MKUTANO wa viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), umeanza jana chini ya Uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete.
Miongoni mwa mambo yanayotarajiwa kuchukua nafasi kubwa kujadiliwa katika mkutano huo, ni migogoro ya kisiasa nchini Zimbabwe na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Macho na masikio ya Waafrika wengi yako jijini Dar es Salaam ambako mkutano huo unafanyika, na kikubwa wanachofuatilia ni nini viongozi wa jumuiya hiyo watamuambia au kumshauri Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, ambaye pia anahudhuria mkutano huo.
Wengi wanataka kusikia viongozi hawa watasema nini kuhusu Zimbabwe na Mugabe, kutokana na matukio ya hivi karibuni ambayo yamevuka mipaka ya kawaida ya ushindani wa kisiasa na hata ubinadamu, yaliyofanywa na vyombo vya dola vya serikali ya Mugabe dhidi ya viongozi wa vyama vya upinzani, wanaharakati na viongozi kadhaa wa dini.
Ni jambo lililo dhahiri kuwa viongozi wa jumuiya hii wanamkumbatia Mugabe, wanayafumbia macho maovu anayofanya dhidi ya wananchi wake kwa kisingizio cha kupambana na maadui wake wa kisiasa, ambao pia ni Wazimbabwe kama yeye.
Sababu kubwa ya kumkumbatia Mugabe ni ile ile, ya huyu ni mwenzetu, tumetoka naye mbali.
Lakini cha ajabu katika hilo ni kwamba, viongozi hawa wanasahau kuwa hata hao Wazimbabwe walio katika mateso makali kutoka utawala wa Mugabe, nao ni wenzao, walipigania uhuru pamoja, na kwamba Mugabe peke yake, bila kuwapo hao anaowatesa, asingefanikiwa kutimiza ndoto aliyokuwa nayo ya kuung’oa utawala wa kikoloni na kuwa kiongozi wa kwanza wa taifa hilo.
Lakini la kusikitisha zaidi kwa viongozi wa jumuiya hii, Tanzania ikiwa kinara wao, ni pale wanaposhindwa kumwambia ukweli Mugabe, kuwa damu ya wananchi wake wakakti wa kudai uhuru, haikumwangika kwa ajili ya kutafuta mateso anayowapa sasa.
Viongozi wengi wanaounda jumuiya hii nchi zao zimetawaliwa na watu weupe na zimepata uhuru kwa njia ya mtutu wa bunduki, tunajiuliza, hivi hawa wamesahau mateso waliyokuwa wakiyapata msituni wakati wa kudai uhuru?
Tunashangazwa na ukimya wa viongozi hawa dhidi ya vitendo vya Mugabe, ambao unaweza kutafsiriwa kuwa anayofanya Mugabe dhidi ya wana wa Afrika wazaliwa wa Zimbabwe, kwao viongozi hawa, kwa sababu Mugabe ni Mwafrika, ni sahihi.
Hii ina maana kuwa, ni Wazungu tu wanaopaswa kulaaniwa wanapofanya vitendo vinavyokiuka haki za binadamu, lakini kwa Waafrika ni sahihi?
Sisi tunadhani muda wa kumwambia ukweli Rais Mugabe umefika, ili kuepusha aibu inayoweza kuwakuta viongozi wa jumuiya yetu hii wanaoendelea kumkumbatia. Hatutaki Mugabe ang’olewa kwa aibu madarakani na wananchi wake ambao tunaamini wamechoshwa na mateso anayowapa.
Tunatambua kuwa Mugabe na Chama chake cha ZANU - PF ni maswahiba wakubwa wa viongozi walioko madarakani pamoja na vyama wanavyo viongoza.
Lakini pamoja na uswahiba huo, litakuwa jambo la busara walau, wakiyakataa matendo yake, lakini wakaendelea kumpenda, vinginevyo watambue kuwa tafsiri iliyopo sasa ni kwamba, wapigania uhuru wa Afrika waliomwaga damu yao nchini Zimbabwe, waliimwanga ili Mugabe aingie madarakani na kumwaga damu ya Wazimbabwe wenzake.
Chonde chonde, tunawasihi viongozi hawa, wawe wawazi kwa Mugabe kwa ajili ya masilahi ya Wazimbabwe walio wengi ambao sisi sote ni ndugu zetu.