BAADA ya kuwa kimya kwa kipindi kirefu, majambazi wameibuka kwa kasi mkoani Arusha na kusababisha kifo na uporaji.
Wakitumia staili mbalimbali, kundi moja la majambazi waliwavamia watalii wakati kundi jingine likiziba barabara na kuteka magari.
Rais Jakaya Kikwete, ambaye yupo katika ziara mkoani humo, jana alilazimika kumuondoa Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, kutoka Karatu alikokuwa naye na kurudi mjini Arusha kuhakikisha kuwa anasimamia operesheni ya kuwasaka majambazi hao.
Hayo yalitokea kufuatia taarifa kuwa, watu wawili, wanaodhaniwa kuwa majambazi wakiwa na silaha, waliwavamia watalii na kuwamiminia risasi na kumuua mmoja wao na kuwajeruhi wengine pamoja na mtu aliyekuwa akiwaongoza.
Rais Kikwete alitoa agizo hilo kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Karatu jana mchana baada ya kupewa taarifa ya watalii hao kupigwa risasi.
Habari kutoka Arusha zilipasha kuwa watalii hao walikumbwa na mkasa huo wakati wakitembea kwa miguu kutoka katika Hoteli ya Mountain Village, iliyopo Arumeru, yapata kilometa 15 kutoka mjini Arusha. Walikuwa wakielekea kupanda Mlima Kilimanjaro.
Wakati akitoa ruhusa kwa RPC kuondoka, Rais Kikwete alisema serikali haitakubali kuona watu wachache wanatumia uhuru wao kukatisha maisha ya watu wengine na kuagiza jeshi hilo kuwakamata wale wote waliohusika katika tukio hilo.
Katika tukio hilo majambazi hayo yalimpiga risasi ya tumbo mtalii wa kike aliyekuwa mjamzito raia wa Uingereza na kufariki papo hapo.
Ingawa polisi walishindwa kuthibitisha kifo hicho, lakini watalii hao wametambuliwa kuwa ni Jaquie Lutz, raia wa Marekani, Raymond Mollica na R.G. Lutz.
Katika sakata hilo, mtu aliyekuwa akiwaongoza watalii hao, aliyefahamika kwa jina la Charles Safari, alijeruhiwa baada ya kupigwa risasi na majambazi hao.
“Baada ya kuona wamefanikiwa kumpiga risasi ya tumbo yule mtalii wa kike, majambazi hayo yaliamua kumgeukia mwongazaji wao na kumpiga risasi ya kichwa na kumjeruhi vibaya,” kilisema chanzo chetu cha habari.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa simu kutoka Arusha, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani humo, Evarist Mangara, alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema jeshi hilo linaendesha msako mkali katika maeneo mbalimbali ili kuwatia mbaroni wale waliohusika.
Alisema tukio hilo lilitokea jana majira ya saa nne asubuhi ambapo majambazi hayo yalikuwa yakitumia bastola na mapanga kuwapiga watalii hao.
“Ni kweli tukio hili limetokea majira ya saa nne asubuhi na hadi sasa timu yetu ya askari ikiongozwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Basilio Mathei, iko kwenye eneo la tukio kwa ajili ya kuendesha msako wa wale wote waliohusika,” alisema Mangara.
Alisema hadi jana jioni walikuwa hawajapata taarifa ya mtalii kuuawa lakini alikiri kuwa wamepigwa risasi na hali zao si nzuri.
Aidha, alikiri kuwa mtu aliyekuwa akiwaongoza naye amejeruhiwa vibaya na alikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, mkoani Kilimanjaro, kwa ajili ya matibabu.
Alisema watalii wengine waliojeruhiwa vibaya kwa risasi walilazimika kukimbizwa Nairobi nchini Kenya kwa ajili ya matibabu zaidi na wametambuliwa kuwa ni raia wa Marekani.
Wakati huo huo, watu watano wanaosadikiwa kuwa ni majambazi, baadhi yao wakiwa wamevalia sare za askari wa usalama barabarani, juzi usiku waliteka magari matano ya kubebea mizigo na kupora mamilioni ya fedha katika eneo la Makuyuni.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana jana, tukio hilo lilitokea majira ya saa 3 usiku na majambazi hao walitokomea baada ya tukio hilo.
Habari kutoka kwenye eneo la tukio, zimeeleza kuwa kabla ya watu hao kupora, waliweka vizuizi barabarani na kuyalazimisha magari yote yaliyokuwa yakipita katika barabara hiyo kusimama.
Kisha waliwalazimisha waliokuwamo katika magari hayo kushuka na waliwapekua wao na mizigo yao.
Habari hizo zimeeleza kuwa majambazi hao, ambao baadhi yao walikuwa na silaha za moto, yalitanda eneo lote na kuendesha unyama huo katika muda mfupi tu na kisha kutokomea porini.
Walioshuhudia tukio hilo walisema kuwa walidhania kuwa watu hao walikuwa ni askari wa usalama barabarani kutokana sare nyeupe pamoja na makoti waliyokuwa wamevaa.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Evarist Mangara, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa upelelezi wa tukio hilo bado unaendelea ili kuwatia mbaroni watuhumiwa hao.