VIONGOZI wa kijiji kimoja mkoani Mara, wameuza eneo la ekari 10 kwa kampuni ya uchimbaji madini na kusababisha malalamiko kutoka kwa wananchi.
Miongoni mwa maeneo ambayo yako ndani ya ardhi iliyouzwa na viongozi hao katika mazingira ya kutatanisha na ambayo tayari yameanza kulalamikiwa, ni shule moja ya msingi na ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambazo ziko katika hatua ya mwisho kukamilika kiujenzi.
Hatua hiyo ya viongozi wa kijiji imesababisha malalamiko juu ya uuzwaji huo wa ardhi, na sasa suala hilo limeshafikishwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara na viongozi wa CCM, ambao wanalalamikia kuuzwa kwa ofisi yao kinyemela.
Habari ambazo Tanzania Daima imezipata zinaeleza kuwa, tayari Mkuu wa Mkoa wa Mara, Isidori Shirima, ameombwa kuingilia kati mgogoro huo wa ardhi unaofukuta katika Kijiji cha Nyamichare, Kata ya Kibasuka wilayani Tarime.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake 20 aliofuatana nao, Katibu wa CCM wa Kijiji cha Nyamichare, Sairo Wambura, alidai mbele ya waandishi wa habari mjini hapa kuwa, baadhi ya viongozi hao, wakiongozwa na mwenyekiti wa kijiji hicho, Abel Maginga, wameuza ardhi yenye ukubwa wa ekari 10.
Alidai kuwa, ardhi hiyo iliuzwa mwaka jana kwa wamiliki wa mgodi wa dhahabu wa North Mara.
Wambura alizidi kudai kuwa, ardhi hiyo iliyouzwa bila ya ridhaa ya serikali ya kijiji hicho, inajumuisha eneo la Shule ya Msingi Nyakunguru C na ndani yake kulikuwa na jengo la ofisi ya CCM, ambalo lilikuwa katika hatua za awali za ujenzi.
Alidai kuwa, baada ya kuuza eneo hilo, viongozi hao sasa wako mbioni kuuza pia eneo lililosalia la ekari 24, katika mazingira hayo hayo ya siri, huku uongozi wa mgodi wa North Mara ukiwa mbioni kulifanyia tathimini kabla ya kulinunua kwa lengo la kupanua eneo la mgodi.
Alifafanua kuwa, wamejaribu kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufikisha malalamiko yao katika ngazi husika za kata na wilaya, lakini hawakupata msaada wowote na ndiyo maana wameamua kuuomba uongozi wa mkoa uingilie suala hilo.
Uongozi wa CCM wilayani Tarime umekiri kupokea malalamiko hayo ya kuuzwa kwa ardhi hiyo, likiwemo jengo la chama hicho na kuongeza kuwa, Oktoba mwaka jana, uliwaandikia viongozi wa Kata ya Kibasuka ukilalamikia kitendo hicho, lakini hadi sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa kurekebisha kasoro hizo.
Kwa upande wao, uongozi wa mgodi wa North Mara unaomilikiwa na kampuni ya uchimbaji madini ya Barrick, umekiri kununua eneo hilo kutoka kwa uongozi wa kijiji hicho cha Nyamichare kwa gharama ya sh milioni 6.2 na kufafanua kwamba, wananchi wanapaswa kuwasiliana na viongozi wao ili kupata taarifa sahihi ya manunuzi hayo.
Shirima alipoulizwa kuhusu suala hilo, alikiri kupokea taarifa za malalamiko hayo na akaahidi kumuagiza Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Stanley Kolimba, kulitafutia suala hilo ufumbuzi haraka iwezekanavyo.