ASKARI Magereza waliokuwa zamu ya kufungia wafungwa katika Gereza la Kanegele, wilayani Bukombe, wanadaiwa kumpiga hadi kufa mfungwa aliyetambuliwa kwa jina la Charles Madoshi (20).
Tukio hilo lilitokea Machi 13, mwaka huu baada ya mfungwa huyo kujaribu kutoroka kwa kuruka uzio wa gereza.
Watu walioshuhudia tukio hilo walieleza kuwa, askari waliokuwa zamu ya kufungua wafungwa siku hiyo, waligundua kutokuwepo kwa mfungwa huyo wakati wakiwahesabu kabla ya kuwafungia katika vyumba vyao.
Baada ya kugundua kutokuwapo kwake, askari hao walimsaka na kufanikiwa kumkamata akiwa angali ndani ya uzio wa gereza, ndipo wakaanza kumwadhibu kwa kumpiga mpaka alipopoteza fahamu, wakampeleka katika zahanati ya Masumbwe.
Habari zaidi zinaeleza kuwa, baada ya askari hao kubaini kuwa hali ya mfungwa huyo inazidi kuwa mbaya, waliamua kumpeleka katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama kwa ajili ya matibabu zaidi.
Mashuhuda hao walieleza kuwa, askari waliohusika kumpiga mfungwa Charles, waliutaarifu uongozi wa gereza kuwa alipigwa na walinzi wa jadi (Sungusungu) ambao walimkamata wakati akijaribu kutoroka baada ya kuruka uzio wa gereza.
Alipoulizwa kwa njia ya simu, Kamanda wa Magereza mkoani Shinyanga, Kamishina Msaidizi wa Magereza, Elika Pesha, alikiri kupokea taarifa za kifo cha mfungwa huyo, lakini hakutoa ufafanuzi zaidi.
Kamanda huyo aliahidi kulifuatilia tukio hilo na kutoa taarifa kwa vyombo vya habari, lakini alipotafutwa baadaye, simu yake ya kiganjani ilikuwa ikiita bila kupokelewa.
Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Kahama, Helen Yesaya alithibitisha kumpokea mfungwa huyo akiwa mahututi kutokana na kipigo kilichosababisha apoteze fahamu.
Yesaya alisema baada ya kumpokea, walijitahidi kumtibu, lakini alifariki alfajiri ya Machi 22 na kwamba kifo chake kilisababishwa na majereha mengi aliyoyapata.