VIONGOZI wa serikali ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DARUSO), ambao wanamaliza muda wao kesho, huenda wakafikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuhusika na ubadhirifu wa mamilioni ya shilingi.
Wanaotuhumiwa katika ubadhirifu huo ni rais anayemaliza muda wake, Mwita Magesa, Waziri Mkuu wake, Mathias Renatus na Waziri wa Fedha, Mwakarukwa Kaptain, ambao wote kwa pamoja wanatuhumiwa kudanganya, kutoa taarifa za uongo, kujaribu kutoa rushwa ili wasichunguzwe na kuiba mali ya umma inayofikia sh milioni 34.
Hayo yalibainika jana katika kikao cha mwisho cha bunge la serikali hiyo (USRC) kilichoitishwa kwa dharura na spika, Kamazima Idd, kujadili ubadhirifu huo.
Katika kikao hicho, wabunge walisomewa taarifa ya ubadhirifu wa sh milioni 34, unaodaiwa kufanywa na uongozi wa juu wa DARUSO, kwa kuandaa taarifa mbili tofauti, zinazoelezea matumizi ya fedha hizo.
Kabla ya kikao hicho kilichoketi kwenye Ukumbi wa TBA chuoni hapo, spika alisoma barua ya rais wa DARUSO anayemaliza muda wake, ambaye naye ni miongoni mwa watuhumiwa.
Rais huyo aliandika barua hiyo kwa lengo la kueleza kuwa hakitambui kikao hicho kwa kuwa bunge lilikuwa limeshavunjwa.
Lakini, waliohudhuria walihoji iwapo bunge lilikuwa limevunjwa na uongozi wa DARUSO kufikia kikomo, yeye (rais) alipata wapi mamlaka ya kusaini waraka huo akiwa kama Rais wa DARUSO?
Walihoji pia iwapo alikuwa hatambui kikao hicho, kwa nini alikiandikia barua na kutoa maelezo?
Alipomaliza kusoma waraka huo, spika alionya kuwa iwapo kuna watu walikuwa wameandaliwa kufanya fujo, wangeshughulikiwa kikamilifu kwa kuwa kikao hicho kilikuwa halali, kwani bunge hilo litavunjwa baada ya bunge jipya kuapishwa.
Taarifa iliyosomwa katika kikao hicho ilionyesha kwa ujumla kuwa Waziri wa Fedha wa serikali inayomaliza muda wake, Mwakarukwa Kaptain, alikuwa anapeleka bungeni bajeti inayoonyesha kiasi kidogo cha matumizi na kupeleka taarifa nyingine tofauti katika ofisi ya utawala ya UDSM ikionyesha kiasi kikubwa cha matumizi.
Taarifa hiyo inadai kuwa Machi 2, mwaka huu, DARUSO ilipeleka bungeni bajeti inaonyesha matumizi ya mwaka mzima wa 2006 yalikuwa sh milioni 18, matumizi ambayo wabunge waliyakataa kwa madai kuwa kilikuwa ni kiasi kikubwa mno.
Hiyo ndiyo iliyoleta wasiwasi na kusababisha bunge lifuatilie kwenye ofisi za utawala na kubaini kuwa kulikuwa na taarifa mbili tofauti zinazoonyesha bajeti ya DARUSO.
Hata hivyo, bunge hilo lilitupa lawama kwa mkaguzi mkuu wa ndani wa chuo kwa kuzembea hadi pesa nyingi kiasi hicho zikawa zinachotwa bila kudhibitiwa.
Wakichambua namna ubadhirifu huo unavyodaiwa kufanywa, waraka huo uliosomwa bungeni ulidai kuwa wakati taarifa za mkaguzi zinaonyesha kuwa fedha zilizotumika katika mwaka zilikuwa ni sh milioni 34, ripoti iliyowasilishwa bungeni inaonyesha kuwa matumizi ya mwaka yalikuwa ni sh milioni 18.
Baadhi ya matumizi mabaya yaliyoanishwa katika taarifa hiyo ni sh 900,000 zilizoidhinishwa na mkaguzi kwa ajili ya kulipa mafundi wa kutengeneza tovuti wakati ripoti iliyopelekwa bungeni DARUSO iliomba sh 500,000 kwa ajili hiyo.
Akichangia, mmoja wa wabunge alisema kuwa walikuwapo wanafunzi waliokuwa wameombwa wapatiwe kazi hiyo lakini wakaambiwa kuwa alikuwa amepatikana fundi atakayelipwa chini ya sh 300,000 walizoomba wao.
Taarifa inaonyesha kuwa waziri mmoja wa serikali hiyo alikuwa akitumia fedha zake kiasi cha sh 200,000 kwa ajili ya mawasiliano kwa makubaliano kuwa atalipwa.
Ingawa waziri huyo bado hajalipwa, taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa sh milioni tatu zimetumika kwa ajili ya mawasiliano, ingawa DARUSO iliomba bungeni sh 560,000 tu.
“Ni vigumu DARUSO kujisafisha kwa hili, kwanza tumedanganywa na kuonekana wajinga, kwa kutuletea ripoti ambayo siyo, inabidi tuwachukulie hatua zinazopaswa, ikiwamo kutangazwa kwenye mbao za matangazo, wafahamike kuwa wao ndio wabadhirifu si sisi,” alisema mmoja wa wabunge wakati akichangia.
Baada ya mjadala, wabunge walikubaliana kwa njia ya kupiga kura kuwa viongozi hao wa DARUSO wapewe siku saba kulipa fedha hizo na wakishindwa, vyeti vyao vizuiliwe, akaunti zao zifungwe, chuo kikuu kiwaandikie ripoti mbaya kwenye vyeti vyao na hatimaye wafikishwe mahakamani.