Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Utata ujambazi wa Mbeya uwe fundisho kwetu sote
Utata ujambazi wa Mbeya uwe fundisho kwetu sote
By Habari Tanzania | Published  03/28/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated

LIMETOKEA tukio lenye utata linalohusisha matukio mawili ya ujambazi yaliyotokea mkoani Mbeya katika maeneo mawili tofauti, hivi karibuni.

Kubwa katika matukio hayo, ni lile lililotokea Mbeya Mjini mwishoni mwa wiki na kusababisha kifo cha askari polisi mmoja katika uwanja wa mapambano.

Tukio hilo lilifuatiwa na kukamatwa kwa watu wanne ambao awali walitajwa kuwa ndio waliokuwa wakihusishwa kuwa majambazi waliovamia duka moja maarufu la Ndiyo Mini Supermarket lililoko katika barabara iendayo Zambia.

Siku moja baada ya kukamatwa kwa watu hao ambao ni wafanyabiashara wa nyama katika mji wa Tukuyu, ndugu na jamaa zao waliandamana hadi katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Mbeya wakipinga kuhusishwa kwao na tukio la ujambazi lililotokea katika duka hilo.

Ukiyasikiliza maelezo ya ndugu na jamaa hao wa watuhumiwa, unaweza ukashikwa na mshawasha wa kukubaliana nao mara moja kuwa wao si sehemu ya majambazi waliotoroka mapigano ya polisi muda mfupi baada ya kupora katika duka hilo.

Aidha, ukiyasikiliza maelezo yaliyotolewa siki ya tukio la ujambazi na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Selemani Kova kuhusu tukio la uporaji katika duka la Ndiyo, unaweza ukajikuta ukipatwa na hisia ya kuwaunganisha watu hao na tukio hilo la uporaji.

Kwa sababu tayari utata umeshatokea ambao unapaswa kupatiwa ufumbuzi wa haraka na kwa kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Said Mwema na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya wameshatoa rai ya kuanza kwa uchunguzi, sisi tunaamini kwamba suala hilo litafanywa kwa haraka na kupatiwa majibu.

Tunasema hivyo tukitambua kwamba, uchunguzi huo, kwanza utasaidia sana kumaliza utata huo na kurejesha imani ambayo wananchi si wale wa Tukuyu pekee bali Watanzania wote wanapaswa kuwa nao kwa Jeshi la Polisi ambalo katika kipindi cha mwaka mmoja tu uliopita, limekumbwa na misukosuko kadhaa.

Lakini pia tunatoa rai ya uchunguzi huo kufanyika haraka ili kuwawezesha watuhumiwa hao kupatiwa haki wanayostahili, mapema iwezekanavyo.

Tunaamini kwamba, iwapo kweli wao si sehemu ya tukio la ujambazi lililofanywa katika duka la Ndiyo, vijana hao mbali ya kuuguza majeraha ya risasi ambayo wanadai waliyapata walipovamiwa na majambazi huko Mbalizi, nje kidogo ya Jiji la Mbeya wanakabiliwa na shinikizo kubwa la kisaikolojia la kuendelea kuwa chini ya ulinzi.

Lakini iwapo pia vijana hao ni kweli walikuwa ni sehemu ya tukio zima la ujambazi katika duka la Ndiyo, basi tunaamini kwa dhati kabisa kwamba, uchunguzi utakaothibitisha hivyo, utamaliza kihoro walichonacho ndugu, jamaa na Watanzania ambao kwa kweli wanalifuatilia kwa karibu tukio hilo.

Mbali ya hayo yote, tunapenda kuiasa serikali na Jeshi la Polisi kuongeza umakini wakati wa utendaji wake wa kazi, ikiwa ni pamoja na kuimarisha nidhamu kwani mambo hayo mawili yatasaidia sana katika kukabiliana na ujambazi kwa umakini na katika hali itakayoondoa uwezekano wa kuwapo kwa utata kama ule wa Mbeya.

Aidha, tunaamini pia kwamba, tukio hilo la Mbeya litakuwa ni changamoto muhimu kwa polisi, hasa wakati huu jeshi hilo likiwa na maelekezo ya Amiri Jeshi Mkuu ambaye hivi karibuni wakati akiwa Arusha alikaririwa akisema kuwa serikali ilikuwa ikipanga kuchukua hatua mbaya zaidi ambazo hakuzitaja dhidi ya majambazi.

Tunaandika hivyo huku tukijua kuwa, iwapo polisi wa Mbeya wangeingia katika mtego wa kuchukua hatua mbaya dhidi ya vijana hao wa Tukuyu, ambao uhusika wao katika ujambazi una shaka, basi huenda polisi wangekuwa wameingia katika lawama mbaya zaidi.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.