KAMATI ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, imesikitishwa na hatua ya serikali kutothamini Taasisi ya Utangazaji Tanzania (TUT), kwa kushindwa kuipatia fedha za kutosha kuyafanyia ukarabati baadhi ya majengo yake, ambayo kwa sasa yana hali mbaya.
Wajumbe wa kamati hiyo walionyesha wazi kusikitishwa na hali ya uchakavu wa majengo ya Televisheni ya Taifa (TvT), walipofanya ziara jana.
Walionyesha kutofurahishwa kwa serikali kushindwa kutoa fedha za kukamilisha ujenzi wa jengo moja ambao ulianza mwaka 1989.
Jengo hilo la ghorofa mbili, ambalo ujenzi wake uliwekewa jiwe la msingi mwaka 1995 na Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, nalo limechakaa kutokana na kutoendelezwa mpaka leo.
Baadhi ya wabunge walihoji sababu za kutokamilika kwa jengo hilo mpaka sasa. Mmoja wa wabunge hao, Maulidah Komu, alisema mradi mkubwa kama huo bila shaka ulipelekwa bungeni, ukajadiliwa na bajeti yake ilipitishwa baada ya kufanyiwa mchanganuo.
“Sasa kama mchanganuo wa bajeti ulifanyika, naamini fedha zilitolewa, lakini zimekwenda wapi?” alihoji.
Alisema kama serikali imeshindwa kumalizia jengo hilo, ni vema iombe msaada toka kwa wafadhili, kama ambavyo imekuwa ikifanya sehemu nyingine, na baadaye warudishe fedha hizo.
Hata hivyo, kiasi cha fedha zilizotumika na kilichobaki katika ujenzi wa jengo hilo, hakikufahamika mara moja hata baada ya wabunge hao kuhoji. Uongozi wa TUT uliahidi kujibu hoja zote za wabunge kwa maandishi.
Aidha, mkurugenzi wa TUT, Tido Mhando, aliiambia kamati hiyo kuwa majengo mengi yanayomilikiwa na taasisi hiyo ni mabovu na yanahitaji ukarabati wa hali ya juu au kukamilisha ujenzi wake.
Wakati huo huo, Mhando alilalamikia pia ufinyu wa bajeti inayotolewa na serikali kwa ajili ya taasisi hiyo. Alisema kuwa kwa muda mrefu sasa, serikali imekuwa haiipatii TUT fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Alisema iwapo serikali itaipatia bajeti ya maendeleo kwa miaka mitatu mfululizo, TUT itaweza kujiendesha yenyewe na haitakuwa tegemezi kama ilivyo hivi sasa.