RAIS Jakaya Kikwete jana alimaliza ziara yake mkoani hapa, akielekeza ujumbe wake dhidi ya majambazi, na watendaji serikalini wanaotumia nafasi zao kuwaonea maskini kwa kuwapokonya ardhi na kuwapa matajiri katika mazingira yasiyokubalika.
Kikwete ambaye bila kufafanua, alisema hatua hizo zitazusha lawama nyingi, alitoa kauli hiyo mjini hapa jana, wakati wa mkutano wa majumuisho ya ziara yake ya kikazi mkoani hapa.
Alisema ili kufanikisha azma yake ya siku zote ya kukabiliana na ujambazi, serikali itaongeza nguvu kwa Jeshi la Polisi ili kuimarisha msako wa majambazi.
Rais ambaye tangu aingie madarakani amekuwa akisisitiza dhamira yake ya kukabiliana na vitendo hivyo ambavyo vimelipuka tena katika siku za hivi karibuni, hususan katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, alisema salama pekee ya watu hao itakuwa ni kuondoka wenyewe hapa nchini.
“Naongea maneno haya nikiwa namaanisha na natambua katika hatua tutakazochukua hivi sasa, tutapata lawama nyingi, lakini hatutakuwa na haya kwa yoyote yule. Naomba wananchi mtoe ushirikiano kwa Jeshi la Polisi,” alisisitiza.
Akizungumzia kuhusu watendaji wa serikali wanaonyanyasa maskini katika ugawaji wa ardhi, alisema hatasita kufuta viwanja vyote vilivyotolewa na halmashauri kwa matajiri kinyume cha utaratibu, hata kama waliopewa viwanja hivyo wanazo hati za kuvimiliki.
Alisema serikali imeamua kuchukua hatua hiyo ikitambua kwamba, isipofanya hivyo sasa, basi hali itakuwa mbaya siku za baadaye.
Rais alisema pia kwamba, kumekuwa na tabia ya watendaji serikalini na katika halmashauri kutumia udhaifu uliopo kwa baadhi ya wananchi kukosa elimu, kuwashawishi katika vikao, hususan vya vijiji, kuidhinisha ugawaji wa ardhi.
“Naomba niseme wazi kuwa, endapo nitaletewa malalamiko ya kiwanja kugawiwa kwa mtu eneo ambalo wakazi wake hawakuliridhia, nitatengua hati ya umiliki wa kiwanja hicho na kukirudisha kwa wananchi wa kijiji hicho,” alisema.
Kikwete aliwataka watendaji kuwa na imani na wanyonge na wasiwe na tabia ya kuegemea upande wa matajiri kwani ipo siku hao wanyonge na masikini watamtafuta masikini mwenzao wanayemuamini na kumpa uongozi ili awatetee.
“Ndugu zangu, haya mambo ninayowaambia si hadithi, yanatokea hapa duniani, angalieni Venezuela na nchi nyingine za Amerika ya Kusini, matatizo ya ardhi ndiyo chanzo cha migogoro mingi katika nchi hizo,” aliongeza Kikwete.
Alisema kuwa iwapo kuna mtu atahitaji ardhi katika kijiji husika, watendaji wahakikishe kuwa wenyeji wanapata kwanza ardhi hiyo, ndipo mgeni huyo naye apewe, tena kwa kushirikisha wakazi wa eneo hilo.
Aliwahakikishia wananchi wa Ngorongoro kuwa, ujenzi wa barabara kutokea Mto wa Mbu kupitia Ngarasero hadi Loliondo, utafanyiwa kazi mapema iwezekanavyo na akawaagiza TANROADS kuishughulikia barabara hiyo.