WAZIRI Mkuu mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rashid Mfaume Kawawa, amewataka wananchi kupambana na viongozi wa ushirika wanaotumia nyadhifa zao kujitajirisha badala ya kunufaisha walengwa kwa kupatiwa mikopo.
Kawawa alitoa kauli hiyo wakati akiwahutubia waumini wa dini ya Kiislamu kwenye baraza la Maulid lililofanyika kitaifa katika Chuo Kikuu cha Kiislamu, mjini hapa.
“Ushirika si sehemu ya kujitajirisha mtu binafsi, ni mahali pa kujiunga ili kupambana na umaskini,” alisema.
Alisema mara nyingi viongozi wa ushirika wakichaguliwa kushika nafasi mbalimbali, hujenga imani kuwa wamekwishatajirika.
“Viongozi wa aina hii lazima tupambane nao ili kuhakikisha ushirika wetu unadumu na kuwanufaisha wanachama wake,” alisema.
Pia alisema njia pekee ya kupambana na umaskini ni kujiunga katika vikundi vya uzalishaji mali na kutumia fursa za mikopo zinazotolewa na asasi mbalimbali katika kuendeleza miradi itakayowakwamua kiuchumi.
Hata hivyo, Kawawa amewaasa waumini wa dini ya Kiislamu kuhakikisha wanawapeleka watoto wao shule ili kupata elimu ya kutosha.
Awali akisoma salamu za Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (BAKWATA), Sheikh Ramadhani Sawaka alisema baraza hilo lina watoto yatima 100 ambao wanahitajika kugharamiwa na baraza hilo.
Alisema baraza hilo linahitaji zaidi ya sh milioni 50 ili kufanikisha mahitaji hayo.
Sheikh Sawaka alitoa wito kwa Waislamu nchini pamoja na watu wenye mapenzi mema kwa yatima, kusaidia upatikanaji wa kiasi hicho cha fedhas ili kufanikisha azma hiyo.