Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Kwanini shilingi ya Tanzania inaporomoka?
Kwanini shilingi ya Tanzania inaporomoka?
By Habari Tanzania | Published  03/20/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:

BENKI Kuu ya Tanzania imekuwa ikizungumzia mara nyingi juu ya mfumuko wa bei, viwango vya ubadilishaji wa fedha za kigeni, riba za benki mbalimbali na taasisi za fedha, ili kuelewa tunatoka wapi katika safari ya kuimarisha uchumi.

Ni muhimu kuangalia hali ya uchumi wa miaka 15 iliyopita katika miaka ya mwanzo ya 2000.

Kati ya mwaka 1995 hadi 2000, mfumuko wa bei, yaani ongezeko la bidhaa zote za mlaji zimekuwa zinapanda bei kwa kati ya asilimia 30 hadi asilimia 36 kila mwaka.
Kwa hali hiyo, fedha imepoteza thamani kwa sababu uwezo wake wa kununua bidhaa umepungua sana.

Riba zinazotozwa na kutolewa na mabenki kwa amana ilibidi ziongezeke kwa sababu ya kupanda kwa bei za bidhaa.

Benki ingepata hasara kama ingekopesha fedha kwa riba ya asilimia kumi wakati mfumuko wa bei ulikuwa asilimia thelathini vile vile walioweka fedha zao katika benki ilibidi walipwe riba za amana za juu.

Hata hivyo hali hiyo haikuwezekana kwa sababu benki zilikuwa mbili, yaani NBC na CRDB na zilikuwa na ukiritimba wa shughuli za kibenki na wawekezaji amana hawakuwa na uchaguzi wa wapi waweke amana zao ili wapate riba ya juu zaidi.
Serikali ya Awamu ya Tatu ilijitahidi kukusanya kodi za mapato, ushuru wa forodha na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Mwaka 1995 Mamlaka ya Kodi TRA ilikuwa inakusanya sh bilioni 30 kwa mwezi lakini baada ya kuongeza bidiii ya kusimamia makusanyo ya kodi, ilipofika mwaka 2000, makusanyo ya kodi kwa mwezi yalifikia sh bilioni 156 na hii imeongezeka hadi zaidi ya sh bilioni 260 kwa mwezi katika awamu ya nne.

Kuongezeka kwa makusanyo ya kodi kulikuwa na faida mbili muhimu katika serikali yetu.

Kwanza, serikali iliweza kupunguza kasi ya bajeti ya serikali na hivyo kupunguza kiwango cha fedha ambazo serikali hukopa kutoka katika benki mbalimbali na hasa Benki Kuu.

Ukopaji huu wa serikali ukiwa wa kiwango cha juu sana huchangia mfumko wa bei kwa ajili ya kuongezeka kwa mzunguko wa fedha wakati uzalishaji wa bidhaa hauongezeki.

Mapato ya ndani ya serikali yakiongezeka ukopaji kutoka nchi za nje hupungua.
Jambo la muhimu zaidi ni kwamba uwezo wa kulipa madeni ya wafadhili huongezeka na matokeo yake ni kupata misamaha ya madeni kwa nchi maskini kama Tanzania katika mpango wa HIPC, na nchi inajenga imani kwa wafadhili kwa kuwa inaonekana inaweza kukopesheka.

Serikali iliongeza nidhamu katika matumizi ya fedha za serikali na kupunguza ujazi au ongezeko la fedha kutoka Benki Kuu ‘money supply’ kufuatana na sera ya fedha ya kubana ongezeko la fedha katika uchumi kufikia asilimia 10 - 12 kwa mwaka.

Kwa kutumia mikakati kama kuuza dhamana za serikali fedha za ziada katika uchumi (excess liqudity), hupungua na hiki ndicho kinachosaidia kupunguza mfumuko wa bei.

Mwaka 1995, mfumuko wa bei ulikuwa asilimia 30 lakini kufikia mwaka 2002 mfumuko wa bei ulipungua hadi kufika asilimia tano na hadi sasa mfumko wa bei umefikia asilimia 4.4.

Hii ina maana bila kuongeza mishahara au mapato mengine kwa wananchi kwa fedha zile zile kwa mwezi kama mapato kushuka kwa mfumko wa bei, kunawawezesha walaji kununua bidhaa nyingi zaidi.

Bidhaa hizi ni pamoja na vyakula, nguo, viatu na bidhaa za ngozi, gharama za usafiri, bidhaa za ndani kama radio na TV, gharama za burudani na kwa ujumla bidhaa zote za mlaji.

Wananchi wa kawaida hufaidika na kushuka kwa mfumuko wa bei kwa sababu matumizi yao ya kawaida kwa chakula ni zaidi ya asilimia 64 ya mshahara au mapato yao kwa mwezi.

Kuimarika kwa uchumi mkuu au ‘macro-economic stability’ ni pamoja na ongezeko dogo la bei za bidhaa zote kwa jumla, ubadilishaji wa fedha za kigeni usiobadilika mara kwa mara na vile vile riba za mabenki zinatabirika.

Wataalamu wa uchumi wanasema kwamba kudhibiti wa mfumuko wa bei huvutia wawekezaji wa nje na ndani ya nchi kwa sababu inakuwa rahisi zaidi kwa wawekezaji kupanga mipango yao ya biashara.

Hii ni pamoja na kujenga mazingira mazuri ya uwekezaji kama kuwa na vivutio vya misamaha ya baadhi ya kodi kwa wawekezaji, uboreshaji wa miundo mbinu, utawala bora na kupiga vita rushwa.

Kati ya mwaka 1995 uwekezaji kutoka nje umeongezeka kutoka dola za Marekani milioni kumi kwa mwaka hadi kufikia dola 350 mnamo mwaka 2004 na juhudi zikifanywa kuvutia uwekezaji kuna uwezo wa kuongezeka kwa uwekezaji hadi kufikia dola 500 milioni kwa mwaka katika kipindi kifupi kijacho, na haya yamewezekana kwa kuimarisha uchumi mkuu na hasa kudhibiti mfumuko wa bei.

Matokeo ya ongezeko la uwekezaji ni pamoja na kuongeza bidhaa zinazozalishwa soko la ndani kwa bei nafuu na ukuzaji wa ajira na fursa nyingi za kuongeza mapato kwa waajiriwa na wale wanaotoa huduma kwa wawekezaji kama sekta ya viwanda na madini.

Wakulima wa pamba wanapata soko la ndani kama viwanda vingi vya nguo vikianzishwa, hivyo kuwawezesha wakulima hao kiuchumi.

Lakini Watanzania hawategemewi kuwa na uchumi mkuu ulioimarika au ‘Macro-economic Stability’.

Kuimarika kwa uchumi ni lazima kusaidie ukuaji wa sekta mbalimbali za uchumi na shughuli za kibiashara, viwanda na uzalishaji kwa wawekezaji au ‘micro-economic units’.

Ukuaji wa uchumi ulikuwa chini ya asilimia 4.4 mwaka 1995, na sekta nyingine zikawa hazikui kabisa hasa viwanda ambavyo vilidumazwa na sera mbalimbali, ikiwamo kulegeza masharti ya biashara ambapo bidhaa nyingi ziliagizwa kutoka nje ya nchi kwa bei nafuu na hivyo bidhaa za ndani kukosa soko.

Kuwa na sera nzuri za biashara, viwanda, madini na utalii kumeongeza uzalishaji katika sekta hizi.

sekta ya madini sasa inakuwa kwa asilimia 17 na kuchangia asilimia nne katika pato la taifa.

Sekta ya viwanda inakua kwa asilimia 8.4 na kuchangia asilimia katika pato la taifa, hivyo kuliweka taifa katika nafasi ya juu kiuchumi.

Vilevile sekta ya utalii imekuwa ikifanya vizuri kwa ukuaji wa asilimia 12 na kuchangia asilimia 16 katika pato la taifa na kupata sh bilioni 600, fedha za kigeni, ikiwa nyuma ya kilimo na madini katika kukuza akiba ya fedha za kigeni.

Ili wananchi wanufaike kwa ukuaji wa uchumi kuna umuhimu katika maisha yao kuwa bora zaidi kwa kupunguza umaskini.

Ndiyo maana serikali ikabuni Mpango wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini (MKUKUTA) kama sera ya ukuaji uchumi na kupunguza umaskini kwa wananchi wake ambao wengi wao ni maskini.

Bajeti kubwa ya serikali inaelekezwa katika sekta za elimu, afya, barabara za vijijini na mapambano dhidi ya HIV-Aids, malaria, TB na magonjwa mengine.

Hata hivyo bajeti hiyo haiwafikii walengwa kama inavyoeleza na badala yake wanaonufaika ni wale wale waliopo madarakani na kuwaacha wananchi wakiendelea kutaabika kwa umaskini wao.

Kuimarika kwa uchumi ni lazima kuwezeshe wananchi wengi zaidi kupata huduma za jamii na za kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kuboresha maisha yao.
Tanzania ni nchi maskani ambayo asilimia hamsini ya watu wake huushi kwa matumizi ya chini ya dola moja ya kimarekani kwa siku, japokuwa imezungukwa na maliasili zinazoiweka nchi katika kiwango cha juu kiuchumi.

Tunaposema Tanzania ni maskini tunakosea, kwani uchumi tunao wa kutosha hususan katika sekta za utalii na madini.

Hivyo sera ya uwezeshaji na sera ya kurasimisha mali na biashara katika sekta isiyo rasmi ina lengo la kuongeza ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini.
lengo hilo linapotoka kutokana na kuwa malengo yaliyowekwa hayatiliwi mkazo na kufanyiwa kazi kwa kutekeleza sera ya kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Wataalamu wa uchumi wa mashirika ya kimataifa ya fedha na wa hapa nchini wanaamini kuwa kama uchumi ukikua kwa asilimia 8 hadi 10, lengo la kupunguza umaskini litafikiwa.

Tanzania ni moja wapo ya nchi ambazo zilitia saini mwaka 1999 kufikia malengo ya milenia (Millennium Development Goals) .

Kuna kila dalili kuwa Tanzania itafikia baadhi ya malengo hayo ifikapo mwaka 2015 kama uchumi utaendelea kuimarika.

Malengo hayo ni kupunguza umaskini wa kipato kwa wananchi ifikapo mwaka 2015.

Lengo jingine ni kila mtoto anayefika umri wa kwenda shule aingie shule za msingi au (Universal Primary Education) na lengo hili limefikiwa zaidi ya asilimia 90.

Malengo mengine ni kupambana na maradhi kama VVU, UKIMWI, TB na malaria.
Kupunguza umaskini ni pamoja na kuondoa njaa na kuongezeka kwa lishe kwa watu walio wengi nchini.

Malengo ya milenia ni pamoja na kupunguza vifo vya kina mama wazazi na vifo vya watoto chini ya miaka mitano, malengo mengine ni kuwawezesha kina mama kiuchumi na kuboresha mazingira kwa kuwa na maendeleo endelevu au ‘Environmental Sustainability’ lengo jingine ni kukuza ushirikiano na mataifa mengine katika maendeleo.

Kukua kwa uchumi ni lazima kuendane na kupunguza tofauti kati ya wananchi wenye vipato vya juu na wale wenye kipato cha chini.

Ukuaji wa uchumi lazima ulete maendeleo ya kiuchumi na huduma za jamii kwa sababu kama Mwalimu J.K. Nyerere alivyokuwa akisema, maendeleo ni lazima yaboreshe maisha ya watu.

Hivyo ukuaji wa uchumi lazima ulete maisha bora kwa Watanzania wote ambao ni lengo kuu la Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.