Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Hofu serikalini
Hofu serikalini
By Habari Tanzania | Published  03/29/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:
na Happiness Katabazi


SERIKALI ya Awamu ya Nne imeingia katika mtego mkubwa wa hatari ya kukumbwa na matumizi makubwa ya fedha, hali ambayo sasa imesababisha nakisi katika bajeti ya serikali kuongezeka.

Mwenendo huo wa mambo umebainishwa katika taarifa mbili tofauti za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinazoishia Septemba 2006 na Desemba mwaka huo huo.

Ripoti ya miezi mitatu ya BoT iliyoishia Septemba mwaka jana ilikuwa ikionyesha kuwapo kwa nakisi ya sh bilioni 341.1 katika bajeti, kiwango ambacho kilikuwa kimepungua kutoka nakisi ya sh 394.3 ya katika kipindi kilichokuwa kikimalizikia Juni mwaka 2006.

Aidha, ripoti nyingine ya BoT ya mwenendo wa kiuchumi iliyokuwa ikiishia Desemba mwaka jana, kipindi cha miezi mitatu tu baada ya ile ya awali ilikuwa ikionyesha kuwa, nakisi katika bajeti (ukiondoa misaada ya wahisani) iliongezeka hadi kufikia sh bilioni 367.9 kutoka kiwango cha sh bilioni 341.1 cha mwezi Septemba.

Aidha, wasiwasi kuhusu mwenendo wa mambo ulibainishwa jana wakati Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, alipokutana na wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Uchumi na Fedha.

Habari ambazo Tanzania Daima imezipata kutoka miongoni mwa wajumbe wa kamati hiyo zinaeleza kuwa, Waziri Meghji alilazimika kuwatoa wasiwasi huo wabunge baada ya mmoja wao kutaka kujua iwapo ni kweli, serikali ilikuwa ikikabiliwa na tatizo la nakisi katika bajeti yake iliyochangiwa kwa kiwango kikubwa na matumizi makubwa ya viongozi.

Taarifa ambazo baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo walizipata kabla ya Waziri Meghji kukutana nao zilikuwa zikieleza kuwa matumizi yanayoweza kuzuilika ya serikali katika kipindi cha nusu ya kwanza cha mwaka 2006/7 yalikuwa yameongezeka kwa asilimia 25.

“Yaani hata sisi wenyewe tunashindwa kuelewa matumizi haya yametokana na nini… ongezeko hili la asilimia 25 ni kubwa sana kwakuwa limevuka hata malengo la MKUKUTA, na hii ni hatari kwa uchumi wa nchi,” alisema mbunge mmoja aliyezungumza na gazeti hili kwa sharti la kutoandikwa jina gazetini.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, ongezeko hilo ni kubwa zaidi kuliko kiwango cha asilimia sita kilichoainishwa chini ya Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupambana na Umaskini (MKUKUTA).

Taarifa nyingine walizokuwa nazo wabunge hao zilikuwa zikieleza kuwa matatizo kadhaa yaliyotokea katika kipindi cha zaidi ya miezi tisa iliyopita yakiwamo, uhaba mkubwa wa nishati ya umeme, kubomoka kwa miundombinu kama barabara na madaraja katika maeneo mbalimbali nchini na kuzuka kwa ugonjwa wa homa ya bonde la ufa kwa kiwango kikubwa yamesababisha serikali ilazimike kupangua bajeti yake.

Habari ambazo baadaye zilithibitishwa kwa simu na Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, zinaonyesha kuwa uamuzi huo wa serikali ambao umefanywa ndani ya bajeti ile ile umechukuliwa kwa lengo la kuziba mapengo yaliyojitokeza.

“Ninachoweza kukuambia kwa uhakika kabisa ni kuwa, hatuna tatizo kabisa la deficit katika bajeti yetu (nakisi ya bajeti) isipokuwa kilichofanyika ni kuchukua fedha zilezile zilizo ndani ya bajeti na kuzipangia matumizi mengine.

“Nimekuwa serikalini kwa zaidi ya miaka 10 sasa. Suala hilo la re-allocation (upanguaji na bajeti) ni la kawaida kabisa na sisi tumelifanya kutokana na kuwapo kwa matukio kama yale ya uhaba mkubwa wa umeme, uharibifu mkubwa wa miundombinu na kuzuka kwa ugonjwa wa RVF mambo ambayo yamesababisha kuibuka kwa mambo ambayo hayakutarajiwa,” alisema Meghji alipoulizwa iwapo ni kweli kumekuwa na nakisi katika bajeti ya serikali.

Habari nyingine ambazo Tanzania Daima imezipata zinaeleza kuwa, upanguaji huo wa mafungu ya fedha yameikumba Ofisi ya Bunge ambako kiasi cha sh bilioni 5.3 ya fedha ilizotengewa zimepelekwa katika maeneo mengine, ili kuziba mapengo yaliyojitokeza.

Taarifa nyingine ambazo Waziri Meghji alizikataa ni zile ambazo baadhi ya wabunge walikuwa nazo ambazo zilikuwa zikionyesha kuwa serikali inakabiliwa na nakisi inayofikia sh bilioni 650 katika bajeti yake.

Kwa upande wake, Meghji alisema jambo kama hilo haliwezi kamwe kutokea kwa sasa kwani, Mamlaka ya Mapato (TRA) imefanikiwa kuongeza makusanyo yake ya mwezi kwa asilimia 8.4 kutoka wastani wa sh bilioni 160 kwa mwezi hadi kufikia sh bilioni 200 katika kipindi cha miezi sita tu iliyopita.

Hata hivyo, mbunge mwingine aliyezungumza kwa simu na gazeti hili alisema kwamba, moja ya sababu ya kuibuka kwa nakisi katika bajeti ni agizo la Rais Jakaya Kikwete la kuamua kukijenga chuo kikuu kingine mjini Dodoma.

“Hilo nalo unalolizungumzia linagusa maendeleo ya elimu nchini ambayo Rais amekuwa akiyapigania tangu aingie madarakani na kama kuna kitu kama hicho, bado hakuna jambo baya kwani matumizi yako katika maeneo mengi na yote yamefanywa ndani ya bajeti ile ile,” alisema Waziri Meghji alipoulizwa na gazeti hili kuhusu ukweli wa madai kwamba agizo la Kikwete ni sababu moja ya kuibuka kwa nakisi hiyo.

Mbunge mwingine aliyezungumza na gzeti hili alisema agizo hilo la Rais limeleta matatizo makubwa kwani halikuzingatia mahitaji ya kibajeti.

"Ndugu mwandishi, hili agizo la rais halikuletwa kwa mfumo wa bajeti na alilitoa wakati bajeti imeishapitishwa na bunge ..hivyo ni wazi kwamba chuo hicho kitajengwa kwa fedha za serikali ambazo ni dhahiri kabisa utaitikisa bajeti,” alisema


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.