BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, imefungua akaunti maalumu katika benki ya NMB tawi la Bank House kwa ajili ya kukusanya madeni kutoka wahitimu walionufaika na mikopo hiyo.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo, inaeleza kuwa imefungua akaunti katika benki hiyo ambayo ina matawi katika mikoa na wilaya zote nchini na pia zina mawasiliano ya elekroniki na matawi yaliyopo Dar es Salaam. Taarifa imeitaja akaunti hiyo ni Higher Education Students' Loans Board namba 2011100205.
Mkurugenzi huyo anaeleza kuwa wale wote walionufaika na mikopo ambao wamehitimu masomo katika vyuo vya elimu ya juu kuanzia mwaka 1994, wanatakiwa kuanza kuwasiliana na bodi hiyo, ili kweka utaratibu ukakaowawezesha kuanza kurejesha mikopo yao katika muda usiozidi miaka 10.
“Waajiri wote wanatakiwa kuleta kwenye bodi kuanzia Julai 2006 orodha ya waajiriwa wao waliohitimu elimu ya juu kuanzia mwaka 1994. Orodha hizo zionyeshe jina, mwaka aliohitimu, chuo alichohitimu, cheo chake, mshahara wake kwa mwezi na kiasi anachopenda kukatwa kwa mwezi,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ileleza kuwa mtu yeyote aliyenufaika na mkopo huo, akashindwa kurejesha bila sababu zinazotosheleza, anakuwa ametenda kosa na atachukuliwa hatua za kisheria.
“Suala la kurejesha mikopo si la hiari bali ni amri kwa mujibu wa sheria namba 9 ya mwaka 2004,” iliongeza taarifa hiyo.
Kutokana na hali hiyo, bodi inawaomba waajiri wote, wizara na taasisi za umma na binafsi kuwapa ushirikiano katika mchakato mzima wa urejeshaji wa mikopo ya elimu ya juu.