SERIKALI imesema kuwa, upo uwezekano wa kuenea zaidi kwa ugonjwa wa homa ya bonde la ufa (RVF) na hivyo kuongezeka kwa madhara yatokanayo na ugonjwa huo nchini.
Hayo yalibainishwa jana na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo, Anthony Diallo, alipokuwa akifungua mkutano wa wakuu wa mikoa sita, wataalamu wa afya na baadhi ya wakuu wa wilaya kutoka katika maeneo yaliyoathirika na homa hiyo hatari.
Alisema uwezekano wa kuongezeka kwa maambukizi hayo, unatokana na hali ya hewa ya mvua za masika zinazoendelea kunyesha katika maeneo mengi nchini.
Diallo alisema kuendelea kunyesha kwa mvua hizo, kunatoa nafasi kwa mbu kuzaliana zaidi, na kutoa tahadhari kuwa, mifugo milioni mbili iliyopo katika ukanda wa bonde la ufa inapaswa kupatiwa chanjo haraka iwezekanavyo.
Alisema upatikanaji wa chanjo bado ni kikwazo kutokana na nchi nyingi kuwa na uhitaji wa chanjo hizo kwa ajili ya kuikinga mifugo yao isipate maambukizi.
Waziri huyo alibainisha kuwa, serikali iliagiza dozi milioni mbili za chanjo ya RVF kwa ajili ya mifugo, lakini mpaka sasa zimepatikana dozi 736,600 tu, ambazo hazitoshi kuchanja mifugo yote, hata katika maeneo ambayo yameathirika.
“Serikali inashughulika kuhakikisha chanjo zaidi zinapatikana na hivi karibuni natarajia kwenda Afrika Kusini kufuatilia chanjo hizo kwa taasisi zinazotengeneza,” alisema.
Alisema chanjo zilizotolewa awali zimepelekwa katika maeneo yenye maambukizi zaidi, zikiwemo wilaya tano za Mkoa wa Dodoma, ambazo tayari zimewekewa karantini ya mifugo.
Diallo alisema katika kukabiliana na maambukizi ya homa ya bonde la ufa nchini, serikali imechukua hatua mbalimbali za kuwaelimisha wananchi athari za ugonjwa huo kupitia vyombo vya habari, vipeperushi, semina na mikutano.
Alisema serikali imeandaa mpango wa dharura wa kitaifa wa kudhibiti ugonjwa wa homa ya bonde la ufa chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, ambao utagharimu jumla ya dola za Kimarekani 12,336,964.
Waziri Diallo alisema tayari mpango huo umeshawasilishwa kwa mwakilishi wa Umoja wa Mataifa hapa nchini, ili kusaidia kutafuta wahisani. Umoja huo ulishasema kuwa, upo tayari kusaidiana na serikali kutafuta fedha kwa ajili ya kugharamia mpango wa udhibiti wa ugonjwa huo, ambao tayari umeshaua makumi ya Watanzania.
Amebainisha kuwepo kwa athari za soko la nyama la nje ya nchi kutokana na homa hiyo, ambapo ameviomba vyombo vya habari kusaidia kuwaelimisha wananchi na kuwatoa hofu kuhusu homa ya bonde la ufa.
Mpaka sasa, jumla ya mikoa minane imethibitika kuathirika na homa hiyo ambayo ni Arusha, Manyara, Tanga, Kilimanjaro, Morogoro, Dodoma, Iringa na Mkoa wa Singida ambao una maambukizi mapya yaliyothibitishwa na maabara ya mifugo iliyoko wilayani Temeke (Dar es Salaam), Machi 23, mwaka huu.
Hadi Machi 20, mwaka huu, jumla ya ng’ombe 46,000, mbuzi 56,000 na kondoo 32,000 walikuwa wameathirika ambapo kati yao, ng’ombe 5,520, mbuzi 6,816 na kondoo 3,888 walikuwa wamekufa kutokana na RVF.
Uchunguzi uliofanywa na wataalamu wa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo, umebaini kuwapo kwa uelewa mdogo miongoni mwa wananchi, hasa wa Mkoa wa Dodoma, kuhusu madhara yatokanayo na kuchinja mnyama aliyeugua.
Aidha, imethibitika kuwepo kwa mazoea ya baadhi ya wananchi kuchinja mifugo pasipo kutumia huduma ya ukaguzi na kuonja baadhi ya sehemu za viungo vya wanyama kama vile maini kabla havijapikwa.
Akilihutubia taifa mwishoni mwa mwezi uliopita, Rais Jakaya Kikwete aliwahakikishia Watanzania kuwa, serikali itafanya kila lililo chini ya uwezo wake katika kukabiliana na homa hiyo.
Aliwataka wananchi wanaojishughulisha na mifugo kuchukua tahadhari zote ili kuhakikisha kuwa, hawaambukizwi homa hiyo.
Alitaja baadhi ya tahadhari hizo kuwa ni kuhakikisha watu wanaochinja mifugo wanakuwa na zana za kujikinga na watu wanatumia chandarua ili kujikinga na mbu wanaoeneza homa hiyo.