BAADA ya kimya kirefu, majambazi yameibuka tena mjini Zanzibar wakiwa na staili mpya ya kuvaa sare za mafundi wa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), na kufanikiwa kuiba mamilioni ya fedha.
Majambazi hao juzi waliibukia Mtaa wa Bububu, ambako kundi la majambazi wapatao sita, wakiwa na sare hizo, waliingia katika nyumba ya mfanyabiashara Abdalla Seif na kufanikiwa kuiba zaidi ya sh milioni 15.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Bakar Khatib Shaaban, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa polisi wanaendele na uchunguzi, ambapo alisema mtu mmoja tayari amekwisha kamatwa kuhusiana na wizi huo.
Alisema kwamba watu hao walikwenda katika nyumba hiyo kwa madai ya kutaka kutengeneza mita ya umeme iliyopo ndani ya nyumba kwa madai kuwa ina hitilafu za kiufundi.
Watoto waliokuwapo katika nyumba hiyo wakati ‘mafundi’ hao wanafika, Zahara Salum (17) na Amina Khamis, waliwaruhusu watu hao kuingia ndani baada ya kujitambulisha kuwa walikuwa mafundi wa umeme.
Hata hivyo, Kamanda Bakari alisema baada ya watu hao kufanikiwa kuingia ndani walishika shika mita na baadaye kuomba kufunguliwa mlango wa chumbani kwa madai ya kufanya matengenezo zaidi.
Kamanda huyo alisema kwamba baada ya kuingia katika chumba cha mfanyabiashara huyo, walivunja droo dogo la kabati na kuondoka na dola za Marekani 12,000, dola za Hong Kong 300 na Dirham 300 pamoja na vitu vingine vya thamani vilivyokuwa vimehifadhiwa humo.
Alisema baadaye watu hao walitoweka haraka kwa kutumia pikipiki na gari.
Kamanda huyo aliwataka wananchi kuwa makini na kuepuka vitendo vya wizi wa udanganyifu, ili kujiepusha na matukio kama hayo.
Vitendo vya ujambazi uliohusisha matumizi ya silaha viliibuka kwa kasi mwishoni mwa mwaka jana na kusababisha raia mmoja wa China na Ofisa Usalama wa Taifa, Mohammed Chande, kupoteza maisha.
Watu hao walipigwa risasi katika matukio ya Darajani Mjini Unguja na huko Mazizini karibu na Ubalozi mdogo wa China. Katika matukio hayo, mamilioni ya shilingi yaliporwa.