HATIMAYE wapiga kura wa Jimbo la Buchosa mkoani Mwanza, wameibuka na kuwaomba wataalamu wa mambo ya sheria wawasaidie kumfungulia kesi mahakamani, Mbunge wao, Samwel Mchele Chitalilo, ambaye mamlaka zimethibitisha kuwa ameghushi vyeti vya elimu yake.
HATIMAYE wapiga kura wa Jimbo la Buchosa mkoani Mwanza, wameibuka na kuwaomba wataalamu wa mambo ya sheria wawasaidie kumfungulia kesi mahakamani, Mbunge wao, Samwel Mchele Chitalilo, ambaye mamlaka zimethibitisha kuwa ameghushi vyeti vya elimu yake.
Wapiga kura wa jimbo hilo, wamewasafirisha wawakilishi wao wawili kuja Dar es Salaam, kwa ajili ya kutafuta msaada wa kisheria ili waweze kumfungulia kesi ya jinai mbunge huyo.
Wakizungumza katika ofisi za gazeti hili jana, wawakilishi hao wa wapiga kura 184 wa Buchosa, walisema kuwa wamejiandaa kulipa gharama za kesi hiyo.
Wawakilishi hao walijitambulisha kuwa ni Amani Ramadhani, ambaye shahada yake ya kupigia kura ina namba 10246048 na Henriko Mshereja, mwenye shahada namba 12517837.
Ramadhani, alisema wamefikia uamuzi wa pamoja wa kuomba msaada wa kisheria ili Chitalilo afikishwe mahakamani kwa mujibu wa sheria za mwenendo wa makosa ya jinai zinazoruhusu mtu kushtakiwa kwa utaratibu wa uendeshaji mashtaka binafsi (Private Prosecution).
“Tumechukua uamuzi huu baada ya kudhihirika wazi kuwa serikali, kupitia kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), hawana mpango wa kumfikisha Chitalilo mahakamani hata baada ya mbunge huyo mwenyewe kuuthibitishia umma kwamba kweli ameghushi vyeti vya elimu yake,” alisema Ramadhani.
Walisema uamuzi wao pia umezingatia kuwa, huko nyuma aliyewahi kuwa Mbunge wa Temeke, Ramadhan Kihiyo, alilazimika kujiuzulu wadhifa huo, baada ya kudhihirika kuwa alikuwa ameghushi vyeti na kusema uongo kuhusu elimu yake, ili kushinda ubunge kama alivyofanya Chitalilo.
“Tunapenda kuuarifu umma kuwa ilipothibitika kuwa Chitalilo amefanya makosa hayo, alipoteza heshima inayoendana na wadhifa wake mbele yetu sisi wapiga kura wake.
“Na tunaamini kuwa, hadi hapo atakaposafishwa mahakamani… kuendelea kumuita mheshimiwa ni kutudhihaki sisi tuliomchagua na ni tusi kubwa kwa Bunge letu tukufu na taifa kwa ujumla,” alisema.
Wawakilishi hao walidai kuwa, mbunge huyo ameacha kabisa kufanya kazi zake za ubunge jimboni humo, kwa kuwa anaona aibu.
Walidai kuwa, Chitalilo hajawahi kuingia ofisini kwake, Nyehunge ambako ndipo ilipo ofisi ya makao makuu ya jimbo, toka uchaguzi mkuu wa 2005 ulipomalizika na pia ameshindwa kuhudhuria vikao vya Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema kama anavyopaswa kisheria.
Walidai kuwa kwa sasa, Chitalilo amebaki na mradi mmoja tu wa kuhudhuria vikao vya Bunge na kuchota fedha za walipakodi bila stahili zozote.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, CCM kimemwadhibu kimya kimya Chitalilo kwa makosa hayo kwa kumzuia asishiriki uchaguzi kwa miaka kumi ijayo, lakini wakamwacha aendelee na wadhifa huo.
“Sisi tunalipinga hilo kwa nguvu zote kwani hakuna chama chochote cha siasa chenye hadhi kisheria na uwezo wa kuadhibu mtu kwa makosa ya jinai, isipokuwa mahakama tu,” alisema Ramadhani.
Walidai kwa kutoa adhabu hiyo kwa Chitalilo, CCM imewadhihirishia wapiga kura wa Buchosa kuwa ni kweli mbunge huyo alitenda kosa hilo.
“Tunafahamu pia kuwa kwa mujibu wa sheria za Tanzania, hakuna mtu aliye juu ya sheria, si mbunge wala waziri na ndiyo maana katika miaka ya 1980 ubunge wa aliyekuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, wakati huo, Jaji Joseph Warioba, ulitenguliwa na mahakama baada ya kushindwa katika kesi ya ubunge jimboni kwake mkoani Mara,” alisema Ramadhani.