KITENDO cha serikali kushindwa kutekeleza mapendekezo ya kitaalamu ya mabadiliko ya sheria yaliyotolewa miaka 10 iliyopita, ndicho chanzo cha kuibuka kwa matatizo kama yale ya mgomo wa mahabusu na kukithiri kwa msongamano wa wafungwa magerezani.
Mapendekezo hayo yalitolewa baada ya aliyekuwa Waziri wa Sheria, Samuel Sitta, ambaye sasa ni Spika wa Bunge, kuizindua rasmi timu maalumu ya wataalamu waliobobea katika masuala ya sheria Juni 8, mwaka 1993 (Task Force).
Ingawa hadi hivi sasa serikali haijafanya lolote kuhusu mapendekezo hayo, kumbukumbu zinaonyesha kwamba, Aprili mwaka 1997, ripoti ya timu hiyo, iliyoongozwa na Jaji Mark Bomani ilitajwa kuwa moja ya kazi bora kabisa za kisheria wakati wa semina maalumu iliyoandaliwa na Benki ya Dunia na kufanyika Washington, Marekani.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Jaji Bomani alisema ingawa ni kweli kwamba matatizo ya fedha yalichangia katika kukwamisha utekelezaji wa haraka wa mapendekezo hayo, bado hakukuwa na dhamira ya kutosha kutoka serikalini.
“Nchi nyingi, hasa za Jumuiya ya Madola, zimejifunza mengi kutoka katika mapendekezo ya timu ile. Tulikuwa na ripoti hii ya timu maalumu iliyosifiwa sana, lakini kasi ndogo ya serikali kutekeleza mapendekezo yake inakatisha tamaa sana,” alisema Jaji Bomani mbele ya Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Mary Nagu.
“Kwa mujibu wa ratiba ya utekelezaji tuliyoipendekeza, mambo mengi yalitakiwa yawe yametekelezwa katika kipindi cha miaka 10, hivyo yangekamilika mwishoni mwa mwaka huu. Inasikitisha kuona kuwa kazi ya utekelezaji ndiyo kwanza inaanza kushika kasi sasa,” alisema Jaji Bomani.
Miongoni mwa wajumbe waliokuwa wakiunda timu hiyo ya kitaalamu ni pamoja na Barnabas Samatta, ambaye sasa ndiye Jaji Mkuu, Spika mstaafu, Pius Msekwa, Jaji Raymond Mwaikasu, Felix Mrema, ambaye ni Mbunge wa Arusha Mjini, marehemu wakili Eliuther Kapinga na Profesa J. Kanywanyi.
Akitoa mfano, Jaji Bomani, alisema iwapo mapendekezo hayo yangefanyiwa kazi matatizo yanayojitokeza leo kama mgomo wa mahabusu wa majuzi pamoja na msongamano wa magereza, yangeepukika.
Timu hiyo ilitoa mapendekezo zaidi ya 100 ambayo utekelezaji wake (wakati huo) ulikadiriwa kugharimu zaidi ya dola za Marekani milioni 200, ambazo asilimia 75 kati yake zingetolewa na wahisani.
Moja kati ya udhaifu ambao ungekuwa umeondolewa katika sekta ya sheria nchini kupitia mapendekezo hayo ni ucheleweshwaji wa utoaji haki kupitia mahakama.
Jaji Bomani alisema kuwa kuna kesi ambazo zinachukua zaidi ya miaka 10 kusikilizwa na ucheleweshwaji wa namna hiyo unaufanya msemo maarufu wa haki iliyoicheleweshwa ni haki iliyonyimwa kuonekana una maana.
Alisema pia kuwa miundombinu mibovu katika taasisi zinazoshughulikia haki, kama mahakama, ni sababu nyingine inayoufanya mfumo wa utoaji haki uonekane kana kwamba haufai.
“Ukienda pale Mahakama Kuu majira ya saa tatu asubuhi katika siku yoyote ya kazi, utashikwa na butwaa kuona kundi kubwa la mawakili na mashahidi wakibanana katika veranda finyu ambazo hazina hewa ya kutosha. Eneo (la Mahakama Kuu) limegeuka kama soko!” alisema.
Alisema majaji bado wanachukua notisi za mwenendo wa kesi kwa mkono, jambo ambalo pamoja na kuchelewesha kesi, linatoa mwanya kwa majaji kushindwa kuchukua notisi hizo kwa ukamilifu, kwa makusudi au vinginevyo.
Jaji Bomani aliyasema hayo katika semina ya wahariri wa vyombo vya habari, iliyoandaliwa na Wizara ya Katiba na Sheria, kuhusu programu ya mabadiliko katika sekta ya sheria nchini.
Katika hotuba yake, Waziri Nagu alisema kuwa ili mabadiliko hayo yafanye kazi ipasavyo, ni muhimu wananchi wakawa na uelewa wa sheria na taratibu mbalimbali zilizo chini yake.
“Lengo hasa la programu hii ni kuhakikisha kuwa kila mtu, hasa wale wenye uwezo mdogo, wanapata haki yao pale wanapoihitaji,” alisema Dk. Nagu na kuongeza kuwa, ndiyo maana programu hiyo inagusa taasisi zote za serikali na zisizo za kiserikali zinazojihusisha na masuala ya sheria, haki, ulinzi na usalama wa raia pamoja na utawala bora.
Hata hivyo, Dk. Nagu alisema katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, serikali imetekeleza baadhi ya mapendekezo ya timu iliyoongozwa na Jaji Bomani na kutaja kuundwa kwa mfumo mbadala wa kusuluhisha mashauri, kuwa moja ya mapendekezo yaliyotekelezwa.
Katika mwaka huu wa fedha, serikali imepanga kutumia sh bilioni 11.89, kati ya hizo, serikali itatoa sh milioni 466 tu, huku sehemu kubwa ikitarajiwa kutolewa na wafadhili ambao hadi sasa bado hawajafanya hivyo.
Mmoja wa maofisa wa mpango huo, Juvenalis Motete, alisema kuwa wafadhili bado hawajaingiza fedha kwa ajili ya utekelezaji wa programu hiyo na huenda wakafanya hivyo katikati ya mwezi ujao.
Hata hivyo, mhadhiri mwandamizi kutoka Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Sifuni Mchome, alisema kuwa itachukua muda mrefu, na kazi kubwa kuibadilisha sekta ya sheria nchini.
Alisema sekta hiyo bado inatumia misingi iliyowekwa miaka mingi iliyopita. Akitoa mfano, alisema kuwa suala la msaada wa kisheria, ambalo limeanishwa katika mabadiliko yaliyopangwa, bado linatekelezwa kwa kutumia misingi iliyokuwa imeandikwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1967.
“Pia tuna utitiri wa sheria, ambazo zingine zinapingana, ni changamoto kubwa inayoikabili programu hiyo,” alisema.