SAKATA la ujambazi uliolitikisa Jiji la Mbeya na kuamsha hisia tofauti, limechukua sura mpya, baada ya mamlaka mbalimbali kuamuru upelelezi wa kina ufanyike ili kubaini ukweli wa mambo.
Wakati Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile, ameagiza kufanyika uchunguzi kuhusu tukio hilo, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema, tayari ameshatuma makachero wanne, kwenda jijini humo kusaidiana na wenzao wa Mbeya katika kutafuta ukweli kuhusu tukio hilo.
Mwakipesile alitoa agizo hilo baada ya uchunguzi wa awali kuwahusisha vijana kadhaa kutoka wilayani Rungwe, ambao walikamatwa lakini jamaa zao wakaandamana wakipinga kuhusishwa kwao na tukio la ujambazi lililosababisha kifo cha askari mmoja.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari ambao ulihudhuriwa pia na Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Suleiman Kova, Mwakipesile alisema kuwa amelazimika kutoa agizo hilo kufuatia utata uliojitokeza baada ya kukamatwa kwa wafanyabiashara watatu wa nyama kutoka Tukuyu wilayani Rungwe wakihusishwa na tukio hilo la ujambazi.
Tukio hilo lilitokea Ijumaa iliyopita katika duka maarufu jijini Mbeya la Ndiyo Mini Super Market.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa, kukamatwa kwa wafanyabiashara hao na kuhusishwa kwao na ujambazi huo kumezua utata mkubwa.
Hii ni baada ya wafanyabiashara wa nyama wapatao 200 kutoka Tukuyu, ambao juzi waliandamana hadi kwenye ofisi yake, wakipinga kukamatwa kwa wenzao kwa madai kuwa hawahusiki na ujambazi huo.
“Wafanyabiashara hao kutoka Rungwe walifika ofisini kwangu wakiwa saba kwa niaba ya wenzao wengi waliokuwa nje, wakanieleza kuwa wenzao wanaodaiwa kuwa ni majambazi si majambazi, kwani wakati tukio hilo linatokea walikuwa Tukuyu. Nimewasikiliza na kuwataka waniletee ushahidi wa kutosha,” alisema Mwakipesile.
Alisema kuwa kitendo cha kukamatwa kwa watu hao na kuhusishwa na tukio hilo, ni uchunguzi wa awali, utakaolisaidia jeshi hilo liweze kufanya kazi yake vizuri. Alisisitiza kuwa, hatua hiyo haiwahukumu watu hao kuwa walihusika na tukio hilo.
Mwakipesile alisema utata uliojitokeza umelisababisha suala hilo liwe gumu, na kwamba mahakama ndiyo itakayoweza kuthibitisha usahihi wa masuala hayo yote. Aliwataka watu kuwa watulivu wakati suala hilo linashughulikiwa.
Alisema kuwa, watuhumiwa waliokamatwa wamo kwenye mchakato wa kubaini nani kahusika, na kinachotakiwa kufanywa na Jeshi la Polisi ni kuchunguza kwa kina, ili kubaini iwapo kulikuwapo na matukio mawili tofauti, ili isije ikatokea watu wasiokuwa na hatia wakateswa kwa tukio ambalo hawakuhusika.
“Serikali haipendi kuona watu wake wakiteswa bila kosa lolote, kila mtu anajua fika kuwa ujambazi umetokea. Sasa ni vizuri mchunguze ili kuona kama tukio la Mbalizi halitegemeani na lile la Ndiyo Mini Super Market, tusije tukafanya kosa na kuwaumiza watu ambao si wahusika. Hilo lifanyike haraka,” Mwakipesile alimweleza Kamanda Kova.
Uchunguzi wa awali uliofanywa na Tanzania Daima unaonyesha kuwa maelezo ya wafanyabiashara hao yanashabihiana na yale yaliyotolewa na mashuhuda wa tukio jingine, linalodaiwa kufanyika katika mji huo mdogo wa Mbalizi.
Inadaiwa kuwa, wafanyabiashara hao waliokamatwa walishambuliwa na majambazi alfajiri ya Jumamosi iliyopita, wakati wanatoka kwenye nyumba ya kulala wageni ya Mapemba, wakijiandaa kuelekea kwenye mnada wa ng’ombe, Mbuyuni wilayani Chunya.
“Nakuagiza kamanda na watu wako nendeni mkachunguze upya matukio hayo kufuatia taarifa zilizotolewa na vyombo vya habari ambavyo vimefanya kazi kubwa ya kuibua taarifa nyingine zinazoweza kusaidia kupata ukweli kuliko kuendelea kukazania tukio moja, kumbe majambazi waliohusika walikimbia mapema, chunguzeni upya,” aliagiza.
Aidha, Mwakipesile alieleza kwamba hatua ya wafanyabiashara wa mjini Tukuyu kuwatetea wenzao ni ya manufaa zaidi katika mchakato mzima wa tukio hilo la Ujambazi, kutokana na ukweli kwamba taarifa zao zinapanua wigo wa upelelezi wa matukio ya ujambazi mkoani humo.
Mkuu huyo wa mkoa aliwashukuru waandishi wa habari mkoani humo kwa jinsi walivyolishughulikia suala hilo kwa kuingia kwa undani zaidi, na hivyo kuibua mazingira yanayotoa mwanga katika uchunguzi.
Wafanyabiashara hao walioandamana, waliondoka jana jioni kurejea wilayani Rungwe wakisema kuwa wameridhishwa na hatua zilizochukuliwa na mkuu wa mkoa aliyewahakikishai kuwa haki itatendeka.
Kamanda Kova kwa upande wake alimhakikishia mkuu huyo wa mkoa kwamba Jeshi la Polisi lipo tayari kupokea ushahidi wa mtu yeyote kuhusu matukio hayo ya ujambazi ili haki itendeke na kwamba ndiyo maana hawajawapeleka mahakamani watuhumiwa hao.
“Hawa watu wapo polisi kuhojiwa, we are very fair, hatuna sababu ya kumuonea mtu, tutatekeleza maagizo yote tuliyopewa na mkuu wa mkoa… ndiyo maana hatuwanyanyasi na endapo itabainika kuwa si wahusika, tupo tayari kuwaachia na kama ikibainika ni wahusika, mahakama itachukua mkondo wake,” alisema Kamanda Kova.
Uongozi wa waandishi wa habari mkoani Mbeya, ulimweleza mkuu wa mkoa huo kwamba waandishi wa habari wataendelea na msimamo wao ili kuhakikisha kuwa haki inatendeka kwa wote, wakiongozwa na maadili ya kazi zao.
Katika hatua nyingine, IGP Mwema amewatuma maofisa wake kwenda kuchunguza tukio hilo ili ukweli ujulikane.
Akizungumza jana, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Peter Kivuyo, alisema jeshi hilo limetuma maofisa wanne kwenda kupata ukweli kuhusu hali iliyojitokeza mkoani Mbeya.
Alisema hadi sasa watu wanane wanashikiliwa na polisi kuhusu tukio hilo, na makachero hao watawahoji wanaoshikiliwa pamoja na watu wengine ili kubaini wahusika wa tukio hilo.
Kivuyo alisema jeshi hilo halijui uchunguzi huo utakamilika lini, kwa kuwa itategemea uharaka wa kumalizika kwa upelelezi huo na ushirikiano kutoka kwa wananchi.
Jeshi hilo limeingizwa katika mtihani mkubwa baada ya kuibuka kwa malalamiko yanayoonyesha kuwa watu watatu waliohusishwa na tukio la ujambazi wa mwishoni mwa wiki wamekamatwa kimakosa.
Habari zaidi kutoka Iringa zinasema kuwa Polisi mkoani humo wamefanikiwa kumnasa mtu mmoja kuhusiana na tukio hilo la ujambazi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Advocate Nyombi, amesema mtu huyo alikamatwa kufuatia upekuzi uliofanywa katika chumba alichokuwa akiishi marehemu Anjelo Mveyange (25), mmoja wa watu wanaotuhumiwa kuwa majambazi waliofanya uporaji huo, ambaye aliuawa katika tukio hilo.
Marehemu Mveyange alikuwa mfanyakazi wa Kampuni ya Coca Cola mjini hapa.
Pamoja na kufanikisha kukamatwa kwa mtu huyo, Nyombi alisema pia Polisi walifanikiwa kukamata vitu kadhaa ikiwa ni pamoja na silaha zinazoaminika kuwa zilikuwa zikitumika katika matukio ya uhalifu.
Kamanda Nyombi amesema upekuzi huo ulifanyika Machi 25, Kata ya Nyamhanga Ipogoro, Manispaa ya Iringa. Katika upekuzi huo, polisi walikamata risasi 22 za bastola aina ya Revolver, funguo 55 zinazotumika kufungua sehemu mbalimbali, mkanda wa kuwekea bastola na gloves.
Alivitaja vitu vingine vilivyokamatwa kuwa ni kofia zinazotumika katika ujambazi na bangi gramu 0.9.
Alimtaja mtu aliyekamatwa kutokana na upekuzi huo kuwa ni Oscar Mulungu (20), kibarua wa Kampuni hiyo ya Coca Cola, ambaye alikuwa na funguo za chumba hicho.
Kova kwa upande wake, aliwaambia waandishi wa habari kuwa kwa kushirikiana na wenzao wa Iringa, wamemtia mbaroni mtuhumiwa mwingine, Mtenga Kimuli (35).