Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Jarida maarufu la kimataifa lamkosoa JK
Jarida maarufu la kimataifa lamkosoa JK
By Habari Tanzania | Published  03/28/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:
na Mwandishi Wetu


JARIDA maarufu na linaloheshimika duniani, The Economist, limefanya tathmini ya uongozi wa mwaka mmoja wa serikali ya Rais Jakaya Kikwete na kuuelezea kuwa uliopoteza matumaini makubwa yaliyojengwa wakati wa kampeni.

Kwa mujibu wa jarida hilo, matumaini makubwa ya kutokea kwa mabadiliko mema yaliyojengwa kwa watu wakati wa kampeni zenye ushawishi mkubwa zilizokuwa zikiongozwa na Kikwete mwenyewe, yameendelea kuporomoka kadiri muda unavyokwenda.

The Economist katika toleo lake la Machi 22, mwaka huu ambalo nakala yake inapatikana katika mtandao wa intaneti, linaeleza kuwa, kukosekana kwa mabadiliko yoyote katika kipindi hicho hatimaye kumesababisha Serikali ya Awamu ya Nne iendelee kujenga taswira ile ile ya kukatisha tamaa ya zama za serikali iliyopita iliyokuwa ikiongozwa na Benjamin Mkapa.

“Zaidi ya mwaka mmoja uliopita, Jakaya Kikwete aliukwaa urais kwa kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa urais, baada ya kujipatia zaidi ya asilimia 80 ya kura zote.

“Watanzania wengi walikuwa na imani kuwa hoja zenye ushawishi mkubwa za wakati wa kampeni zingetekelezwa na kuleta mabadiliko serikalini na utawala mpya ungekuwa na uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko makubwa yaliyokuwa yakisubiriwa kwa hamu.

“Bahati mbaya, ukweli huo umekuwa tofauti, huku serikali ikikumbwa na tuhuma za rushwa pamoja na kukwama kufanikisha kutatua kile kilichokuwa kikionekana kuwa tatizo sugu lisilokwisha la umeme,” linaandika The Economist.

Pamoja na kusema kwamba hakuna mabadiliko yoyote katika kipindi hicho, jarida hilo linakiri kwamba, matatizo kama yale ya umeme na rushwa inayoendelea kubakia pale pale, yalikuwapo hapa nchini muda mrefu kabla Kikwete mwenyewe hajaingia madarakani.

Pasipo kutaja chanzo chake cha habari, gazeti hilo, limemkariri Kikwete akitaka mafanikio ya utendaji wa serikali yake kuanza kufanyiwa tathmini baada ya kutimiza muhula wake wa miaka mitano serikalini na si kwa kukiangalia kipindi cha miezi 12 tu iliyopita.

Jarida hilo limeandika pia kuwa, kikubwa anachoonekana Kikwete kuanza kukifanya sasa ili kukabiliana na uwezekano wa kuhukumiwa na wananchi ni kuanza kwake kuweka mikakati ya utekelezaji wa mipango ya wizara moja moja.

Kikwete ili kuhakikisha anajipatia alama nzuri, amekuwa akifanya mikakati yake kuhakikisha jambo hilo linafanikiwa. Wakati wa uchaguzi wa mwaka 2005, Chama tawala cha CCM kiliwasilisha ilani yake, ambayo ilifikia hatua ya kubainisha mradi mmoja mmoja ambao ulilengwa kutekelezwa.

“Ili kujaribu kuhakikisha kuwa lengo hili linafikiwa, mawaziri kwa sasa hutakiwa kufanya tathmini kila mwaka ili kuangalia mikakati gani imetekelezwa kwa ajili ya kusaidia kupanga bajeti ya mwaka kwa ajili ya miradi mingine. Lengo la tathmini hiyo linaonekana ni kujaribu kumwezesha rais kupata sehemu ya kujigamba wakati anapolihutubia taifa kuwa amefanikiwa kutekeleza ahadi hii na ile, akionyesha muhtasari wa utekelezaji huo kama ilivyoorodheshwa katika ilani ya CCM,” linaandika jarida hilo la Marekani linalosambazwa katika mataifa mbalimbali duniani.

Pamoja na kuainisha mikakati hiyo, jarida hilo linakosa mwelekeo huo na kuuelezea kuwa ni wa kuwahadaa wananchi na unaokinzana na matatizo ya msingi yanayolikabili taifa.

Kwa mujibu wa The Economist, tatizo la Tanzania haliko katika kukwama kwa miradi iliyoainishwa katika programu za wizara au zilizoainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005, bali ni kuporomoka kwa ari ya kazi ya watu wengi.

“Mikakati ya sasa inayolenga kujipatia sifa au kuhakikisha serikali inachaguliwa tena katika muhula ujao inadumisha fikira za sasa za serikali hii: Jukumu lake limekuwa kusimamia milolongo ya miradi badala ya kuangalia tatizo kuu linalokwamisha maendeleo ambalo ni ukosefu wa ari ambayo ni muhimu katika kuwezesha utatuzi wa matatizo mengi yanayoikabili nchi,” linabainisha jarida hilo.

Kwa mtazamo wa jarida hilo, mafanikio mema kwa Tanzania hayawezi kupatikana kwa kutekelezwa kwa miradi, bali yataletwa na kuwapo kwa mabadiliko ya mfumo wa kiuongozi.

Jarida hilo linatabanaisha pia kwamba, mahusiano ya kikazi kati ya Chama tawala (CCM) kwa upande mmoja na serikali, kunasababisha kuwapo kwa shaka iwapo kweli Ilani ya Uchaguzi ya CCM au Mkakati wa Taifa wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA) vitafanikiwa, kutokana na kutojulikana kipi kati yao kimelengwa zaidi katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo.

Aidha, jarida hilo linaikosoa ilani ya CCM likisema imekaa zaidi kisiasa, ikisisitiza katika miradi pasipo kuwashirikisha wadau wengi zaidi ili kulifikia lengo la taifa lililoainishwa katika MKUKUTA.

Jarida hilo linasema pia kwamba, tatizo jingine linaloonekana kuukabili utawala huo wa Kikwete ni ukweli kwamba katika kipindi chote cha mwaka mmoja, maamuzi yote makubwa yamefanywa na yeye binafsi.

Linaandika pia kwamba, katika majukwaa ya kisiasa, Kikwete na mkewe (Salma) wamekuwa ndio vinara katika majukwaa ya kisiasa kwa kuvutia hadhira, huku Makamu wa Rais (Dk. Ali Mohamed Shein) ambaye anatajwa kuwa mtu ambaye hakuwa chaguo lake (Kikwete), akiwekwa kando.

Aidha, jarida hilo linaendelea kuandika kuwa wakati Shein akitengwa, Waziri Mkuu, Edward Lowassa, yeye anaonekana kuwa ndiye kiongozi mwaminifu zaidi kwa bosi, ingawa amekuwa akionekana kutokuwa na jambo jipya.

Jarida hilo linalielezea tatizo la mgawanyo wa madaraka miongoni mwa viongozi wao watatu wa juu kitaifa, kuwa tatizo linalozikabili nchi nyingine nyingi za Kiafrika mbali ya Tanzania.

Mbali ya hilo, jarida hilo katika hali inayoonekana kuufuatilia kwa karibu mustakabali wa Tanzania, linauelezea wingi wa safari za nje za Kikwete kuwa usio na manufaa makubwa kitaifa hata kufikia hatua ya kusema ametumia muda wake mwingi wa mwaka mmoja madarakani akiwa nje ya nchi.

“Rais Kikwete anadai kuwa safari hizi ni muhimu na za lazima kwa ajili ya kuiweka nchi katika ramani ya kimataifa pamoja na kuvutia wawekezaji wa kigeni. Hata hivyo akiwa nje ya nchi, sehemu kubwa ya serikali inayobakia inaonekana kutoweza kufanya maamuzi makubwa.

“Kila mara rais anaporudi kutoka nje ndipo huonekana kuwapo kwa kasi katika kushughulikia au kuharakisha shughuli fulani, lakini harakati hizo hufifia wakati anapofanya safari nyingine na anaporudi kipaumbele huelekezwa kwenye jambo jingine tofauti,” linaeleza jarida hilo.

Huku likitoa matumaini mema, jarida hilo linaeleza kwamba, kumalizika kwa tatizo la umeme hakuna shaka kwamba hatimaye kutawezesha kiwango cha ukuaji wa uchumi kilichopangwa kufikia kati ya asilimia 6 hadi 7 mwaka huu, na mfumuko wa bei wa chini kwa kadiri iwezekanavyo, ni mambo yatakayowezekana hasa iwapo mvua itanyesha vizuri.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by frank robert)
    Rating
    kweli mimi binafsi nakubaliana kabisa na hili gazeti,kuhusiana na mfumo mzima wa mzee kikwete.nipo cape town hapa south africa
     
Submit Comment


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.