DALILI za awali za matokeo ya Uchaguzi Mdogo wa Ubunge Tunduru, zimeanza kuonyesha dhahiri kwamba, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeshinda kwa mara nyingine tena.
Ushindi huo wa CCM katika uchaguzi huo, unazidi kukiwekea rekodi nyingine chama hicho kikongwe cha siasa ya kushinda mara nyingi katika chaguzi ndogo tangu kuasisiwa kwa mfumo wa vyama vingi Julai mwaka 1992.
Kwa kunyakua kiti hicho kilichokuwa kikishikiliwa na Juma Akukweti aliyefariki kwa majereha ya moto yaliyotokana na ajali ya ndege Januari mwaka huu, CCM imeendelea kuvifanya vyama vya upinzani viendelee kubakia na rekodi ya kushinda majimbo ya Temeke na Magu tu katika uchaguzi mdogo.
Wakati Augustine Mrema, akiwa Mwenyekiti wa Taifa wa NCCR Mageuzi, alishinda Jimbo la Temeke katika uchaguzi mdogo na John Cheyo akiwa katika wadhifa kama huo huo katika chama cha United Democratic (UDP) alishinda ubunge huko Magu mwaka 2003.
Mbali na majimbo hayo mawili, CCM imekuwa ikishinda chaguzi nyingine zote ndogo kuanzia mwaka 1992 ukianzia na Kwahani (Zanzibar), Ileje (Mbeya), Makete (Iringa), Igunga (Tabora) na hata Bariadi Mashariki (Shinyanga).
Ukiacha mwenendo huo wa chaguzi ndogo, hali imekuwa hivyo hivyo hata wakati wa Uchaguzi Mkuu, kwani majimbo ambayo wapinzani wamekuwa wakiyapata tangu mwaka 1995 yamekuwa yakiendelea kupungua, ukiweka kando hali ya kisiasa Zanzibar.
Kimsingi, kila unapofanyika uchaguzi uwe mdogo au mkubwa, mwenendo wa mambo katika hali ya jumla umekuwa ukionyesha namna CCM ilivyo na nguvu kubwa kuliko walivyo wapinzani.
Ingawa ni kweli kwamba nguvu za CCM zina mizizi ya kihistoria, ni kweli pia kwamba, jeuri hiyo ya chama tawala imekuwa ikichombezwa na harakati na operesheni za waziwazi na nyingine za chinichini za vyombo vya dola.
Mwenendo wa vikosi vyetu vya usalama kila mara unapofanyika uchaguzi, hususan katika maeneo ambayo nguvu ya upinzani huonekana kuwa kubwa, umekuwa ni wa kutiliwa shaka.
Hali kama hiyo ya vyombo vya dola kutumia nguvu kubwa kupita kiasi, imewahi kutokea wakati Mrema alipokuwa tishio kubwa kwa CCM Temeke, Dk. Masumbuko Lamwai alipokuwa na mabavu ya kutosha Ubungo, Cheyo alipokitikisa chama tawala Magu na katika chaguzi nyingine zote huko Zanzibar.
Huko Tunduru nako, ambako CUF imekuwa ikionekana kuwa na nguvu za kutosha hata wakati wa kampeni za mwaka juzi, kulikuwa na matukio ya polisi wetu kupambana na wapinzani kwa mawe na mabomu ya machozi yaliyokwenda sambamba na kutiwa ndani mara kadhaa kwa wafuasi na wapenzi wa vyama vya CUF na CHADEMA.
Mwenendo huu wa mambo unaodhoofisha vyama hivi vya upinzani unaokwenda sambamba na kununuliwa kwa kasi kwa viongozi wa ngazi mbalimbali wa upinzani, ni mambo ambayo yanathibitisha kitu kimoja kwamba, bado hatujajiandaa vya kutosha kuendesha mfumo wa ushindi wa vyama vingi.
Ingawa CCM imekuwa ikifanya kila linalowezekana kushinda kila kiti, kiwe cha udiwani, ubunge na hadi urais, uwiano mbovu wa kiuwakilishi kati ya chama hicho tawala kwa upande mmoja na wapinzani kwa upande mwingine, unaendelea kuifanya nchi yetu iendelee kuwa dhaifu katika uimarishaji wa misingi ya demokarasia na utawala bora.
Wakati CCM ikijipanga kuendeleza jadi yake ya kushangilia kila ushindi inaoupata, inapaswa kutambua pia kwamba, upinzani dhaifu huzaa demokrasia legelege na hatimaye serikali dhaifu.