Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  CCM waanza kuchezeana rafu
CCM waanza kuchezeana rafu
By Habari Tanzania | Published  04/2/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Mathias Marwa, Tarime


JOTO la uchaguzi wa viongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), limeanza kupanda kwa baadhi ya vigogo wa chama hicho wilayani hapa, wanaodaiwa kuhofia kupokwa nafasi zao.

Katika kuhakikisha kuwa wanazilinda nyadhifa zao na maswahiba wao wa kisiasa ndani ya chama hicho, baadhi ya viongozi wameanza kutumia nyadhifa walizonazo kuwazuia wale wanaoonekana kuwa tishio kwao, kugombea uongozi katika wadhifa wowote.

Habari zilizoliikia Tanzania Daima, hivi karibuni zinaeleza kuwa, makundi mawili yenye uhasama wa kudumu ndani ya CCM wilayani hapa, yamekuwa yakijiwinda vikali huku kila moja likiwania kuchukua nafasi nyeti za uongozi wa chama wa wilaya.

Kundi moja, ambalo lina watu wenye ukwasi wa kutisha, na linalodaiwa kuwaweka mfukoni viongozi wa chama wa wilaya, linadaiwa kutumia nguvu kubwa ya pesa, kuwamaliza kabisa wapinzani wao kwa kuwazuia wasigombee nafasi yoyote ya uongozi katika uchaguzi huo.

Habari hizo zinaeleza kuwa, kundi la wenye ukwasi linajaribu kuwazuia makada walio katika kundi la makabwela kutogombea kabisa kwa sababu wanaungwa mkono na nguvu kubwa ya umma.

Mmoja wa viongozi ambaye amekwishajitokeza hadharani kupambana na kundi hilo la makabwela, ni Mwenyekiti wa Vijana wa CCM Mkoa wa Mara, Marwa Mathayo ambaye hivi karibuni alitangaza kuwapiga marufuku baadhi ya viongozi kushiriki katika uchaguzi.

Mathayo alitangaza marufuku hiyo wakati akifungua rasmi Ofisi ya Kata ya Koryo iliyo katika Jimbo la Uchaguzi la Rorya.

Alikaririwa akiwataka viongozi aliowataja kuwa wameshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wao ndani ya chama hicho, ambacho kinaisha baadaye mwaka huu, kutothubutu kuchukua fomu za kugombea.

Mathayo ambaye alitoa mchango wa sh 500,000 na kueleza kuwa ni jitihada zake za kuunga mkono juhudi za waliofanikisha ujenzi wa ofisi hizo za Kata ya Koryo, alisema kuwa marufuku aliyoitangaza ina lengo la kukiimarisha chama hicho.

Akifafanua kauli yake hiyo, alisema chama hicho kinahitaji kuwa na viongozi wachapa kazi na wawajibikaji, ili wananchi waendelee kuwa na imani nacho na kuendelea kukichagua kuiongoza nchi.

“Wale ambao hamkutekeleza majukumu yenu vizuri, ni heri msichukue fomu kabisa, hata sisi hatutawaunga mkono, msing’ang’anie madaraka maana mkishindwa hamtataka hata kusalimiana na walioshinda, badala yake ni kujenga chuki ambazo zinakitafuna chama,” alisema Mathayo.

Kauli hiyo ya Mathayo ambayo aliitoa mbele ya wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Kata, makamanda wa Umoja wa Vijana (UVCCM), madiwani, mabalozi na viongozi wa matawi, ilielezwa kama ni ujumbe aliotumwa kuufikisha kwa wapinzani wa kundi la wenye ukwasi ndani ya chama chao wilayani hapa.

Baadhi ya makada wa chama hicho waliokuwa kwenye hafla hiyo, walionyesha kushtushwa na kauli hiyo na kueleza sasa mapambano ya kuwania uongozi wilayani hapa, yameanza na kwamba kamwe kundi la makabwela wanaodaiwa kutotekeleza majukumu yao, halitakaa kimya, litajibu kwa nguvu kauli hiyo.

Walisema kundi hilo limeamua kutumia nguvu ya pesa ili kupitisha watu wao wengi katika uchaguzi, jambo ambalo walidai kuwa wanajua namna ya kulishughulikia.

Aidha, walibeza mchango wa sh 500,000 uliotolewa na Mathayo kusaidia ujenzi wa ofisi hizo, kwamba unalenga kuwapumbaza wananchi ili wawachague kutokana na pesa walizonazo.

Walidai kuwa, wana wasiwasi kama fedha hizo ni za Mathayo mwenyewe, na wengine walisikika wakidai kuwa zimetolewa na wanachama wawili wa chama hicho ambao wamefadhili ujenzi wa ofisi hizo kwa pesa zao binafsi.

Kauli nyingine ya Mathayo iliyoonyesha utata ni onyo alilolitoa dhidi ya baadhi ya wananchi na viongozi wa chama hicho

wanaopingana na kundi la wenye ukwasi wilayani hapa kuhusu mahali panapofaa kuwa makao makuu ya wilaya mpya ya Rorya itakapoundwa.

Akizungumza kuhusu makao makuu ya wilaya hiyo, alisema wananchi ni lazima watambue kuwa fedha za maendeleo, hutolewa kwa wilaya nzima na kisha hugawanywa kwa kila tarafa na baadaye katika kila kata kwa kutegemea mwongozo wa bajeti kwa malengo yaliyokusudiwa na kwa kipindi maalumu.

Malumbano ya ni wapi panafaa kuwa makao makuu ya wilaya mpya ya Rorya, yalianza baada ya Rais Jakaya Kikwete kutangaza azma ya serikali ya kulipa Jimbo la Rorya hadhi ya kuwa wilaya.

Baada ya kauli hiyo ya Rais Kikwete, uliibuka mvutano mkali baina ya wakazi wa jimbo hilo ya wapi makao makuu ya wilaya yanapaswa kuwa, na miji iliyokuwa ikipendekezwa na makundi mbalimbali kuwa inafaa ni Utegi, Randa na Shirati.

Katika hatua nyingine, Mathayo alikabidhi sare 60 za waimba kwaya wa kata tatu za Mang’ore, Bukwe na Koryo zilizotolewa na Diwani wa Koryo, Lameck Airo, ikiwa ni maandilizi ya ugeni wa Katibu Mkuu wa CCM, Luteni Yusufu Makamba, anayetarajiwa kufanya ziara wilayani hapa, baadaye mwezi huu.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.