*Ni aliyemwita mtanzania 'sokwe mweusi'
*Bosi wake toka Afrika Kusini akerwa naye
Na Mwandishi Wetu
SUALA la kudhalilishwa kwa Mtanzania, mtumishi wa mradi wa ujenzi wa minara pacha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) limeingia sura mpya, baada ya makao makuu ya Kampuni ya Group Five International kumrejesha Afrika Kusini ofisa wake, Ruan Kidson aliyehusika na kashfa hiyo.
Makao makuu ya kampuni hiyo, yamefikia uamuzi huo ambao ulitangazwa jana jijini Dar es Salaam baada ya awali kumsimamisha kazi Kidson aliyemfananisha Mtanzania Pius Masekesa na sokwe mweusi.
Uamuzi huo ulifikiwa wakati wa kikao baina ya Meneja Raslimali Watu wa Group Five International, Conrad La Grange kutoka Afrika Kusini na viongozi wa wafanyakazi wa mradi huo.
Wiki iliyopita, gazeti hili liliandika taarifa za raia huyo wa Afrika ya Kusini kumfananisha Masekesa na sokwe mweusi, huku akimwonyesha picha za mfanyakazi anayeteswa.
Grange ambaye aliwasili nchini Alhamisi wiki iliyopita, akiwa ametumwa na uongozi wa juu wa Group Five International, alikuwa na jukumu la kufuatilia kadhia hiyo.
Katika kikao hicho, Grange alipitia ushahidi uliotolewa na mlalamikaji (Masekesa) na utetezi wa Kidson kabla ya kukubaliana na uamuzi wa kumsimamisha kazi.
Habari zaidi kutoka katika kikao hicho zinasema, Grange alikieleza kikao hicho kuwa Group Five International imesikitishwa na kitendo hicho cha Kidson na kwamba ni nia ya kampuni yake kujenga uhusiano mwema na wafanyakazi wake sehemu yoyote duniani.
Awali, uongozi wa kampuni hiyo ulimwandikia barua Gavana wa BoT, Dk Daudi Balali, ukimtaka aruhusu uchunguzi wa suala hilo kwa maelezo kuwa lilikuwa likichafua jina la Group Five International.
"Hata Grange alitumwa kuja nchini ili kutafuta wanasheria ambao wangeshughulikia wale wote waliochafua jina la kampuni kwa kuandika na kudai Kidson kamfananisha Mtanzania na sokwe mweusi," mmoja wa viongozi wa kampuni hiyo aliiambia Mwananchi.
Hata hivyo, habari kutoka BoT na kampuni hiyo zinasema Grange alilazimika kukubaliana na uamuzi wa uongozi wa Group Five International, tawi la Tanzania wa kumsimamisha kazi Kidson baada ya kupitia ushahidi wote uliokusanywa.
Wakati Kidson akifungishwa virago na kurejeshwa kwao, ushahidi mwingine ambao gazeti hili limeupata unaonyesha jinsi ambavyo baadhi ya wafanyakazi wazawa ambao wamekuwa wakinyanyaswa, kufukuzwa kazi bila ya utaratibu kufuatwa, hasa wanapotoa taarifa hizo kwenye vyombo vya dola.
Miongoni mwa waliokumbwa na uonevu huo ni Emmanuel Mawazo Tweve, aliyetimuliwa kazi mwaka jana baada ya kuwasilisha malalamiko ya kutukanwa na kutishiwa kupigwa na nondo kulikofanywa na kiongozi wake, mmoja ambaye jina lake tunalihifadhi kwa sasa.
Baada ya Tweve kufungua malalamiko katika kituo kidogo cha polisi kilichoko Mtaa wa Shaaban Robert, eneo la Gymkhana jijini Dar es salaam, alishauriwa kufuta shauri hilo na viongozi wake, lakini baada ya siku tatu alitimuliwa kazi.
Barua ya kumfukuza kazi Tweve ilidai kuwa alikuwa ni mwajiriwa wa mdomo, yaani aliyeajiriwa bila ya mkataba wa maandishi, jambo ambalo ni kinyume na ajira yake.
Uchunguzi wa gazeti hili unaonyesha kuwa Tweve aliajiriwa na kampuni hiyo Agosti Mosi 2004 kwa mkataba rasmi.
Lakini, barua ya kumfukuza kazi iliyoandikwa Septemba 11, mwaka jana, ikiwa ni siku moja baada ya kufuta malalamiko ya kutishiwa kupigwa nondo, ilieleza kuwa mkataba wake wa ajira (oral Contract) ulikuwa umesitishwa na kwamba alitakiwa kulipwa madai yake kulingana na taratibu zilizopo.