Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Tunduru wakimbia uchaguzi
Tunduru wakimbia uchaguzi
By Habari Tanzania | Published  03/20/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Charles Mullinda, Tunduru

KATIKA hali ya kushangaza, watu wengi waliokuwa wamejiandikisha kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa Jimbo la Tunduru, hawakujitokeza kupiga kura.

Ukiondoa matokeo kutoka kata nne ambayo yalikuwa hayajapatikana hadi tunakwenda mitamboni jana, matokeo kutoka katika kata zaidi ya 20 zilizosalia, yanaonyesha kuwa idadi ya watu ambao hawakupiga kura ni asilimia 62.2 ya watu wote waliojiandikisha.

Kwa kujumlisha matokeo ya kata hizo, mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdallah Mtutura, anayeelekea kushinda uchaguzi huo, alikuwa amepata asilimia 24.2 tu ya kura zote zilizopigwa, ikiwa ni pungufu ya zaidi ya asilimia 35 ya waliokacha kupiga kura.

Katika matokeo hayo ya kata 21, ni kata moja tu ambako mgombea wa CUF alimshinda mgombea wa CCM. Hiyo ni katika Kata ya Namasakata, ambako watu 4,441 walikuwa wamejiandikisha kupiga kura na watu 681 walimpigia kura mgombea wa CUF, huku CCM ikiambulia kura 168. Chadema ilipata kura 87 katika kata hiyo.

Ingawa hali inaonyesha hivyo, wagombea kutoka vyama vya upinzani, hawakuiona hiyo kama moja ya sababu zilizosababisha kushindwa vibaya, badala yake walibaki wakinung’unikia miundombinu mibovu na mabavu ya nguvu za dola.

Matokeo ya awali kutoka katika kata hizo 21, yanaonyesha kuwa jumla ya watu 118,206 walikuwa wamejiandikisha kwa ajili ya uchaguzi huo lakini ni asilimia 37.9 tu ndio waliojitokeza kupiga kura.

Kati ya hao, watu 1,686, sawa na asilimia 1.8, walimpigia kura mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Shaibu Akwilombe, huku watu 14,279 wakimchagua mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF), Mazee Rajab.

Katika kata hizo, mgombea wa CCM, Abdallah Mtutura, alijizolea kura 28,609, sawa na asilimia 24.2 huku watu 73,463 wakishindwa kujitokeza kupiga kura.

Kama ilivyotarajiwa, baadhi yao walitoa shutuma kali kwa CCM, na kudai kuwa chama hicho kimewahujumu, hasa wakati wa kampeni.

Aidha, walielezea ubovu wa miundombinu katika sehemu nyingi jimboni humu, kuwa ni sababu nyingine kubwa iliyochangia kushindwa kwao.

Viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), walidai katika nyakati tofauti kuwa CCM imetumia mbinu mpya za kimafia kuhakikisha inawavuruga wapinzani.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Wilfred Lwakatare, ambaye amekuwa mjini Tunduru kwa wiki kadhaa akiongoza kampeni za CUF, alisema ushindi wa mgombea wa CCM, Mtutura Mtutura, umechangiwa na mbinu mpya za kimafia zilizotumiwa na chama hicho kuvuruga kampeni za wapinzani.

Aidha, Lwakatare, ambaye katika uchaguzi mkuu uliopita alipoteza Jimbo la Bukoba Mjini kwa mgombea wa CCM, alidai kuwa pamoja na ubovu wa miundombinu, ukwasi wa CCM, nao ulichangia kwa kiasi kikubwa kukipa ushindi chama hicho tawala.

Akifafanua kuhusu miundombinu, Lwakarate alisema kuwa ubovu wa barabara ulimkwamisha mgombea wao, Mazee Rajab, kufika katika baadhi ya maeneo yaliyokuwa na wapiga kura wengi.

“Kampeni zilikuwa ngumu, kuna maeneo zikinyesha mvua hayafikiki… mgombea wetu alishindwa kufika huko. Zipo sehemu magari yalikwama, mgombea akapanda pikipiki peke yake kwenda kwa wapiga kura.

“Sehemu nyingine hata pikipiki haipiti na sehemu nyingine hata kwa miguu hakufikiki, hili limetupunguzia sana kura zetu... ambako hatukifika (wapiga kura) walidhani tumewadharau,” alisema.

Pia alikiri kuwa mtandao mkubwa wa CCM ulikisaidia chama hicho kuwafikia watu wengi zaidi wakati wa kampeni. Hata hivyo, alidai kuwa CCM ilitumia sana vyombo vya dola kuwafikia wapiga kura wengi.

“Tunajua CCM wanatumia mtandao mpana wa serikali kupata ushindi… katika hili wanatuumiza wapinzani. Walimwagwa usalama wa taifa mpaka kwenye kata, hawa wana ‘radio call’ ambazo wanaweza kuzitumia kupanga matokeo,” alisema.

Mgombea wa Chadema, Shaibu Akwilombe, alisema alilazimika kukatisha ratiba yake ya kampeni mara kwa mara kutokana na ubovu wa barabara.

Alisema ili kufika katika baadhi ya maeneo alilazimika kutembea kwa miguu kwa saa mbili, jambo lililokuwa likimchosha na kumvurugia ratiba yake.

“Kampeni zilikuwa nzuri, tatizo lilikuwa miundombinu, baadhi ya sehemu nilitembea kwa saa mbili nikiwa nimeacha gari langu ili kuwafikia wapiga kura, hili lilinichosha sana na kuvuruga ratiba yangu ya kampeni,” alisema Akwilombe.

Mbali ya ubovu wa barabara, Mazee aliitaja sababu nyingine iliyowapa wakati mgumu wapinzani kuwa ni ubabe wa polisi dhidi ya wapinzani, hasa wakati wa kampeni.
Alisema ingawa polisi walijitahidi kulinda amani, wakati mwingine walikuwa wakikiuka taratibu za kazi zao.

Mazee alidai kuwa baadhi ya polisi walionyesha waziwazi kuwa wanafanya kazi zao kwa shinikizo la viongozi wa CCM, waliokuwa wakiwaamuru kuwashambulia wapinzani katika sehemu wanazoonyesha upinzani mkali dhidi ya CCM.

Alitoa mfano wa tukio la Alhamisi wiki iliyopita, ambapo polisi waliwatawanya wanachama na wafuasi wa CUF kwa mabomu ya machozi katika ofisi za chama hicho wilayani hapa.

Mazee alisema polisi walitumia nguvu kubwa kuwatawanya wanachama hao wa CUF kutokana na shinikizo la viongozi wa CCM, kutokana na hofu waliyokuwa nayo dhidi ya CUF.

Akizungumzia matokeo mabaya ya wapinzani katika uchaguzi huo, Mbunge wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya Chadema, Zitto Kabwe, naye alidai kuwa viongozi wa CCM wametumia mbinu mpya za kimafia kushinda uchaguzi huo.

Alisema tangu mwanzo viongozi hao wa CCM walibaini kuwa uwezekano wao wa kushinda iwapo taratibu zitafuatwa kama zilivyo, ni mdogo hivyo wakapanga njama kuwahujumu wapinzani.

Alidai kuwa katika mbinu hiyo mpya iliyobuniwa na chama hicho tawala, CCM iliwapeleka viongozi wakuu wa chama hicho vijijini.

Kabwe alieleza kushangazwa na kitendo cha Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, Makamu Mwenyekiti (Bara), John Malecela, viongozi wengine pamoja na wabunge kadhaa wa CCM, kuhamia vijijini ambako walipiga kambi kwa wiki kadhaa.

Alisema jambo hilo halijapata kutokea katika historia ya chama hicho.

Wakati huo huo, matokeo ya awali kutoka katika Kata ya Kalulu, yanaonyesha kuwa CCM imejizolea kura 536, wakati CUF imepata kura 362 na Chadema 29. Wagombea wa DP na UDP wamepata kura moja kila mmoja.

Jumla ya watu 2,545 walijiandikisha kupiga kura katika kata hiyo lakini watu 1,617 hawakupiga kura.

Katika Kata ya Kidodoma, waliojiandikisha walikuwa 3,483 na Chadema ikajipatia kura 41, CUF kura 795, CCM kura 1,190. Watu 1,450 hawakupiga kura. Katika Kata ya Ligoma anakotoka mgombea wa CCM, waliojiandikisha ni 4,325. Kati ya hao, Chadema ilijipatia kura 141, CUF (520), CCM (1,239) na watu 2,423 hawakupiga kura.

Matokeo kutoka Kata ya Lukumbule yanaonyesha kuwa kati ya watu 3,590 waliojiandikisha kupiga kura, Chadema imepata kura 78, CUF (615), CCM (862) na watu 2,026 hawakupiga kura. Katika Kata ya Matumba, waliojiandikisha ni 6,381 na Chadema ikajipatia kura 104, CUF (405), CCM (1,050) na wasiopiga kura ni 4,813.
Kutoka Kata ya Mbesa, inaonyesha kuwa waliojiandikisha walikuwa 6,652 huku Chadema ikijipatia kura 32, CUF (530), CCM (1,162) na watu 4,923 hawakupiga kura. Wakazi 3,468 wa Kata ya Mchesi nao walijiandikisha kupiga kura na kati yao 36 walimpigia kura mgombea wa Chadema, 593 walimchagua mgombea wa CUF huku CCM ikijizolea kura 1,015 wakati watu 1,820 wakiacha kupiga kura.

Katika Kata ya Mchoteka, watu 4,973 walikuwa wamejiandikisha kupiga kura na Chadema ikapata kura 47, CUF ilipata kura 765, CCM ikavuna 1,819 huku watu 2,334 wakishindwa kupiga kura.

Kutoka Kata ya Mindu, watu 4,008 walijiandikisha kupiga kura, na watu 116 walimpigia kura mgombea wa Chadema. Watu 293 walimchagua mgombea wa CUF wakati mgombea wa CCM alipata kura 1,075 na watu 2,517 hawakujitokeza kupiga kura.

Kata ya Msichele, watu 3,424 walijiandikisha na kati yao Chadema ilipata kura 109, CUF (379), CCM (1,002) na watu 1,926 hawakupiga kura.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
This article has been added to your 'Articles to Read' list.
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.