JESHI la Polisi mkoani hapa, limeingizwa katika mtihani mkubwa baada ya kuibuka kwa malalamiko yanayoonyesha kuwa watu watatu waliohusishwa na tukio la ujambazi wa mwishoni mwa wiki wamekamatwa kimakosa.
Hali hiyo imejitokeza baada ya mamia ya wananchi wanaotokea Tukuyu yaliko makao makuu ya Wilaya ya Rungwe kuandamana hadi katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa, John Mwakipesile wakipinga kukamatwa kwa watu hao watatu ambao polisi inawahusisha katika tukio la ujambazi lililogharimu maisha ya askari polisi, Rajabu Juma Tenga mwishoni mwa wiki.
Kundi hilo la watu wanaozidi 200 wakiwamo wafanyabiashara, liliwasili katika ofisi za Mwakipesile likiwa katika mabasi manne ya kukodi.
Watu hao walioonekana wakiwa na hasira, waliieleza Tanzania Daima kuwa, walilazimika kusafiri hadi Mbeya baada ya kupata taarifa zisizo sahihi zilizokuwa zikiwahusisha jamaa zao na tukio la ujambazi la mwishoni mwa wiki.
Baadhi ya viongozi wa msafara huo, walisema kuwa baada ya kusikia kuwa wenzao walikuwa wamekamatwa kwa tuhuma za ujambazi, wafanyabiashara hao jana waliamua kufunga maduka yote ya kuuzia nyama yapatayo 12 katika soko la Tukuyu mjini na kusafiri hadi Mbeya kujua kulikoni.
Watu hao walisema wataendelea kuyafunga maduka hayo ya nyama hadi hapo watakapofanikiwa kuwatoa hatiani jamaa zao ambao walidai walikamatwa kwa makosa yasiyo yao.
Mmoja wa viongozi wa soko la Tukuyu walilokuwa wakifanyia biashara watuhumiwa hao, Zuhura Salum, alisema kuwa taarifa zilizotolewa na polisi kuhusu kukamatwa kwa watuhumiwa hao, si za kweli kwa madai kuwa, wakati tukio likitokea majira ya saa 12:00 jioni jijini Mbeya, wafanyabiashara hao walikuwa kwenye bucha zao mjini Tukuyu.
Walisema watuhumiwa hao, ni Hamad George, kaka yake Godfrey George aliyepigwa risasi sehemu za kiunoni na miguuni na polisi kwa madai kuwa ni jambazi na mwenzake Sambayete Chacha.
“Tunawafahamu watuhumiwa tangu wakiwa wadogo, hadi wazazi wao walipofariki. Hakuna hata siku moja wamefikishwa polisi kwa tuhuma yoyote ya uhalifu, na kama wangekuwa wahalifu, wasingethubutu kwenda polisi kuomba PF 3… mnaona jinsi mambo yalivyo? Watoto wanaumia bila hatia,” alisema Zuhura.
Mtu mwingine, aliyejitambulisha kuwa ni baba mdogo wa watuhumiwa wawili ambao ni mtu na binamu yake, Ezekiel Nassor, ambaye pia ni mmiliki wa bucha mjini Tukuyu, alipinga kitendo cha vijana hao wawili kuhusishwa kwenye tuhuma za ujambazi wakati wakiwa wafanyabiashara wanaojulikana.
Alisema kuwa siku ya tukio hilo, vijana wake hao waliondoka na pikipiki majira ya saa 1.00 jioni mjini Tukuyu kuelekea Mbalizi, nje kidogo ya Jiji la Mbeya na kufikia kwenye nyumba ya kulala wageni ya Mapemba ambako alfajiri majira ya saa 10.45 walikuwa wakitakiwa kuondoka kwenda kwenye mnada wa kununua ng’ombe katika Kijiji cha Mbuyuni wilayani Chunya.
Alisema vijana wake hao walipokuwa wakitoka nje ya geti la nyumba hiyo ya wageni, ndipo walipovamiwa na majambazi kwa risasi ambazo zilimjeruhi mmojawapo aliyetajwa kwa jina la Godfrey.
Muda mfupi baada ya tukio hilo, mmoja wa vijana hao alikwenda kutoa taarifa Ktuo cha Polisi cha Mbalizi ambako hakumkuta askari yeyote wa zamu.
“Nimekwenda kumuona mtoto hospitali, nimeongea naye na amenieleza kila kitu kuhusu jinsi walivyovamiwa asubuhi hiyo, ndipo walipoamua kukimbilia Hospitali ya Rufaa kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya haraka kutokana na PF 3 waliyopatiwa kituo cha kati polisi, sasa huo ujambazi wameufanya saa ngapi?” alihoji.
Mwingine aliyejitambulisha kuwa ni balozi wa soko la Tukuyu, Adela Goliati alisema kuwa, akiwa kiongozi wa usuluhishi kwenye soko hilo, haijawahi kutokea watuhumiwa hao wakatajwa kwa kosa lolote.
“Hivi wote tumeamua kufunga soko, hatuwezi kuendelea na biashara huku vijana wetu wasiokuwa na hatia wakiwa wamekamatwa bila sababu. Tumeambiwa kuwa majambazi waliohusika na uhalifu huo wametoka mkoani Iringa, sasa hawa vijana wetu waliovamiwa katika tukio jingine, iweje waunganishwe kwenye kosa ambalo si wahusika?” naye alihoji.
Mfanyabiashara mwingine wa nyama sokoni hapo, Hussein Shaba, alisema kuwa, watuhumiwa hao wawili waliondoka kwa pikipiki aina ya BAJA Cc 250 na muda unaotajwa walikuwa safarini kuelekea jijini Mbeya huku wakiwa hawana silaha yoyote na kwamba hawajawahi kununua silaha ya aina yoyote.
“Kama huyu Chacha, japokuwa watu wanasema kuwa ni Mkurya wa Musoma, hakujui kabisa huko, amezaliwa Tukuyu na kulelewa na wajomba zake tangu alipozaliwa… mama yake ambaye ni marehemu, alikuwa akiitwa Magreth Asagwile na Nassoro ni mjomba, amelelewa bila kuwepo kwa tuhuma zozote juu yake.
“Tunaomba polisi wachunguze tukio la majambazi waliovamia duka la Ndiyo kwa makini, wamewakamata watu wengine… inatutia uchungu sana,” alisema Shaba.
Tanzania Daima ilipofuatilia kwa undani, iligundua kuwa, kwa mara ya mwisho, Sambayete alilipia mapato yake TRA na kupewa risiti yenye namba Cs 1863506 ya sh 20,000 ya tarehe 21 Januari mwaka 2007 akiwa na TIN No 02/p1434 ambayo ndiyo anayoitumia katika biashara yake ya kuuza nyama mjini humo.
Kwa upande wa George, uchunguzi unaonyesha kuwa, alianza biashara hiyo Septemba 29 mwaka 2005 kwa kupatiwa leseni yenye namba B 0009881277, na kwamba kwa kipindi hicho chote, watuhumiwa hao wamekuwa wakienda mnadani wilayani Chunya kununua ng’ombe kwa ajili ya kuchinja na kuuza kwenye bucha zao.
Uchunguzi wa Tanzania Daima uliofanywa jana mchana kwenye nyumba ya kulala wageni ya Mapemba inayomilikiwa na mama mjane, Amina Sande au maarufu kama Mama Mapemba, umebaini kuwa naye ametiwa nguvuni kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kuwasaidia polisi.
Kukamatwa kwa mama huyo, kunakwenda sambamba na wafanyakazi wawili wa nyumba hiyo ya kulala wageni waliotajwa kwa jina moja moja la Jackson na Babu, ambaye ni mlinzi.
Mmoja wa wahudumu waliokutwa wakiendelea na kazi kwenye nyumba hiyo hiyo, Anna Mwasomola, alisema kuwa tajiri yake na wafanyakazi wawili walikamatwa na polisi na jana mchana waliwapelekea chakula na hawajui chochote kinachoendelea huko.
Aidha, alikiri kuwa, vijana waliokamatwa walikuwa ni wateja waliokuwa wanafika kwenye nyumba hiyo mara kwa mara na siku zote walikuwa wanafikia kwenye chumba namba 108.
Kuhusu watuhumiwa wa ujambazi waliokamatwa, Mwasomola alisema kuwa, hao ni wateja wao wa siku zote na hufika hapo kwa ajili ya kwenda minadani kununua ng’ombe na huondoka majira ya saa 11.00 alfajiri kwenda Chunya.
Alisema walipofika kwenye nyumba hiyo juzi, walikuwa salama, lakini baadaye alipata taarifa kuwa, mmoja wao alikuwa amepigwa risasi.
Alipofuatwa jana, Mwakipesile ilidaiwa kuwa yupo kwenye kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama cha mkoa huo pamoja na Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Suleiman Kova.
Mpaka saa 11 jioni, viongozi hao bado walikuwa wakiendelea na kikao hicho huku wananchi hao wakiwa wamejikusanya nje wakiwasubiri.
Ajenda ya kikao hicho, ambacho kiliwahusisha pia wakuu wa wilaya zote za Mbeya, hazikuweza kufahamika mara moja.
Watu wawili, wanaodaiwa kuwa walikuwa katika kundi la majambazi wanne, waliuawa juzi baada ya uvamizi katika duka la Ndiyo na wengine wawili wakafanikiwa kutoroka baada ya kumuua kwa kumpiga risasi Tenga.
Katika taarifa aliyoitoa, Kova alidai kuwa watuhumiwa hao walidai kuwa ni wachezaji wa timu ya mpira wa miguu kutoka katika mji mdogo wa Ifunda, mkoani Iringa.