Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Majambazi yaua mbele ya RPC
Majambazi yaua mbele ya RPC
By Habari Tanzania | Published  03/25/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Christopher Nyenyembe, Mbeya


MIRINDIMO ya risasi zilizokuwa zikipigwa hovyo na kundi la majambazi wanne waliotokea mkoani Iringa na kuja kufanya uhalifu Jijini Mbeya, juzi, ziliamsha huzuni kubwa baada ya mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Chuo Kikuu cha Mzumbe tawi la Mbeya, Juma Rajabu Tenga (27) kupigwa risasi kichwani na kufa muda mfupi baada ya kufikishwa kwenye Hospitali ya Rufaa Mbeya.

Tenga ambaye pia ni askari wa Jeshi la Polisi nchini, aliyekuwa anasomea Shahada ya Sheria, alikuwa umbali wa meta mbili toka alipokuwa amelala Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Suleiman Kova ambaye alinusurika kifo wakati akiongoza mashambulizi dhidi ya majambazi hayo, huku akimshuhudia mwanafunzi huyo akipigwa risasi mbele yake na kupoteza maisha.

Kwa mujibu wa watu walioshuhudia tukio hilo, lililolitikisa Jiji la Mbeya juzi majira ya saa 12.00 jioni, lililotokea kwenye duka maarufu la Ndiyo Mini Supermarket, jambazi moja liliuawa hapo hapo na jingine muda mfupi lilipopigwa risasi na polisi. Mmiliki wa duka hilo, Simon Kahemele alifanikiwa kuliua jambazi la kwanza lililokuwa limebeba mkoba.

Habari za ndani zinadai kuwa, majambazi hayo yaliyotokea katika mji wa Ifunda mkoani Iringa, yalikuwa yakijifanya kuwa ni wachezaji soka katika timu za Ruaha na Kibwabwa Shooting Club.

Inadaiwa kuwa, uvamizi huo wa aina yake ulifanywa na majambazi hao waliokuwa wakitumia bunduki aina ya SMG na bastola moja ambao walianza kusambaza risasi baada ya kuona mwenzao aliyejulikana kwa jina moja la Voice anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 30 akipigwa risasi na kufa papo hapo.

Kufuatia tukio hilo na milio ya risasi iliyokuwa ikirindima hovyo kutoka kila kona, ndipo mwanafunzi huyo wa Mzumbe ambaye ni askari polisi alipoamua kujitosa na kufanya kazi kubwa ya kuwataka raia walale chini ili kuokoa maisha yao huku akiwa sambamba na kamanda wa jeshi hilo mkoani hapa, Kova.

Tanzania Daima ilipofuatilia Hospitali ya Rufaa majira ya saa nne usiku, ikitokea eneo la tukio kulikokuwa na ulinzi mkali wa polisi waliokuwa doria, huku giza likiwa limetanda, habari zilizopatikana zinadai kuwa, jambazi jingine lililokuwa likijulikana kwa jina la Anjelo Mveyange (25), nalo liliuawa katika majibishano ya risasi na polisi waliofika haraka kwenye tukio hilo.

Mbali ya majambazi hayo mawili kuuawa akiwemo mwanafunzi huyo wa Mzumbe, PC Tenga, raia wawili walijeruhiwa akiwemo mke wa mmiliki wa duka hilo, Irene na mfanyabiashara ndogondogo (mmachinga), Ephraim Gumbo (23) aliyepigwa risasi mguuni kwenye unyayo na kutokea upande wa pili.

Alipohojiwa katika Hospitali ya Rufaa alikokuwa amelazwa kwenye wodi namba moja, Gumbo alisema kuwa akiwa kwenye pilikapilika zake za kufanya biashara akipita katika eneo hilo la tukio kujionea kulikoni, huku watu wakiwa wamejazana, ndipo aliposhtuka kuona kuna kitu kimepenya ghafla mguuni.

“Sikujua chochote ndipo niliposikia kitu kikipita chwaa mguuni, nikatupa bidhaa zangu zote na kuanza kupiga kelele, nilipojiangalia kwenye kiatu nilichovaa, nilikuta tundu lililoanzia upande wa kushoto na kutokea upande wa kulia, askari walipokuja ndipo wakagundua kuwa nimepigwa risasi na kukimbizwa hospitalini,” alisema mmachinga huyo.

Akisimulia tukio hilo, mmiliki wa duka la Ndiyo, Kahemele, alisema majambazi hayo yalifika katika duka lake majira ya saa 12.00 jioni na akiwa nje ya duka hilo upande wa nyuma, alisikia kelele kutoka kwa binamu yake aitwaye Elizabeth, aliyekuwa na mkewe Irene akipiga yowe kuwa walikuwa wameingiliwa na majambazi.

Alisema baada ya kusikia kelele hizo, alipanda juu ghorofani na kuchukua bunduki yake aina ya shotgun na kujibanza kwenye upenu, ambako aliwaona majambazi wanne wakiwa wanatoka kwenye lango kuu la duka hilo huku wakiwa wamepora fedha kiasi cha sh milioni moja zilizokuwa zimewekwa kwenye mkoba na vitu vingine, zikiwemo simu za mkononi.

Kahemele alisema majambazi hayo yakiwa yapo tayari kukimbia, ndipo alipomlenga jambazi aliyekuwa ameshika mkoba na kumpiga risasi kiunoni, baada ya kuanguka, ndipo mlinzi wa duka hilo alipomkamata huku kundi la wananchi wenye hasira walipojitokeza na kuliua jambazi hilo.

Kufuatia tukio hilo, majambazi mengine yalianza kujihami kwa kupiga risasi hovyo zilizosababisha watu wengi waende kukabiliana nao na kwamba mawili yaliyokuwa na bunduki, yalikimbia kuelekea kwenye msitu wa hoteli ya siku nyingi ambayo ni magofu ya Bush trekker, kisha wakatokomea kwenye mashamba ya mahindi.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Kova alipohojiwa jana aliyataja majambazi mawili yaliyouawa katika tukio hilo kuwa ni Voice na Mveyange, ambayo maiti zao zimehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya ukiwamo mwili wa PC Tenga aliyeuawa kwa kupigwa risasi na majambazi hayo.

Kova alisema polisi walifika dakika chache baada ya kupigiwa simu na wakaanza kujibishana risasi na majambazi hayo mawili ambayo alisema pamoja na kukimbia yalikuwa yamejeruhiwa vibaya.

Alisema katika mapambano hayo, polisi walifanikiwa kuinasa bastola moja iliyodondoshwa na majambazi hayo baada ya kuzidiwa nguvu.

“Tukiwa tunapambana na majambazi hayo, tulikuwa sambamba na marehemu Tenga ambaye ni askari polisi mwenye namba F 862, aliyekuwa mwaka wa pili Mzumbe, aliyekuwa meta chache kutoka kwangu akiwataka wananchi waliokuwa katika eneo hilo walale chini, lakini ghafla nilishuhudia akipigwa risasi kichwani,” alisema Kamanda Kova.

Alisema kifo cha askari huyo ni cha kishujaa kwa Jeshi la Polisi na taifa kwa ujumla, kwani hakujali wajibu wake kama mwanafunzi, pale alipoamua kujitosa kuokoa maisha ya wananchi wengi ambao hawakuwa na mbinu zozote za kujikinga wakati risasi zikipigwa hovyo na majambazi hayo.

“Huyu kijana amekufa kishujaa, amefanya kazi kubwa ya kuokoa maisha ya watoto wadogo waliofika kushuhudia tukio hilo, akiwataka walale chini, na aliifanya kazi hiyo akitimiza wajibu wa jeshi kutokana na kiapo alichokula kuwa, yupo tayari kupoteza maisha yake kwa ajili ya kuokoa maisha ya wengi na ndivyo alivyofanya,” alisema Kova.

Alisema mwanafunzi huyo wa Mzumbe aliyekuwa masomoni jijini hapa, akitokea Mwanza kiliko kituo chake cha kazi, atazikwa nyumbani kwake Same mkoani Kilimanjaro kwa heshima zote za Jeshi la Polisi. Tenga alikuwa mpambe wa RPC wa Mwanza, Kamanda Zelothe Stephen.

Kuhusu majambazi yaliyojeruhiwa, Kamanda Kova alisema kuwa, msako mkali unaendelea kufanywa kila kona na amewataka wananchi na wamiliki wa hospitali zote katika mkoa huo na mikoa mingine ya nyanda za juu kusini kutoa taarifa haraka endapo majambazi hayo yatajitokeza kutaka kutibiwa.

Tukio hilo limeamsha simanzi kubwa kwa wanafunzi wote wa Chuo Kikuu cha Mzumbe jijini hapa ambapo jana Tanzania Daima ilipotembelea, iliwakuta wanafunzi wenzake wakiwa wameweka msiba wakisubiri taratibu za kuusafirisha mwili huo kwenda Same kwa mazishi.

Marehemu anadaiwa kuwa ni ndugu wa mwanasheria maarufu hapa nchini, Dk. Ringo Tenga, ambaye baada ya taarifa za tukio hilo, marafiki wa jirani na mwanasheria huyo, waliwapigia simu baadhi ya waandishi wa habari kuelezea juu ya kifo cha mwanachuo huyo.

Tukio hilo limekuja huku Rais Kikwete akiwa ameyatangazia vita majambazi, akisema sasa atachukua hatua mbaya zaidi katika kuhakikisha msako dhidi ya ujambazi unafanyika kwa ufanisi.

Rais Kikwete aliyarudia hayo, safari hii kwa msisitizo mkubwa alipokuwa anahitimisha ziara yake mkoani Arusha.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.