Na Manyerere Jackton, Dodoma
SERIKALI, kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, imetangaza vivutio vingi kwa vijana watakaojitokeza kujaza nafasi 3,500 za ualimu. Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Margaret Sitta, amesema hii ni nafasi pekee kwa vijana wenye sifa, kujitokeza kwa wingi kufaidika na fursa hiyo.
Sitta alikuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za Bunge mjini Dodoma . Maudhui ya mkutano huo yalikuwa kutoa ufafanuzi wa serikali kuhusu kuajiri walimu 3,500. Alisema mpango huo umeandaliwa kwa umakini wa hali ya juu, na kwamba walimu hao ambao watakuwa ni wahitimu wa sekondari na chuo kikuu, ni vijana makini na wenye uwezo. “Tusiseme kuwa huu ni UPE, mpango huu umeandaliwa kwa umakini, tutachukua vijana wenye uwezo waliofaulu kwa principal pass 2 katika masomo yanayofundishwa katika shule za sekondari,” alisema.
Sitta alisema katika kipindi cha mwaka 2004-2006, shule mpya za serikali 1,050 zilijengwa na kufanya idadi ya shule hizo nchini kufikia 1,699 kwa mwaka huu. Wanafunzi 147,000 mwaka 2003 waliingia kidato cha kwanza, na wanafunzi 243,359 waliingia kidato cha kwanza mwaka 2006. Alisema ongezeko la shule na wanafunzi limesababisha upungufu wa walimu 9,500.
Upungufu huo, alisema utaondolewa kwa kuajiri wahitimu wa stashahada 3,207 kutoka vyuo vya ualimu vya stashahada, 500 kutoka chuo kikuu na wastaafu 260 ambao wana utayari wa kufundisha. “Salio la walimu 3,500 wanahitajika kwa utaratibu maalumu wa mafunzo ya muda mfupi ya wiki nne kuanzia mapema Julai, 2006. “Kutokana na upungufu uliopo wa walimu 4,010, mkakati wa dharura kukabiliana na upungufu huo umeanzishwa, aidha, sera ya kupata walimu tarajali bado ipo pale pale,” alisema Sitta.
Sitta ametangaza sifa za vijana wanaotakiwa kujiunga na mpango huo. “Wahitimu wa kidato cha sita tangu mwaka 2001 hadi sasa ambao wamefaulu kwa kiwango cha principal pass 2 katika masomo yanayofundishwa sekondari.
“Wahitimu wa kidato cha sita ambao walishatuma maombi ya kujiunga na mafunzo ya stashahada wanaruhusiwa kuomba pia. Waombaji waliokwishatuma maombi kabla, watume maombi upya kwa wakuu wa vyuo vilivyo karibu nao. “Waombaji wenye sifa stahili wataomba kwenye vyuo vilivyo karibu na wanakoishi. Hii itasaidia kumpunguzia mwombaji gharama za usafiri na kumweka kwenye mazingira aliyozoea,” alisema Sitta.
Alisema mafunzo yataendeshwa katika vituo saba, na kwamba mwombaji apeleke barua katika chuo kilicho karibu na mkoa anakoishi. Yapelekwe kwa wakuu wa vyuo. Alitaja vituo hivyo na namba ya faksi kwenye mabano kuwa ni Tukuyu (Mbeya, Rukwa na Iringa, faksi 015 2552357); Mtwara (Ruvuma, Lindi na Mtwara, faksi 023 2333240), Morogoro (Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma, faksi 023 2603867), Korogwe (Tanga, Pwani na Kilimanjaro, faksi 027 2640999), Monduli (Manyara na Arusha, faksi 027 2538060), Tabora (Kigoma, Shinyanga, Singida na Tabora, faksi 026 2604939), na Butimba (Mwanza, Kagera na Mara, faksi 028 2550278). Maombi hayo yanatakiwa yawe yameshatumwa ifikapo Juni 27, 2006, ambako usaili kwa waombaji utafanyika Juni 31,2006.
Sitta alisema Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi itagharimia mafunzo, chakula na malazi. Alisema waombaji watarudishiwa nauli wakishafika chuoni. Usafiri wowote unakubalika, isipokuwa ndege na teksi. Watakaosafiri kwa treni watagharimiwa daraja la pili.
Pia alisema katika mafunzo hayo, wahitimu wa kidato cha sita waliofaulu kwa daraja la tatu kwenye masomo yanayofundishwa sekondari na ambao wako tayari kufundisha, watapewa fursa kuomba nafasi za mafunzo haya. Wawezeshaji watatoka vyuo vya ualimu, Taasisi ya Elimu Tanzania , Baraza la Mitihani, wakaguzi wa Elimu na wataalamu kutoka makao makuu ya wizara waliobobea katika masomo husika.
Sitta alizungumzia utaratibu wa mafunzo na kusema: “Kutakuwa na kiongozi mwezeshaji pamoja na moduli nne zenye kuzingatia utaalamu wa msingi wa kujifunzia na kufundisha, mwalimu na taaluma ya ualimu, ujana na shule, pamoja na uongozi wa shule kwa ajili ya mwalimu mwanafunzi. Moduli hizi zimeandaliwa ili kumwezesha mwalimu mwanafunzi kujisomea akiwa peke yake na kujadili na wenzake.
“Njia na mbinu shirikishi zitatumika katika kuendesha mafunzo haya ambazo zitamjengea mwalimu mwanafunzi uwezo wa kuwa mdadisi, kuthubutu na kushirikisha wanafunzi katika kufundisha. “Kazi ya mwezeshaji itakuwa ni kuwaelekeza walimu wanafunzi kushiriki kikamilifu katika mchakato mzima wa kujifunza. “Mafunzo haya yatajikita kwenye mbinu za kufundisha na kujifunzia, mwalimu na taaluma ya ualimu, ujana na shule na uongozi wa shule.” Alisema masomo hayo yanamwandaa mwalimu kujifunza, kufundisha na kujiamini.
Alisema walimu wanafunzi watakuwa chini ya uangalizi wa wataalamu ambao watasaidia kuwapa ushauri na maelekezo yanayostahili kuhusu kazi ya ualimu. “Baada ya kuhitimu mafunzo hayo, mwalimu atapewa ajira ya muda (kufundisha kwa leseni) kwa miaka miwili.
“Katika kipindi hiki cha kufundisha, mwalimu atajiunga na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ambako atapata mafunzo ya ualimu kwa ngazi ya diploma ya chuo kikuu au shahada kulingana na sifa zake za kidato cha sita,” alisema.
Sitta aliwataka wote watakaokwenda kwenye usaili, kubeba nguo na vifaa vyao muhimu, kwani wakipitishwa, hawatakuwa na muda wa kurejea makwao kuchukua vitu hivyo. “Waje kabisa na mabegi ya nguo zao, watakaochaguliwa wataingia katika mafunzo mara moja,” alisema.
Kutoka: Tanzania Daima