Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Uuzaji wa nyumba za Tazara una walakini
Uuzaji wa nyumba za Tazara una walakini
By Habari Tanzania | Published  03/22/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated

SUALA la uhaba wa nyumba kwa askari polisi ni tatizo lililo wazi na la siku nyingi nchini.

Askari wengi wanaishi katika mazingira magumu wakiwa kwenye makazi yanayofanana na wakimbizi.

Ukiona nyumba za askari wenye jukumu zito la kulinda usalama wa raia ni aibu kusimulia.

Tatizo la nyumba kwa askari ni la kudumu, kwani miaka nenda rudi askari wameonekana wakiishi katika nyumba za ajabu, za mabati , magofu na wengine katika mahema wakiganyagana kama kaa ndani ya kapu wakiwa na familia zao.

Mambo mengine yanatia aibu, askari wetu wanafikia hatua ya kulala chumba kimoja kidogo na watoto, huku watoto wakishuhudia yanayoendelea kwenye kitanda cha wazazi wao.

Askari wa aina hii, kwanini asipokee rushwa na kwenda kupanga nyumba kubwa kwa gharama zake ili kuachana na nyumba za serikali zinazofanana na matundu ya viota vya ndege.

Pamoja na tatizo hilo la nyumba kwao, wapo baadhi ya watu ambao kwa manufaa binafsi na pengine kwa kutoona umuhimu wa watu hao, wanaamua kuwaongezea machungu askari hao kwa kuwanyanyasa hata katika hivyo vijumba vidogo ambavyo wamekubali kuishi ili kuweza kulitumikia taifa lao.

Nasema vijumba kwa kuwa hata hivyo bado havina hadhi ya kuishi wafanyakazi hao ambao wana familia wakiwa na wake na watoto.

Nimelazimika kuandika makala hii kutokana na mgogoro wa nyumba waishizo askari polisi zilizopo eneo la Veterinary – Temeke, ambazo zinamilikiwa na Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA) kuamriwa kuhama na watu wanaodai kununua nyumba hizo.

Askari polisi waishio katika nyumba hizo wameingia katika msukosuko wa kutakiwa kuhama katika nyumba hizo ambazo ni kambi ya polisi kwa madai kuwa nyumba hizo zimeuzwa kwa wafanyakazi wa shirika hilo.

Pamoja na kudaiwa kuwa nyumba hizo zimeuzwa, lakini uuzwaji wa nyumba hizo umefanywa katika hali ya usiri kwani askari wanaoishi humo hawakujulishwa.

Askari hao hawakuwa na taarifa, kwani kama wangekuwa na taarifa wangeweza kuzinunua wao, hasa ukizingatia kuwa tayari wanaishi kwenye nyumba hizo.

Askari hao wameishi humo wakiwa wanabadilishana, baada ya baadhi yao kuhama vituo na wengine kustaafu, hadi shirika hilo lilipoamua kuwapunguza askari hao kutokana na sababu zao binafsi na kubaki na askari wachache.

Hadi sasa askari hao wameshindwa kutoka, kwani hawana sehemu za kwenda, kutokana na tatizo hilo la nyumba.

Askari hao waliendelea kuishi humo kwa kutambua kuwa lengo lao ni moja, hivyo kuishi katika nyumba hizo ni sawa, kwani bado zipo chini yao.

Lakini hivi karibuni askari hao walishtushwa na baadhi ya watu wanaojiita kuwa wamiliki halali wa nyumba hizo kutoka Dar es Salaam, Makambako, Mbeya, Mang’ula na kwingineko.

Watu hao wametoa notisi ya siku 30 ya kuwataka askari hao wahame kwani wanataka kufanya ukarabati kwenye nyumba hizo, kwa madai kuwa shirika hilo lilikwisha kuwauzia tangu mwaka juzi.

Swali la kujiuliza ni kwamba, nani ambaye ameuza nyumba hizo au kutoa idhini ya kuziuza?

Ilikuwaje watoke uko walipo na kuja kununua nyumba ambazo wanaishi wafanyakazi wa serikali wa Dar es Salaam?

Na iwapo ilitolewa idhini ya uuzwaji wa nyumba hizo askari hao kwa nini hawakupewa taarifa na viongozi wao au shirika hilo kwamba nyumba hizo zinauzwa ili nao waweze kujiandaa kununua?

Ni wazi kuwa uuzwaji wa nyumba hizo haukuzingatia haki wala utu wa mtu hata kidogo.

Je, shirika hilo limepata wapi ujasiri wa kuuza nyumba hizo pasipo kuwashirikisha watu hao ambao ndio hasa walinzi wa mali zao, ambao hawalali usiku na mchana kwa kuwalindia nyaya, vipuri na vifaa vyote ambavyo vinahusika na uendeshaji wa reli hiyo ili maharamia wasije kuhujumu!

Wanafanya kazi kwa moyo wa kujituma na kujitolea, si sasa tu, tangu miaka yote iliyopita ambapo shirika hilo lilikuwa likimiliki askari lukuki.

Nafikiri kiburi cha shirika hilo kinafaa kiangaliwe kwa macho mawili, kwani inawezekana kiliwekwa na wakubwa ambao hawaoni umuhimu wa watu hao wasiolitakia mema Jeshi la Polisi.

Watu ambao wanalipwa mishahara midogo, wanakubali kukaa hata kwenye mahema, kulala nje kwa ajili ya kulinda mali za raia na taifa, leo hii wanaambiwa waondoke, wanafukuzwa kama mbwa kwenye nyumba ambazo wameweza kuzitunza zaidi ya miaka 28. Iko wapi thamani yao katika nchi hii?

Kwa kweli suala hili lisifumbiwe, macho kwani ni unyanyasaji na udhalilishaji ambao unalivua nguo taifa la Tanzania na jeshi kwa kuonyesha kuwa nchi hii haina haki kwa raia wema.

Hakuna anayeamini kuwa TAZARA imeweza kufanya hivyo. Lazima kuna mshauri na mwalinu katika hili, tena huyo mwalimu ana chuki binafsi na askari hao pamoja na familia zao.

Mara ngapi askari hao wanahatarisha maisha yao kulitetea shirika hilo kwa kupambana na majambazi, vibaka na wahalifu wote wanaojaribu kufanya uharamia ili kulihujumu shirika?

Ni kiasi gani ambacho askari hao wanalidai shirika hilo kwa kufanya kazi miaka nenda rudi na kushindwa kuwalipa kwa wakati muafaka.

Kama kweli shirika hilo limeamua kuuza nyumba hizo kwa nini lisingewapa kipaumbele askari hao ambao wanavumilia hayo yote, raia hao wema ambao wanalidai shirika hilo kutokana na kulifanyia kazi lakini limeshindwa kuwalipa hadi wengine kifo kuwachukua bila kula jasho lao.

Na kama wanauza kihalali, ni kwa nini waamue kumuumzia mtu mmoja milango minne ambayo askari hao wanaishi na familia zao na kuwafanya wajinga na wanyonge kwa kuwahamishia uswahilini ambapo watashindwa kufanya kazi zao kwa usalama na haki kutokana na kuchanganyika na watu tofauti.

Nasema tatizo hilo lisifumbiwe macho kwani linaweza kuwa sugu kwa askari ambao wanatumiwa na mashirika mbali mbali kuchukua mfano wa kiburi kwa shirika hilo, kwa kitendo chake ambacho si cha kiungwana.

Serikali na Jeshi la Polisi itoe tamko juu ya hatima ya askari hao na haki waliyonayo, ili shirika hili liweze kujua kuwa kilichofanyika si sahihi.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.