Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Askofu matatani kwa fedha za mkopo
Askofu matatani kwa fedha za mkopo
By Habari Tanzania | Published  04/1/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Happiness Katabazi


ASKOFU wa kanisa moja la kiroho nchini, na United Bank of Africa (UBA), wameingia katika mgogoro mzito kuhusu deni la sh milioni 100, ambazo askofu huyo alizikopa kutoka katika benki hiyo miaka kadhaa iliyopita.

Suala hilo limeibuka kuwa mgogoro kati ya pande hizo mbili baada ya benki hiyo na askofu huyo kutoelewana kuhusu marejesho ya mkopo huo.

Wakati Askofu anadai kuwa alisharejesha mkopo huo wote, benki hiyo bado inang’ang’ania kuwa askofu huyo hajaresha kiasi chote cha mkopo kama alivyotakiwa katika mkataba.

Askofu huyo aitwaye, Charles Gadi Kahundami, alikopa fedha hizo kutoka benki chini ya mgongo wa kampuni anayoiongoza ijulikanayo kama SACCOSA.

Malumbano baina ya pande hizo mbili yamefika mbali zaidi na katika harakati zao za kutaka kujisafisha, kila mmoja amefungua kesi katika mahakama akitetea msimamo wake.

Kwa upande wake, Askofu Kahundami, amefungua shauri katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akitaka mahakama hiyo itamke kuwa hadaiwi na UBA kwani alishamaliza kulilipa deni hilo kama alivyotakiwa kupitia mkataba walioafikiana na benki.
Hata hivyo, UBA nayo imekimbilia Mahakama Kuu, kitengo cha Ardhi, ikiitaka mahakama imlazimishe askofu huyo na wenzake, walipe deni hilo.

Mahakama hiyo sasa imepanga kuanza kuisikiliza kesi hiyo Mei 8, mwaka huu. Itaanza kwa kusikiliza pingamizi lililowekwa na askofu huyo, kuitaka mahakama itupilie mbali kesi hiyo ya madai namba 196/2006, iliyofunguliwa mahakamani hapo na UBA, dhidi ya Kampuni ya SACCOSA Ltd na wenzake wanne.

Wadaiwa wengine katika kesi hiyo ni Askofu Kahundami, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Joyce Mhimbira, ambaye ni mke wa askofu huyo, Mohamed Mwenda na Victus Chubwa.

Mdaiwa wa pili na wa tatu ni wamiliki wa SACCOSA Ltd na mdaiwa wa nne na watano ni wadhamini wa mkopo uliokopwa na mdaiwa wa kwanza.

Jumatano iliyopita, Jaji Projest Rugazia, ambaye anasikiliza kesi hiyo, alilazimika kuiahirisha baada ya wakili wa askofu huyo, Kampuni ya uwakili ya Ndyanabo Advocates, kuleta barua ya kujitoa kumtetea.

Kwa mujibu wa barua ya wakili huyo, yenye kumbukumbu JC/1157/SAC/3, ameamua kujitoa kumtetea askofu huyo na wenzake kwa sababu wateja wake hawakumpatia maelezo sahihi kuhusu kesi hiyo.

Baada ya kupokewa barua hiyo, Askofu Kahundami aliiomba mahakama impe muda atafute wakili mwingine na Jaji Rugazia alikubaliana na ombi hilo na kumpa mwezi mmoja kutafuta wakili.

Kwa mujibu wa hati ya pingamizi hilo, Askofu Kahundami, anaiomba mahakama hiyo isisikilize kesi hiyo kwa sababu tayari kuna kesi ya madai namba 260 ya mwaka jana, aliyoifungua Septemba 13 mwaka jana, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Anasema katika kesi hiyo, anaiomba mahakama itamke kuwa alishamaliza kulipa deni hilo na kwamba hadaiwi na UBA. Pia anaitaka mahakama iilazimishe benki hiyo irejeshe hati zake za mashamba na nyumba alizoweka kana rehani wakati anakopa.

Hata hivyo, UBA, inadai mbele ya Mahakama hiyo ya Ardhi kuwa tayari ilishawasilisha pingamizi katika Mahakama ya Kisutu, la kutaka kufutwa kwa kesi hiyo, kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kuendesha kesi za migogoro ya ardhi, au migogoro ya kibiashara.

Wakati kesi hiyo iliposikilizwa kwa mara ya mwisho katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Hakimu Esther Mbaga, alisema atatoa uamuzi wa pingamizi hilo lililowasilishwa na UBA Aprili 25, mwaka huu na kuzitaka pande zote ziwasilishe hoja zao kwa maandishi.

Hata hivyo, UBA, inayotetewa na Henry Chaula, tayari imewasilisha hoja zake kama ilivyoagizwa lakini mawakili wa askofu huyo waliwasilisha barua ya kujitoa katika kesi hiyo nayo.

Benki hiyo ilifungua kesi katika Mahakama ya Ardhi dhidi ya askofu huyo na wenzake wakidai kuwa hawajalipa deni la sh milioni 100, ambazo walikopa mwaka 2004, kwa ajili ya kufanyia biashara. Mkopo huo ulitakiwa kurejeshwa katika kipindi cha miezi 12.

Kwa mujibu wa hati ya madai, wadaiwa walifanya marejesho kidogo kidogo lakini wakashindwa kumalizia kurejesha fedha zote Februari 2005, kama walivyotakiwa.

Ilipofika muda huo, wadaiwa waliomba kuongezewa muda wa kulipa na waliongezewa hadi mwezi Desemba mwaka huo na wakalipa fedha kidogo.

“Ilipofika Februari 23, 2006, deni ambalo halijalipwa na wadaiwa lilikuwa ni sh 58,698,115.88, tena wadaiwa wakaomba waongezewe muda hadi Mei 2006, wakapewa lakini wakashindwa kumaliza kulipa,” inasomeka sehemu ya hati hiyo.

Hati hiyo inaonyesha kuwa wakopaji hao waliweka rehani nyumba iliyopo kiwanja namba 731 kitalu A, iliyopo Kijitonyama na mashamba mawili yaliyopo Pongwe Kiona, wilayani Bagamayo, kama dhamana ya mkopo huo.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.