Na Mohammed Abdullahman, Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Amani Abeid Karume, amemshitaki Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, kwa Serikali ya Uingereza, kwamba aheshimu maamuzi ya wananchi.
Rais Karume alitoa mashitaka hayo jana wakati wa mazungumzo yake na Balozi wa Uingereza nchini, Philip Perham, aliyetembelea Ikulu Zanzibar kwa mazunguzo na Rais Karume.
Rais Karume alisema ni hatari kwa wananchi wa Zanzibar kuwakabidhi madaraka viongozi wa upinzani ambao hawana utamaduni wa kuwapisha wenzao kushika nyadhifa za juu ndani ya vyama hivyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kitengo cha habari Ikulu ya Zanzibar , Rais Karume amesema imedhihirika wazi kwamba vyama vya upinzani viongozi wake wana tabia ya kuhodhi madaraka kwa muda mrefu, jambo ambalo si la kawaida katika siasa za demokrasia ya vyama vingi.
“Jambo ambalo linatishia uimara wa hali ya kisiasa nchini ni kwamba kwa upande wa vyama vya siasa vya upinzani, vimedhihirika kuwa baadhi ya viongozi wake wanahodhi madaraka kwa muda mrefu, jambo ambalo si la kawaida katika siasa za kidemokrasia,” alisema Rais Karume.
Katika mazungumzo hayo, Rais Karume hakumtaja kiongozi wa chama cha siasa, lakini Katibu Mkuu wa CUF, Seif Sharif Hamad, ndiye amejitokeza kuwa mgombea urais wa Zanzibar mihula yote mitatu tangu kuanzishwa mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Hamad mara ya kwanza aliangushwa katika uchaguzi wa mwaka 1995 na Rais mstaafu wa Zanzibar , Dk. Salmin Amour, baadaye aliangushwa mara mbili na Rais wa sasa wa Zanzibar , Amani Abeid Karume.
Rais Karume alisema kumejitokeza tabia kwa baadhi ya viongozi wa upinzani kupotosha taarifa za kisiasa na mwenendo mzima wa maendeleo, jambo ambalo alisema ni hatari na linaweza kuharibu amani katika jamii.
Rais Karume alisema hivi sasa SMZ inaelekeza nguvu zake kisiwani Pemba ili kuweka uwiano wa ukuaji sekta ya uchumi kati ya Kisiwa cha Unguja na Pemba .
Alisema hatua ya kuimarisha miundombinu ya mawasiliano itasaidia kukaribisha wawekezaji katika kisiwa hicho na kukuza hali ya maisha ya wananchi wa huko.
Akizungumzia kauli hiyo, Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salum Bimani alisema Hamad si king'ang'anizi wa madaraka, isipokuwa Rais Karume anamhofia inapofika wakati wa uchaguzi.
Bimani alisema Maalim Seif hujitokeza kugombea nafasi hiyo kutokana na ridhaa ya wanachama wa CUF, kupitia vikao halali na kupewa nafasi kubwa ya kisiasa na wananchi wa Zanzibar , lakini kikwazo kikubwa ni viongozi wa SMZ na CCM.
“Sisi tumekuwa tukishinda lakini hatupewi nafasi, na inaonekana Maalim Seif ni mwiba unaowanyima usingizi viongozi wa CCM,” alisema Bimani.
Alisema msimamo wa CUF ni kwamba uchaguzi wa Zanzibar ulivurugwa na kuna haja ya kufanyika uchaguzi mwingine chini ya usimamizi wa jumuiya ya kimataifa.
Kutoka: Tanzania Daima