JITIHADA za serikali kuunganisha wizara, idara, tasisi, mikoa na wilaya katika mtandao mmoja wa mawasilianio kwa dhamira ya kuongeza kasi ya utendaji, imeanza kutekelezwa kwa vitendo.
Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein, jana aliweka jiwe la msingi wa ujenzi wa jengo litakalokuwa na mitambo ya mawasiliano inayounganisha taasisi zote zilizopo chini ya serikali katika kufanikisha mradi ujulikanao kama ‘serikali mtandao’ au e-governance kwa Kiingereza.
Pamoja na mambo mengine, mfumo huo wa mawasiliano unatarajiwa kuwezesha maamuzi ya kiutendaji kufanyika kwa kasi na kuwafikia wahusika kwa ajili ya utekelezaji wa haraka.
Mafanikio hayo yataiwezesha serikali kufikia kwa haraka zaidi azma yake ya kuleta maendeleo kwa kasi.
Inatarajiwa pia kuwa, juhudi hizo zitaisaidia sekta ya umma kujenga mazingira mazuri ya utoaji huduma nzuri na ya haraka na kuweka kumbukumbu, hivyo kuharakisha maendeleo ya taifa.
Akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi, Dk. Shein alisema kuwa jengo hilo litakuwa kitovu cha serikali-mtandao, hivyo kuweza kuwa na mawasiliano rahisi serikalini na pia wananchi watapata unafuu katika kuwasiliana na serikali.
Alisema nia ya serikali ni kuifanya serikali-mtandao kuwa ni sehemu muhimu katika utekelezaji wa sera ya taifa ya habari, elimu na teknolojia, ambapo nguzo mojawapo kati ya 10 ilikuwa ni kuimarisha sekta ya miundombinu na huduma za kiuchumi.
“Jengo hili ni muhimu kwa ajili ya kuwa na serikali-mtandao, ambayo itasaidia kongeza tija na ufanisi katika uendeshaji wa sekta ya umma, kupunguza gharama za mawasiliano serikalini, kupanua wigo wa upatikanaji wa taarifa muhimu katika kila ngazi ya serikali na kuiwezesha serikali kuwa na mawasiliano rahisi na wananchi na wahisani,” alisema Makamu wa Rais.
Pia alisema jengo hilo litasaidia kutoa nafasi za kufanyia kazi katika Ofisi ya Rais na Menejimenti ya Utumishi wa Umma, kwani kupanuka kwa wizara hiyo kumekuwa sambamba na ukuaji wa ajira nchini.
Aliitaka wizara hiyo kuhakikisha kuwa ujenzi wa jengo hilo unakamilika haraka na litakapoanza kutumika, linatimiza malengo yake ya msingi, ili kuunganisha serikali kwa njia ya mtandao kwa lengo la kuiwezesha ifanye kazi kama chombo kimoja na kwa ufanisi zaidi.
Pia alisema mkakati huo ujielekeze kwenye kujenga uwezo wa watumishi katika ngazi zote, ikitiliwa maanani kuwa watumishi ndio nguzo muhimu ya msingi ya kutekeleza mkakati huo wa serikali mtandao.
Hata hivyo, alisema serikali ilichelewa kuingia katika matumizi ya mtandao huo kwa kuwa teknolojia hiyo inahitaji mtaji mkubwa kuifanikisha.
“Kwa vile nchi yetu ni maskini, tuliamua kukamilisha kwanza zile huduma za msingi zaidi katika jamii kama vile huduma za afya, elimu, mawasiliano ya barabara na kadhalika, ambazo mpaka sasa tunaendelea kuzifanya, ili ziwe bora zaidi.
“Pia teknolojia ya kompyuta na mtandao wake inahitaji utaalamu, kwa maana ya watendaji wenye uwezo wa kumudu teknolojia yenyewe. Kwa hiyo isingekuwa ni jambo la busara kuikumbatia teknolojia ambayo hatukuwa na uwezo wa kuimudu,” alisema.
Awali, akitoa maelezo ya jengo hilo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia, alisema kuwa jengo hilo litakalokuwa la ghorofa tano, linajengwa na serikali kwa ushirikiano na Serikali ya Japan na ujenzi wake utagharimu sh bilioni 4 hadi kukamilika.
Alisema kati ya fedha hizo, Serikali ya Japan imetoa sh bilioni moja na zilizosalia zitatolewa na serikali.
Waziri Ghasia alisema ofisi yake, chini ya programu ya kuboresha utumishi wa umma, iliandaa mpango mkakati wa matumizi ya kompyuta, ambao uliridhiwa na Baraza la Mawaziri Aprili 2, 2004.
Mpango huo umeiwezesha kuiweka wizara kwenye njia inayoongoza kufikia serikali-mtandao, ili kuendana na mabadiliko ya kisayansi na teknolojia ulimwenguni.
Alisema ujenzi wa jengo hilo ulianza Januari 30, 2006 na linatarajiwa kukamilika katika kipindi cha mwaka huu wa fedha.