KWA mara nyingine, wafadhili wameonyesha dhahiri dhamira yao ya kupambana na ufisadi, baada ya kutoa masharti matano wanayotaka yawepo katika sheria mpya ya kupambana na rushwa.
Masharti hayo, yalitolewa kama mapendekezo na Balozi wa Denmark nchini, Bjarne Soreusen, katika kikao cha Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, kilichoanza kujadili Muswada wa Sheria ya Kuzuia Rushwa wa mwaka 2007 jana.
Balozi Soreusen alisema ili kupambana na rushwa kikamilifu, kunatakiwa kuwepo kifungu katika muswada au sheria hiyo, kitakachohakikisha kinatoa uwezo kwa taasisi kusimamia sheria kikamilifu na kuviwezesha vyombo husika kufanya kazi kikamilifu bila kuingiliwa.
Alisema wadau wa maendeleo wamependekeza kuwe na uwazi katika uteuzi wa maofisa waandamizi wa chombo cha kuzuia na kupambana na rushwa, walichokiita kwa kifupi PCCB.
Wanataka pia chombo hicho cha kupambana na rushwa kianzishwe kama chombo cha kikatiba sawa na vyombo vingine kama vile Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Sekretariati ya Maadili.
Alisema hilo liendane sambamba na kuwekewa ulinzi kwa mkurugenzi mkuu wa maofisa waandamizi katika kipindi chote wawapo madarakani.
Mapendekezo mengine ni pamoja na kutambua umuhimu wa jukumu, si tu la PCCB, bali pia wadau wengine katika mfumo wa Mahakama, kama vile waendesha mashitaka wa serikali na majaji, katika kupambana na rushwa.
Pia, wadau hao wamependekeza mtiririko mzuri wa madaraka ya wakurugenzi wakuu wa mashitaka, katika masuala ya kushughulikia makosa yanayotokana na rushwa, kama vile kutoa sababu za uamuzi wake wa kufungua mashitaka.
Mapendekezo mengine ni pamoja na kuwapo kwa utaratibu wa kupeleka ripoti zote za mwaka kwa rais na bungeni.
Kwa mujibu wa Balozi Soreusen, wadau hao wamependekeza bodi ya PCCB ambayo ni madhubuti, na lazima ishirikishe wadau wengi zaidi kutoka sekta binafsi, ikiwa ni pamoja na vyombo vya habari, taasisi na mashirika ya kidini na wabunge, pia ushirikishwaji wa wadau hao katika mchakato mzima wa maamuzi ambao utaleta usawa ndani na nje ya serikali.
Wadau hao wa maendeleo wanataka pia sheria hiyo ieleze kinagaubaga jinsi habari kuhusu rushwa zitakavyosambazwa miongoni mwa wadau na pia kuwepo kwa vyombo kisheria, vitakavyoangalia utendaji wa taasisi itakayokuwa na jukumu la kuongoza mapambano dhidi ya rushwa.
Walitaka pia kuwe na uwazi katika masuala ya bajeti ya PCCB.
Hata hivyo, wadau hao waliipongeza serikali kwa hatua iliyofikia ya kuandika muswada huo kwa lugha ya Kiswahili ili kuwawezesha Watanzania wengi zaidi kuelewa.
Akizungumza baadaye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Philip Marmo, alisema kuwa muswada huo wa kuzuia rushwa, unafuatiliwa kwa makini na watu mbalimbli ndani na nje ya nchi.
Alisema muswada huo ni muhimu katika harakati za kujiletea maendeleo ambayo yanakwenda sambamba na mikakati kama MKUKUTA, MDGs na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025.
Marmo alisema kuwaTanzania ambayo inasifiwa kwa utawala bora ni nchi ya kwanza barani Afrika kuandaa muswada kama huo ambao kwa mara ya kwanza ulianza kujadiliwa Desemba 13, 2006.
Alisema kwa upande wa nje ya nchi muswada huo unafuatiliwa kwa karibu kwa sababu wahisani wanataka kuhakikisha matumizi ya fedha za misaada inayotolewa.
Kwa mujibu wa Marmo, karibu asilimia 75 ya muswada huo ni masharti ya mikataba ya kimataifa, ambapo asilimia 25 ni ya kitaifa.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Leadership Forum, Hebron Mwakagenda, alisema chombo kitakachopewa jukumu la kuongoza mapambano hayo kitakuwa na nguvu iwapo adhabu kutokana na makosa ya rushwa zitarekebishwa.
“Adhabu irekebishwe… mla rushwa mkubwa aliyekamatwa, kulipa laki tano ni ndogo, ni sawa na kumwambia aendelee kula rushwa, kwani ana uwezo wa kulipa na akaendelea kula rushwa, tungekopa kutoka kwenye sheria ya ‘Money Laundering’, ambapo mtu akishikwa na kosa, faini ni milioni kumi na kifungo miaka 10 jela,” alisema.