea katika kuudhibiti.

Mwishoni mwa tathmini yake, Lipumba alionyesha wasiwasi wake kuhusu kuwapo kwa mazingira ya Ofisi ya Rais Ikulu kutumia fedha nyingi kuliko kiasi kilichopangwa katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa bejeti 2007/2008.

Kuhusu mikopo kwa wajasiriamali, Lipumba alisema uamuzi wa serikali kuiratibu kisiasa, ni moja ya sababu zilizosababisha kushindwa kutimizwa kwa malengo yaliyokusudiwa.

Alisema utaratibu wa kuwataka waombaji kupitisha maombi kwa uongozi wa serikali za mitaa au kijiji, huku ikijulikana bayana kuwa nyingi kati ya hizo zinaongozwa na CCM, ni jambo linalosababisha wasio wanachama wa chama hicho kutopata.

Kutokana na hali hiyo, Lipumba alisema ili waweze kufanikiwa, waombaji wengi wamekuwa wakilazimika kuwa wanachama wa CCM ili wafanikiwe kupata mikopo hiyo.

Alisema kwa kuzingatia ukweli kuwa fedha hizo zinatokana na walipakodi wote, wana CCM na wasio wana CCM, basi si vyema kwa wanachama wa chama hicho peke kupatiwa mikopo hiyo.

Lipumba pia alizilaumu benki za NMB na CRDB kwa kutoa mikopo kwa kasi ndogo, hata kusababisha kuwapo kwa wasiwasi kwamba hali isiporekebishwa, basi mikopo itakuwa haijamalizika hata baada ya bajeti mpya ya mwaka 2007/08.

“Hali hii kwa kweli ni ya kusuasua zaidi kwani hadi kufikia Machi 23 mwaka huu NMB ilikuwa imetoa kiasi cha sh bilioni 1.419 kwa mikoa yote 19 isipokuwa mikoa ya Ruvuma na Rukwa, ambapo katika zoezi hilo waombaji 2,013 wamepatiwa mikopo… NMB inatarajiwa kutoa mikopo ya shilingi bilioni 15.5,” alisema.

Alisema kiwango hicho walichotoa hadi hivi sasa kiko chini ya asilimia 9.2 ya kiasi chote wanachotarajiwa kutoa, hivyo kuonyesha namna walivyo na kasi ndogo.

Mbali ya hilo, Lipumba alisema kasoro nyingine inaonekana katika idadi kubwa ya maombi ya wakopaji walioomba mikopo kuliko kiasi kilichotengwa.

Akitoa mfano, alisema kupitia benki hiyo ya NMB, kiasi cha sh bilioni 105. 2 walichoomba watu ni mara saba ya kiasi ambacho benki hiyo imepatiwa kwa ajili ya wajasiriamali wadogo wadogo.

Kwa upande wa CRDB, Lipumba alisema benki hiyo imetoa asilimia 2.6 ya mikopo yote iliyotarajiwa kutolewa na benki hiyo kwa SACCOS.

Kuhusu ugonjwa wa RVF, Prosefa Lipumba alisema zoezi zima la utoaji wa huduma ya chanjo na takwimu zinazotolewa zimegubikwa na siasa.

“Kama si siasa, unadhani hili suala lingekuwa halijapata tiba? Kwani serikali yetu ilipewa tahadhari ya ugonjwa huu karibu miaka mitano iliyopita, lakini cha ajabu ilikaa kimya hadi ugonjwa umetokea, hii ni siasa,” alisema.

Alisema hata mashine za kupimia ugonjwa huo zimeingizwa nchini mwanzoni mwa mwaka huu, kabla ya hapo sampuli zilipelekwa nchi za Kenya na Afrika Kusini kwa ajili ya uchunguzi.

Kuhusu matumizi makubwa ya fedha, Lipumba alisema chama chake kimeshtushwa na matumizi makubwa ya fedha za serikali zinazotumika Ikulu, na akamtaka Rais Kikwete kupunguza kasi ya matumizi katika ofisi yake.

Alisema matumizi katika robo ya kwanza ya bajeti yamekuwa makubwa kinyume cha makadirio.

“Ofisi ya Rais inaongoza katika ukosefu wa nidhamu katika matumizi ya fedha za serikali ambapo katika robo ya kwanza ya bajeti ya mwaka 2007/08 Consolidated Fund ambayo hujumuisha bajeti ya Ikulu na kulipia madeni ilikuwa sh bilioni 54,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema kiasi hicho ni zaidi ya mara mbili ya sh bilioni 23.4 ambazo ndiyo bajeti iliyotengwa kwa ajili hiyo.

“Jamani matumizi haya ni makubwa mno kwa kipindi hiki kifupi… hizi ni fedha za wananchi, hivyo lazima tuzungumze kwa nguvu zote juu ya matumizi haya, ambayo yanaonekana kuwa makubwa kupita kiasi,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema sababu nyingine inayochangia kuongezeka kwa matumizi ya fedha hizo ni safari nyingi za Rais Kikwete nje ya nchi hali iliyochangia kutokuwepo na nidhamu.

“Suala hili limechangiwa na mambo mengi… kumekuwa na safari nyingi za nje, na nadhani kuna mambo fulani fulani ambayo tunapaswa kuyakemea kwa nguvu zote ili kuokoa fedha hizi,” alisema Profesa Lipumba.

Hii si mara ya kwanza kwa Profesa Lipumba kutoa kauli kama hiyo. Mapema mwaka jana, alishutumu ofisi ya Waziri Mkuu kutengewa kiasi kikubwa cha fedha kuliko hata kile kilichopelekwa Ikulu.

“Matumizi ya Waziri Mkuu (Vote 25) ndiyo yenye kasi kali ya kuongezeka kwa matumizi ya fedha, kwani bejeti yake sasa imefikia bilioni 4/- ambapo awali ilikuwa bilioni 1.7/-. Ongezeko hili ambalo ni sawa na asilimia 130, limezidi hata Ikulu yenyewe. Matumizi haya yote yanatoka wapi?” alihoji Lipumba wakati huo.

Wakati huo, Lipumba aliishutumu serikali ya awamu ya nne akisema imeongeza kasi ya kutisha katika gharama za uendeshaji wa serikali.

Akitoa mfano, alisema matumizi ya kawaida ya wizara yameongezeka kutoka sh trilioni 1.7 hadi sh trilioni 2.0, kiasi ambacho ni sawa na ongezeko la asilimia 17, kitu alichokielezea kuwa kinatisha kwa nchi maskini kama Tanzania.

“Kasi hii ya ongezeko la bajeti kwa kila wizara imetoka wapi? Gharama za uendeshaji sasa zinatisha… au hii ndiyo ari, kasi na nguvu mpya aliyotangaza Rais Jakaya Kikwete kabla ya kuingia madarakani? Sisi CUF tunamtaka achukue hatua madhubuti za kupambana na matumizi haya, ni makubwa kwa nchi masikini kama Tanzania,” alisema Lipumba wakati huo.

Alisema kwa kuwa bajeti ya Tanzania bado inategemea misaada ya wafadhili wa nje kwa asilimia 46, Ofisi ya Waziri Mkuu haikutakiwa kuonyesha kasi ya matumizi makubwa kama hayo, kwa vile kufanya hivyo ni sawa na kuwaongezea mzigo wananchi.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by John)
    Rating
    Good news...JK awekwe kiti motto juu ya uchumi wa Nchi.Msafara umekuwa mkubwa mno na hakuna wanachokifanya wakija nje zaidi ya shopping.
     
Submit Comment


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.