MAHABUSU ambao wiki iliyopita waligoma kwa siku nne kushuka katika magari walipoletwa mahakamani kusikiliza kesi zao, sasa wamekuja na madai mapya kuwa wanatishiwa maisha na askari magereza.
Vitisho hivyo vimedaiwa kuwa ni sehemu ya mkakati wa mamlaka, kutaka kuwafahamu mahabusu walioongoza mgomo huo ulioitikisa serikali.
Taarifa hiyo ilitolewa jana na mahabusu kutoka Gereza la Segerea, ambao hawakutaka kutajwa majina yao.
Wakizungumza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana, walisema kuwa Machi 16, Mkuu wa Jeshi la Magereza, Nicas Banzi, aliwatisha akiwataka waachane na mgomo huo.
“Baada ya kusema maneno hayo, mahabusu wote tuliokuwa hapo tulimwitikia kwa kumpa moyo tu, na kwa kuwa alikuwa anatoa kauli za vitisho… lakini katika akili zetu tulikuwa na mawazo ya kuendeleza mgomo huo kama kawaida,” walidai mahabusu hao.
Walidai kuwa baada ya kutembelewa na mawaziri Machi 21, waliamua kusitisha mgomo huo na kuingia mahakamani, lakini walisema siku mbili zilizofuata, viongozi mbalimbali wa gereza hilo, walikwenda kuwahoji tena na kuwauliza maswali ambayo yalizua mambo mengi kwao.
“Wakuu hao walituita na kutuhoji maswali ya vitisho ya kututaka kuwataja vinara wa mgomo, na jinsi walivyoweza kutayarisha mabango yaliyokuwa na ujumbe, na hata kuweza kutoka nayo gerezani hadi mahakamani na kutuhoji mambo mengi kuhusu kesi zetu,” walidai.
Walisema kuwa walihojiwa hadi usiku wa manane bila kujua nia na madhumuni ya kuhojiwa mfungwa mmoja mmoja.
“Huwa tunashinda mchana kutwa bila shughuli yoyote, tunashangaa kwa nini tuhojiwe usiku wa manane,” alisema mmoja wao.
Hata hivyo, walisema kuwa waliulizwa maswali yale yale ambayo walikuwa wameyaandika kwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa.
Aidha, katika mahojiano hayo, walidai kulazimishwa kuwataja askari ambao walihusika kuwachochea kugoma, pamoja na kuwaandikia mabango, na kuwahoji ni nani ambaye aliwaandikia mabango hayo.
“Walikuwa wanatulazimisha kuwataja walioandika na kutuingizia mabango hayo wakati hata wao wakuu walikuwa wanatuona wakati yanaingia mlangoni na hadi kufika nayo mahakamani bila hata kuhusisha askari magereza yeyote aliyekuwamo ndani,” walidai mahabusu hao.