Na Nasra Abdallah
BARABARA ya Sam Nujoma inatarajiwa kutengenezwa kwa vipande vipande kutokana na pingamizi zilizowekwa mahakamani na baadhi ya wakazi waliojenga pembezoni mwa eneo la barabara hiyo.
Mhandisi wa Mfumo wa Mawasiliano ya Kompyuta wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Rickson Joseph, alisema hayo juzi, alipozungumza na Tanzania Daima kwenye maonyesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja Dar es Salaam .
“Ukweli ni kwamba katika ujenzi huo kuna baadhi ya nyumba zilizoko kwenye eneo la barabara zinazopaswa kuondolewa na nyingine upanuzi wa barabara unalazimu kuzikumba, na hizo ndizo zina malalamiko mahakamani, hatuwezi kuzibomoa mpaka mahakama itakapotoa uamuzi,” alisema.
Joseph alisema barabara hiyo inayotarajiwa kukamilika Juni mwaka 2007, itagharimu sh bilioni 12,973 na itakuwa na njia nne pamoja na njia ya waenda kwa miguu.
Barabara hiyo yenye urefu wa km 4 kutoka makutano ya Barabara ya Bagamoyo hadi Ubungo, itajengwa kwa kiwango cha lami na kuwekwa taa za kuongozea magari katika makutano ili kuepuka msongamano wa magari.