Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Mtanzania aliyelipua ubalozi Dar aomba radhi
Mtanzania aliyelipua ubalozi Dar aomba radhi
By Habari Tanzania | Published  03/25/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Mwandishi Wetu, NEW YORK, Marekani


WIZARA ya Ulinzi ya Marekani, imesema kuwa, mfungwa katika gereza la Guantanamo ambaye ni raia wa Tanzania, Ahmed Khalfani Ghailani ameomba radhi kwa kuhusika kwake katika ulipuaji wa ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam mwaka 1998.

Imeelezwa kwamba, Ghailani amejitetea kwamba, hakujua kuwa kuna mpango wa kulipua ubalozi huo kama Jeshi la Marekani linavyodai.

Kwa mujibu wa maelezo yake, Ghailani aliliambia jopo la maofisa wa kijeshi kuwa, yeye si mfuasi wa al-Qaida na hakujua watu aliokuwa akishirikiana nao wanatoka kundi gani wakati alipowasaidia kusafirisha bidhaa pamoja na kuwasilisha nyaraka alizotumwa.

Alisema kuwa, anaomba radhi kwa Serikali ya Marekani na anasikitika kwa kilichozipata familia ambazo wapendwa wao walipoteza maisha katika ulipuaji wa ubalozi huo.

Ghailani amefunguliwa mashitaka na Mahakama ya Marekani kwa kuhusika kwake katika shambulio hilo lililoua watu 11 na kujeruhi 85.

Hati ya maelezo yake inasema kuwa, wakati wa usikilizaji wa kesi hiyo, Ghailani alikiri kupata mafunzo katika kambi ya al-Qaida nchini Afghanistan, kukutana na viongozi wa kigaidi nchini Tanzania, kutafuta lori na kusafirisha mabomu kwa ajili yao.

Lakini akijitetea, alisema kuwa hakuwa akijua matokeo ya vitendo hivyo na kwamba alichukua mafunzo kama sehemu ya kujipa uwezo wa kujilinda na hakujua mpango wa watu hao kuhusiana na upatikanaji wa lori na mabomu.

Aidha juzi, Pentagon ilitoa maelezo ya mtu mwingine anayetuhumiwa kuwa gaidi raia wa Malaysia, Mohammed Farik bin Amin, ambaye pia hujulikana kama Zubair.

Alituhumiwa kuhusika na kundi la kigaidi la Indonesia lijulikanalo kama Jemaah Islamiya, na kusafirisha dola 50,000 kusaidia mfuko maalumu kwa ajili ya kulipua hoteli ya jijini Jakarta, Marriott Hotel mwaka 2003, ambako watu 12 waliuawa na wengine karibu 150 kujeruhiwa.

Wakati wa usikilizaji wa kesi hiyo, Jeshi la Marekani pia lilimtuhumu kwa kupanga mtu wa kujitoa mhanga katika mashambulizi yaliyokuwa yafanyike nchini Marekani.

Kwa mujibu wa maelezo hayo, Zubair alisema hakutoa maelezo yoyote wakati wa usikilizaji kesi, lakini alijibu ‘ndiyo’ au ‘hapana’ baadhi ya maswali kutoka kwa maofisa wanaoendesha kesi hiyo.

Kesi hizo zinazosikilizwa na mahakama maalumu, zinaendeshwa na maofisa watatu wa kijeshi wa Marekani na zina lengo la kutambua iwapo wafungwa hao wako upande wa adui au la.

Iwapo wako upande wa adui, hupelekwa katika mahakama za kijeshi chini ya sheria mpya iliyoridhiwa na Bunge la Marekani, mwaka jana.

Mamia ya wafungwa wameachiwa kupitia mchakato huu na wengine wanaendelea kutathminiwa, lakini hali hiyo haitarajii kutokea upande wa kina Ghailani, Zubair na wengine 12 wanaotuhumiwa kuwa magaidi waandamizi, ambao walihamishiwa katika gereza la Guantanamo mwaka jana kutoka katika magereza ya siri ya Marekani yaliyoko nchi nyingine.

Mashirika ya haki za binadamu yamekuwa yakitaka wafungwa wa Guantanamo waachiwe au kushitakiwa katika mahakama za kawaida za kiraia au kijeshi. Mkurugenzi wa uhamasishaji wa Shirika la Haki za Binadamu (HRW), Tom Malinowski, anasema kuwa, mchakato unaoendelea Guantanamo, hauwezi kubadili hali halisi za watuhumiwa hawa au mustakabali wa maisha yao ya baadaye.

“Nadhani bado kuna utata kwa sababu hakuna hata mmoja wa watu hawa aliyekabiliwa na mashitaka ya kweli katika mahakama za kiraia au kijeshi. Nadhani hadi siku watakapofikishwa mahakamani na kushitakiwa kwa tuhuma wanazoshitakiwa, bado kutakuwa na utata wa ukweli wa kukiri kwao, kwani upo uwezekano wa kuwa katika shinikizo fulani,” alisema.

Ghailani ambaye alikuwa katika orodha ya watu waliokuwa wakiongoza kusakwa kwa ahadi ya donge nono la mamilioni ya dola kwa yeyote atakayesaidia kukamatwa kwao, alikamatwa mwaka 2004, nchini Pakistan na majeshi ya nchi hiyo katika operesheni iliyoendeshwa kwa ushirikiano na Marekani.

Ghailani anadaiwa kutumia majina mengi tofauti, yakiwamo Ahmad Khalfan Ghilani, Ahmed Khalfan Ahmed, Abubakar K. Ahmed, Abubakary K. Ahmed, Abubakar Ahmed, Abu Bakr Ahmad, A. Ahmed, Ahmed Khalfan, Ahmed Khalfan Ali, Abubakar Khalfan Ahmed, Ahmed Ghailani, Ahmad Al Tanzani, Abu Khabar, Abu Bakr, Abubakary Khalfan Ahmed Ghailani, Mahafudh Abubakar Ahmed Abdallah Hussein, Shariff Omar Mohammed, 'Foopie', 'Fupi', na Ahmed Mtanzania.

Ghailani alizaliwa mwaka 1974 katika Kisiwa cha Zanzibar na anazungumza Kiswahili. Alitumikia kama mhadhiri wa Kiislamu anayesafiri 'tabligh', na inasemekana alikuwa akitembelea Pakistan kwa shughuli hiyo.

Baada ya kujiunga na kundi la al-Qaida, anaelezwa kufuzu utaalamu wa utengenezaji mabomu na alipangiwa kutengeneza bomu jijini Dar es Salaam kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na wenzake katika mpango wa ulipuaji wa ubalozi huo, Mohammed Sadiq Odeh na Khalfan Khamis Mohammed.

Inaelezwa kuwa, alipewa jukumu hilo na kwa kuwa hakuweza kuendesha gari, ilibidi malighafi za utengenezaji mabomu zibebwe na mtu mwingine katika gari badala ya baiskeli yake.

Ghailani alikuwa jijini Nairobi Agosti 6, 1998 ambako anaelezwa alikodi chumba katika Hoteli ya Hiltop na alifanya vikao na wenzake na kuruka kwenda Karachi kwa Shirika la Ndege la Kenya (Kenya Airways) kabla ya bomu kulipuka.

Akiwa Pakistan au Afghanistan, alioana na mwanamke wa Uzbek na kujipatia watoto.

Baada ya kukamatwa nchini Pakistan kufuatia operesheni ya kuwasaka vinara wa ulipuaji wa balozi za Marekani nchini Kenya na Tanzania mwaka 1998, alipelekwa kusikojulikana kabla ya kuhamishiwa gereza hilo lililopo nchini Cuba, ambalo limekuwa likikosolewa mno na jumuiya ya kimataifa, zinazotaka lifungwe.

VOA


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.